HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 12, 2019

KTO YAPONGEZWA KWA KUCHANGIA JITIHADA ZA SERIKALI KWENYE VYUO VYA MAENDELEO YA WANANCHI

Na Francis Daudi, Blogu ya jamii
MAFUNZO ya uwezeshaji kwa wakufunzi wa walimu wa elimu ya awali kutoka Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi yaliyoandaliwa na shirika lisilo la Kiserikali la Karibu Tanzania Organization (KTO) yamehitimishwa.

Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo hayo,  Mkurugenzi wa Elimu ya mafunzo ya ufundi (TVET) Dkt. Noel Mbonde  amesema, kuwa Serikali inaunga mkono jitihada zinazofanywa na taasisi hiyo ya Karibu Tanzania Organization na kwamba miradi ya namna hiyo na kueleza kuwa yanayofanywa na shirika hilo ni sehemu ya mipango ya Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi kwa kuwa Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi vina nafasi kubwa katika kulipeleka taifa katika uchumi wa viwanda.

Aidha, Serikali  imeahidi kushirikiana na KTO katika shughuli wanazozifanya ambazo zina malengo ya kuchangia jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwenye kuviimarisha Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi ili viwe na  tija kubwa kwa vijana wengi wenye kutokea kwenye familia za  Watanzania wenye vipato duni.  

Baadhi ya miradi ambayo taasisi ya KTO inashirikiana na wizara ni pamoja na ‘Elimu Haina Mwisho’ ambayo ni programu ya kuwapatia maarifa na ujuzi wanawake vijana waliokosa fursa  hiyo  kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ndoa za utotoni, ukeketaji na kupata ujauzito wakiwa shuleni. Vilevile, KTO inaendesha programu ya ‘ Mpira Fursa’ inayohusika na kuendeleza mpira wa wanawake na hapa nchini ambapo mafunzo hutolewa katika Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi na Wanawake vijana wanaopata programu ya ‘ Mpira Fursa’ hawajifunzi kucheza mpira pekee, bali pia kupata mafunzo na ujuzi mwingine.

Dr. Mbonde ameongeza kusema,   kuwa KTO imekuwa kiungo muhimu katika Vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi nchini na Wizara pamoja na wahisani wa Kimaendeleo kama SIDA,( Sweden) HDIF ( Uingereza) na Mastercard Foundation ( Canada) na wengineo wamekuwa bega kwa bega na KTO pamoja na kushiriki katika kuboresha utolewaji wa Mafunzo ndani ya Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi.


Pia ametoa mwito kwa vyuo vyote vilivyopata vifaa hivyo kuvitunza na kuvitumia kwa malengo tarajiwa na kusisitiza kuwa vifaa hivyo vitumike na kuleta manufaa kwa wengi zaidi na 
mafunzo hayo waliyoyapata yawe sehemu muhimu katika kuandaa walimu ambao watawafundisha watoto ambao kwa miaka ijayo ndio hasa watakuwa nguvu kazi ya Taifa.

"Kwa niaba ya Wizara na Serikali niwashukuru tena wadau wengine wa Maendeleo kama vile HDIF, Aflatoun International na SIDA kwa kuendelea kusaidia Programu za namna hii ambazo ni chachu katika kuleta maendeleo nchini" Alisema Dr. Noel Mbonde.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi wa taasisi ya KTO  Ndugu Maggid Mjengwa amesema kuwa taasisi hiyo itaendelea kutoa mafunzo pamoja na vitendea kazi katika kuhakikisha azma ya kulipeleka taifa kwenye uchumi wa kati linafikiwa.

Mjengwa amesema kuwa baada ya mafunzo hayo ya siku kumi, taasisi imetoa vifaa ambavyo vitawasaidia wawezeshwaji katika kutekeleza majukumu yao. Vifaa  hivyo ni pamoja na kompyuta 10 zenye thamani ya shilingi milioni 7, External hard driver 10 ambazo zina programu za kufundishia watoto kama vile Ubongo kids zenye thamani ya shilingi milioni 2.8, projector 20 zenye thamani ya shilingi milioni 18  pamoja na vitabu vya elimu ya awali vyenye thamni ya shilingi milioni 5.2.

Mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka nchini Uholanzi Chiara Massaroni amesema kuwa mafunzo hayo ya awali yana tija hasa katika ukuaji watoto na ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kutoa ushirikiano.

 Mkurugenzi wa taasisi ya Karibu Tanzania Organization (KTO) Maggid Mjengwa (aliyesimama) akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo na kuwasisitiza wawezeshwaji kutumia maarifa na vifaa walivyopata katika kuleta mandeleo.
 Mkurugenzi wa Elimu ya mafunzo ya ufundi (TVET) Dkt. Noel Mbonde akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyoandaliwa na taasisi ya KTO ambapo alihaidi kuwa ushirikiano baina ya Taasisi hiyo na Serikali utazidi kudumishwa.
Viongozi wa taasisi ya KTO wakiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo yaliyochukua takribani siku kumi za kuwajengea uwezo wakufunzi hao kutoka Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad