HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, February 6, 2019

DKT. KIJAJI - UTARATIBU UFUATWE ILI KUFUNGUA KITUO CHA FORODHA MANDA

Na Saidina Msangi, WFM, Dodoma
Serikali imemtaka Mbunge wa Ludewa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Njombe kuandaa andiko la kuwasilisha Serikalini katika hatua ya kufungua Kituo kipya cha forodha katika bandari ya Manda iliyopo katika Ziwa Nyasa.

Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, Bungeni Jijini Dodoma, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Ludewa Mhe. Deogratias Ngalawa, aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanzisha Kituo cha Forodha katika bandari ya Manda, ili kurahisisha huduma kwa wananchi wanaokwenda nchi jirani hasa kwa shughuli za biashara.

Dkt. Kijaji alisema kuwa, utaratibu wa kufungua kituo kipya cha forodha unatakiwa kuzingatia Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2004, ambayo inaitaka nchi mwanachama kuwasilisha kwenye Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki maombi ya idhini ya kuanzisha kituo kipya cha forodha na hatimaye kutangazwa kwenye gazeti la Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kupata nguvu ya kisheria.

“Mchakato wa ndani wa kuwasilisha maombi ya kufungua kituo kipya cha forodha unaanza katika ngazi ya mkoa ambapo mkoa unatakiwa kuwasilisha maombi ya kufungua kituo kipya cha forodha katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki”, alisema Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa baada ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kujiridhisha itamfahamisha Kamishna Mkuu Mamlaka ya Mapato Tanzania ili kufanyia kazi maombi husika kwa kuzingatia sheria ya forodha ya afrika ya mashariki na hatimaye kuwasilisha maombi hayo kwenye sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad