HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 21 February 2019

MICHEZO YA MAJESHI KUANZA KUTIMUA VUMBI JUMAMOSI HII

*Wananchi waombwa kujitokeza kwa wingi kujipatia burudani kutoka kwa vyombo vyao vya ulinzi

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
VYOMBO vya ulinzi na usalama kupitia Baraza la Michezo ya Majeshi ya Tanzania (BAMMATA) wameandaa michezo ya majeshi yenye kauli mbiu ya “ Michezo ni Kazi na Mshikamano” yatakayofanyika jijini Dar es salaam katika viwanja vya Uhuru kuanzia Jumamosi ya tarehe 23 na kuhitimishwa Machi 9 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) Brigedia Jenerali Suleiman Mzee amesema kuwa lengo la kufanya mashindano hayo ni kuendeleza uhusiano, urafiki na undugu baina ya majeshi ya ulinzi, usalama na idara maalumu za Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na wananchi, kuibua na kuinua vipaji, kuendeleza na kudumisha sera ya taifa  ya michezo katika majeshi ya ulinzi na usalama na kuendeleza elimu ya viungo na utimamu wa mwili katika majeshi.

Brigedia Jenerali Mzee amesema kuwa mashindano hayo yatafunguliwa  rasmi siku ya jumamosi na Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na kufungwa rasmi Machi 9 mwaka huu na Waziri mwenye dhamana ya Ulinzi na Jeshi la kujenga taifa Dkt. Hussein Ali Mwinyi na baadaye kufuatiwa na hafla ya chakula cha jioni ambapo Waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo Dkt. Harrison Mwakyembe anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Akieleza washiriki wa mashindano hayo Brigedia Jenerali Mzee amesema kuwa timu zitakazoshiriki ni kutoka Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania, vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Jeshi la Polisi, Jeshi la kujenga taifa, Idara ya uhamiaji, Magereza na zima moto huku michezo inayotarajiwa kushindaniwa ni pamoja na mpira wa pete(kwa wanawake,) mpira wa miguu (kwa wanaume,) mpira wa mikono (kwa wanawake na wanaume,) mpira wa wavu (kwa wanawake na wanaume,) mpira wa kikapu(kwa wanawake na wanaume,) ndondi kwa wanaume, kulenga shabaha (kwa wanawake na wanaume) na riadha kwa wanawake na wanaume.

Pia amewaalika wakazi wa jiji la Dar es salaam na Mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya michezo hiyo ili kuweza kujipatia burudani safi kutoka kwenye vyombo vyao vya ulinzi na usalama pamoja na kujipatia fursa ya kuimarisha uelewano, urafiki na ushirikiano baina yao na vyombo vinavyowalinda.

Michezo hii ilianza rasmi mwaka 1997 ikihusisha  Brigedia na vikosi vya jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania pekee na mwaka 1984 kwa mara ya kwanza michezo hiyo ilianza kuwashirikisha washiriki wengine nje ya JWTZ waliojulikana kama kanda.
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA) Brigedia Jenerali Suleiman Mzee akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na michezo itakayoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama, mashindano yanayotarajiwa kuanza kutimia vumbi jumamosi hii katika viwanja vya uhuru, jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad