HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 1 February 2019

MAHAKIMU MAHAKAMA ZA MWANZO, WAJUMBE MABARAZA YA KATA WAPIGWA MSASA

MAHAKIMU wa Mahakama za Mwanzo na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata katika Wilaya za Nyamagana na Ilemela wametakiwa kutambua mipaka na majukumu yao ya usimamizi wa haki ili kuleta suluhu na kupunguza migogoro kwenye vyombo vya juu vya kutoa haki kwa jamii.

Pia watendaji wa kata, mitaa, vijiji na vitongoji wameonywa na kutakiwa kuacha kupora majukumu ya mabaraza ya kata kwa kusilikiza mashauri na kuyatolea maamuzi, kwani wanakiuka kwa kuwa mabaraza yapo kwa mujibu wa sheria.

Rai hiyo ilitolewa jana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Jaji Sam Rumanyika wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo mahakimu na wajumbe hao wa mabaraza ya kata yaliyoandaliwa na Chuo cha  Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).

Alisema mafunzo hyo ni utekelezaji wa agizo la  Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Hamis Juma baada ya ziara yake mkoani Tabora mwaka jana, alipokea malalamiko ya utendaji usioridhisha wa Mabaraza ya Kata na alishuhudia maamuzi mengi ya mabaraza hayo kutothibitishwa na Mahakama za Mwanzo kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji wake.

Alisema kutokana na uwezo wa mabaraza hayo katika kutatua migogoro kuwa bado ni kizungumkuti (changamoto) na sababu ya kutowezeshwa katika hali ya uelewa na mazingira, alielekeza zifanyike juhudi za kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata juu ya majukumu ya mabaraza, mamlaka husika kuyalinda ili kuimarisha mfumo wa utoaji haki.

“Mabaraza ya Kata kazi yake ni kutoa uamuzi wa mashauri ya jinai na madai yaliyoanishwa na adhabu zake ni ndogo, lakini yamewekwa kando na wasimamizi (serikali za mitaa).Kwa kuwa yapo kisheria katika muundo wa kutoa haki,yawezeshwe kimiundombinu, vitendea na uelewa wa mambo,”alisema Jaji Rumanyika.

 Aliongeza kuwa ; “Inasikitika kuona mpangilio wa majalada hasa ya ardhi, muundo na ujengaji wa hoja katika kufikia maamuzi na si wingi wa migogoro.Faraja ni lengo la sheria ya mabaraza inayolenga kudumisha suluhu na kupunguza mashauri ikizingatiwa asilimia 70 yanafunguliwa kila siku.Ni imani yangu mabaraza yakijengewa uwezo yatapunguza mzigo na nafuu itapatikana kwenye vyombo vingine.”

Jaji Rumanyika alidai licha ya mabaraza ya kata kuwepo kisheria yameharibiwa na kimsingi utendaji wake si mbaya sana, si mbaya, kutokana na uwezo usioridhisha wa kutatua migororo kwa jinsi rekodi za maamuzi yao zilivyo, hivyo yakiwezeshwa yatakuwa na sura nzuri.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha IJA, Taaluma, Tafiti na Ushauri Fahamu Mtulya alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata kubadilisha uzoefu katika changamoto za utoaji haki na kuzitatua.

Alisema kuwa imedhihirika kuwepo kwa changamoto nyingi kwenye mabaraza hayo na hivyo chuo kiliona umuhimu wa kutoa mafunzo ya uwezeshaji ya kuwajengea uwezo wajumbe wa mabaraza hayo na mahakimu ili kupunguza ama kuondoa changamoto hizo ambazo zimekuwa nyingi nchini.

“Utendaji wa mabaraza hayo si mzuri kwa mujibu wa utafiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria hasa mabaraza ya ardhi ambapo Jaji Mkuu Profesa Juma akiwa tabora alipokea malalamiko mengi na maamuzi yanayotolewa hayazingatii maadili na mienendo ya utumishi,”alisema  Mtulya.

Alisema kuwa si wote wanafahamu mamlaka zao ( mahakimu na wajumbe wa mabaraza) hivyo chuo kiliamua kubeba jukumu la kuwaelimisha na kuwaunganisha ili wajione ni wasimamizi wa haki nchini.

Alieleza kuwa nia na lengo la mabaraza ni kufanya usuluhishi wa migogoro midogo midogo ili jamii iishi salama kwa amani zaidi, hivyo baada ya kupata mafunzo (elimu) hayo mahakimu na wajumbe wa mabaraza ya kata watakuwa mabalozi wa utoaji haki isiyo na shaka.

Kwa mujibu wa Mtulya wanalenga kuwakumbusha muundo na ukomo mamlaka ya Mahakama za Mwanzo, muundo wa Mabaraza ya Kata,mashauri katika mahakama hizo,namna ya kusuluhisha mashauri kwenye mabaraza ya kata na mamlaka ya usimamizi ya Mahakama za Mwanzo kwenye mabaraza hayo .

“Zipo sheria zinawapa mamlaka wajumbe wa mabaraza ya kata kusikiliza baadhi ya mashauri na kuyatolea maamuzi pia kuna sheria mahakimu wanapewa mamlaka ya kuwasimamia wajumbe wa mabaraza ya kata.Pia yapo aina ya mashauri yanayotakiwa kusikilizwa na Mahakama za Mwanzo na mabaraza yana ukomo wa kazi zao pia,”alifafanua Mtulya
 Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi Lushoto (IJA), Taaluma, Tafiti na Ushauri Fahamu Mtulya akizungumza na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo pamoja na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata wa Wilaya za Nyamagana na Ilemela (hapo pichani) wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika juzi jijini Mwanza.Kutoka kulia wa pili ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Jaji Sam Rumanyika na kulia ni Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Kingwele Omari na kushoto ni Mhadhiri wa IJA Dk. Alexander Saba.
 Kaimu MKuu wa Chuo cha Uongozi Lushoto (IJA),Taaluma, Tafiti na Ushauri Fahamu Mtulya akisistiza jambo kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wa Wilaya za Nyamagana na Ilemela na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata (hawapo pichani) kutoka kwenye wilaya hizo mbili wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo.Mtulya aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. 
 Wajumbe wa Mabaraza ya Kata wakiwa pamoja na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Jaji Sam Mpaya Rumanyika, wa tatu kutoka kulia.Wa pili kutoka kushoto ni Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi Lushoto (IJA) Fahamu Mtulya na wa pili kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Mwanza Kingwele Omari.Kushoto ni Mhadhiri wa IJA Dk. Alexander Saba.
 Mgeni rasmi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo pamoja na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Mwanza, Jaji Sam Mpaya Rumanyika (wa tano kutoka kulia) wakiwa katika picha ya pamoja, wanne kutoka kushoto ni Kaimu Mkuu wa Chuo cha IJA Fahamu Mtulya, wa tatu kushoto ni Mhadhiri wa chuo hicho Dk. Alexander Sana na wa nne kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Mwanza  Kingwele Omari.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi Lushoto (IJA), Taaluma, Tafiti na Ushauri Fahamu Mtulya akihojiwa na waandishi wa habari kuhusu mkakati wa chuo hicho kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na Wajumbe wa Mabaraza ya Kata yatakayowawezesha kutimiza wajibu na majukumu yao kwa weledi. Picha zote na Baltazar Mashaka

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad