HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, January 18, 2019

WAZIRI MKUU AIAGIZA NHC KUONGEZA NGUVUKAZI KATIKA UJENZI WA MJI WA SERIKALI

Na Farida Ramadhani na Peter Haule - Dodoma
 Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa, amemuagiza Mkandarasi anayesimamia ujenzi wa Ofisi mpya ya Wizara ya Fedha na Mipango kutoka Shirika la Nyumba la Taifa, kuhakikisha anaongeza rasilimali watu ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa .

Majaliwa, ametoa agizo hilo wakati wa  ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi mbalimbali za Wizara katika mji wa Serikali eneo la Ihumwa Jijini Dodoma. Alisema kuwa  zimebaki siku 21 pekee kukamilisha ujenzi huo na  lengo la Serikali ni kuona kazi hiyo imekamilika ifikapo Januari 31 mwaka huu, na akaonesha hofu yake iwapo ujenzi utakamilika kwa wakati kwa kuwa hakulidhishwa na nguvu kazi iliyopo.

“Mimi ninapokuta watu wachache huku kukiwa na kazi zisizohitaji kusubiri siku mbili kama kazi ya kuweka bimu, natarajia kuona watu wangekuwa wanaendelea kufanya kazi hizo”, alisema . Aidha alisema kuwa Mawaziri kutembelea ujenzi unaoendelea na kuona ubora wa jengo ni  jukumu lao na wanauwezo wa kuonesha kuridhika au kutoridhika na ujenzi huo.

Ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu kuhakikisha mazingira ya eneo la Wizara linapandwa miti  kulingana na ramani ya majengo ya muda na yakudumu. Alisema kama watumishi waliopo ni wachache mkandarasi aongeze vijana ili ujenzi ukamilike mapema kwa kuwa kuna mafundi wengi Mkoani Dodoma na nje ya mkoa huo wanaotafuta kazi.

Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameahidi kusimamia maagizo ya Waziri Mkuu na kuhakikisha jengo linakamilika kwa wakati kwa kuwa hadi sasa asilimia 95 ya vifaa vyote muhimu vya ujenzi vimenunuliwa.

Akizungumzia suala la kuongeza nguvu kazi, Dkt. Kijaji, amesema Wizara itahakikisha Mkandarasi anaongeza nguvu kazi kwa haraka  kutoka mtaani au Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili ifikapo Januari 31 Wizara ikabidhiwe jengo rasmi. Dkt. Kijaji alieleza kuwa Wizara ipo tayari kuhamia katika jengo hilo Februari mosi mwaka huu.

Naye Mhandisi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Elisante  Olomi, anayesimamia ujenzi wa ofisi za Wizara hiyo, amesema ujenzi unaendelea vizuri na mpaka sasa umekamlika kwa asilimia 75, huku akiahidi kuongeza mafundi wakutosha kwa kuwa wapo wengi na wamekuwa wakiomba kazi katika maeneo hayo ya ujenzi. 
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akitoa maagizo ya ukamilishwaji wa Ujenzi wa ofisi ya Wizara ya fedha na Mipango katika Mji wa Serikali, Ihumwa Dodoma, kwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Ashatu Kijaji (wa pili kushoto), alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo.
 Mhandisi Elisante Olomi kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (hayupo pichani) namna ujenzi wa Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango unavyoendelea, Ihumwa Jijini Dodoma.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (katika), akiendelea na ukaguzi katika  eneo la mji wa Serikali Ihumwa Jijini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (kulia), akizungumza jambo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Suzan Mkapa, katika ujenzi wa Ofisi za Wizara hiyo unaoendelea, Ihumwa Jijini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala wa Wizara ya Fedha na Mipango, Alfred Dede (wa pili kushoto) akitoa maelezo ya mipaka ya eneo la Wizara hiyo  kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (kulia), katika Mji wa Serikali  Ihumwa Jijini Dodoma, wa kwanza kulia ni Naibu Katibu Mkuu Bi. Suzan Mkapa na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bi. Grace Sheshui wa Wizara hiyo.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad