HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 8 January 2019

WAFUGAJI WATAKIWA KUACHANA NA KUHAMAHAMA

Jamii ya wafugaji imetakiwa kuhakikisha watoto wao wanajiunga na shule za msingi na sekondari, mara baada ya kufunguliwa wiki hii na kuachana na mtindo wa kuhamahama na mifugo. Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Jackson Sipitieck ameyasema hayo wakati akimsimika Diwani wa Kata ya Naisinyai Kilempu Ole Kinoka kuwa kiongozi wa kimila (Laigwanani) wa Jumuiya ya Kishapuy. 

Sipitieck alisema jamii ya wafugaji inatakiwa kubaki eneo moja kusomesha watoto wao na kuachana na maisha ya kuhamahama na watoto wao ili kutafuta malisho ya mifugo. "Hivi sasa serikali imewekeza miundombinu bora kwenye elimu hivyo jamii ya wafugaji inapaswa kutumia fursa hiyo kwa kusomesha watoto," alisema. 

Hata hivyo, alisema wilaya hiyo imejipanga kuhakikisha wanafunzi wapya wa shule za msingi na sekondari wanapata nafasi kwa kuongeza vyumba vya madarasa. Ole Kinoka akizungumza baada ya kusimikwa ameomba ushirikiano kwa viongozi na jamii kwa ujumla ili aweze kutumikia vyema nafasi hiyo. 

Ole Kinoka alisema uwazi pia ni mzuri kwenye uongozi wake kwani atakuwa anapokea changamoto na utendaji kazi unavyofanyika ili kuhakikisha jamii hiyo inaendelea kushirikiana. Alisema heshima aliyopewa ya kuwa diwani wa kata ya Naisinyai na kiongozi wa kimila wa jamii ni kubwa, hivyo atahakikisha anatumikia nafasi hizo kwa uhadilifu mkubwa na unyenyekevu. 

"Pia tutahakikisha jamii nyingine zaidi ya wamasai wanajiunga kwenye jumuiya yetu ya Kishapuy ikiwemo wameru, wachaga, waarusha na wengineo," alisema Ole Kinoka. Katibu wa Jumuiya ya Kishapuy, Peter Peshut, alisema jumuiya yao ni muunganiko wa mababu waliozaliwa na bibi mmoja aliyekuwa mlemavu wa macho. 

Peshut alisema jumuiya ya Kishapuy ina wanachama 360 wa wilaya ya Simanjiro na Longido mkoani Arusha. Alisema jumuiya hiyo inafanya kazi na serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali, mashirika ya kidini na mengineyo kwa lengo la kuboresha maisha ya jamii. Mtoto wa Ole Kinoka, Martha Kilempu akizungumza baada ya kutoa zawadi kwa baba yao alisema japokuwa mzazi wao ni kiongozi wa kijamii pia anaongoza familia yao. 
 Diwani wa Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Kilempu Ole Kinoka akizungumza baada ya kusimikwa kuwa kiongozi mkuu wa kimila (Laigwanani) wa jamii ya Kishapuy. 
 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Jackson Sipitieck (kulia) wakishuhudia ngoma ya jamii ya wamasai wakati wa kusimikwa kwa Diwani wa Kata ya Naisinyai Kilempu Ole Kinoka (wapili kulia) kuwa kiongozi wa kimila (Laigwanani) wa jamii ya Kishapuy. 
 Diwani wa Kata ya Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Kilempu Ole Kinoka akikabidhiwa katiba ya jamii ya Kishapuy na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Jackson Sipitieck baada ya kusimikwa kuwa kiongozi wa kimila (Laigwanani) wa jamii hiyo. 
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Jackson Leskary Sipitieck akizungumza baada ya kumsimika Diwani wa Kata ya Naisinyai, Kilempu Ole Kinoka kuwa kiongozi wa kimila (Laigwanani) wa jamii ya Kishapuy. 

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad