HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 4 January 2019

WAZIRI LUGOLA ATAKA ASKARI WAPANDISHWE VYEO, WAREKEBISHIWE MISHAHARA, WALIPWE FEDHA ZA UHAMISHO NA LIKIZO

Na Mwandishi Wetu, MOHA-Karagwe.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewataka viongozi Wakuu wa Jeshi la Polisi nchini wahakikishe wanawapandisha vyeo pamoja na kuwarekebishia mishahara askari wote wanaostahili.
Lugola amesema kuna idadi kubwa ya askari wanaostahili kupandishwa vyeo na kurekibishiwa mishahara hivyo askari hao wana haki kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Askari na Watumishi wa Wizara yake, mjini Missenyi na Karagwe Mkoani Kagera, leo. Lugola alisema alitoa agizo kuwa ifikapo  mwezi Agosti mwaka jana agizo hilo liwe limefanyiwa kazi, lakini mpaka umefika mwaka mpya bado halijafanyiwa kazi.
“Kwanini bado hamjapanda vyeo na kubadilishiwa mishahara yenu mpaka sasa wakati nilishatoa maelekezo mpandishwe, nitahakikisha nalifuatilia hili mapema zaidi ili nijue tatizo ni nini.” Alisema Lugola.
Pia Lugola alizungumzia kuhusu ukosefu wa nyumba za makazi ya askari, kuwa licha ya Rais Dkt. Magufuli anatoa mchango mkubwa kwa kulisaidia Jeshi, lakini bado kuna upungufu mkubwa wa nyumba hizo.
“Pamoja na fedha kidogo tunazopata lakini bado tuna tatizo la ukosefu wa makazi wa nyumba za askari, lakini bado Serikali inatafuta fedha ili kuhakikisha changamoto hiyo inaisha,” alisema Lugola.
Pia lugola alisema changamoto nyingine inayowakabili askari wa vyombo vyake ni kutopata fedha za kuhamishwa na atahakikisha madai yote ya askari hao yanafanyiwa kazi. Lugola alisema jambo ambalo linamuumiza kichwa ni kuhusu madai ya askari na watumishi wa wizara yake ambayo anasema kama wafanyakazi hawatalipwa haki zao na utendaji wa kazi utapungua.
Waziri Lugola yupo mkoani Kagera kikazi na jana alimaliza ziara Wilaya ya Bukoba, na leo anaanza ziara Wilaya ya Misenyi, inafuata Karagwe, Kyerwa, Ngara, Biharamulo na Januari 8, 2019 atamalizia ziara yake Wilaya ya Muleba ambapo katika Wilaya hizo pia atazungumza na wananchi pamoja na watumishi waliopo ndani ya Wizara yake ambao ni Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Magereza, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Idara ya Probesheni ambayo jukumu lake kuu ni kupunguza msongamano gerezani na kusimamia wafungwa waliopewa adhabu mbadala na Mahakama au wafungwa waliopata msamaha kupitia sheria ya huduma kwa jamii na kutumikia kifungo chao nje ya Gereza.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto), akimsalimia Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, Wallace Mashanda, wakati alipokuwa anawasili Makao Makuu ya Wilaya hiyo, leo. Katikati ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Luteni Kanali Denice Mwila. Lugola katika kikao chake na Baraza la Askari wilayani humo, aliwataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wahakikishe wanawapandisha vyeo pamoja na kuwarekebishia mishahara askari wote wanaostahili. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera, Luteni Kanali Denice Mwila akimfafanulia jambo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (katikati), katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, kilichofanyika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya huyo, leo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto), akizungumza katika kikao cha Baraza la Askari na Watumishi wa Wizara yake, katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera, jana. Katika hotuba yake Waziri Lugola aliwataka Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake wahakikishe wanawapandisha vyeo pamoja na kuwarekebishia mishahara askari wote wanaostahili. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera. Lugola aliwataka wananchi wa mji huo wahakikishe wanafuata sheria za nchi kwa kuwa nchi ipo salama. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Wilayani humo, Balozi Dkt. Deodarus Kamala, ambaye alipandishwa jukwaani na Waziri huyo ili aweze kuzungumza na wananchi. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad