HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, 20 January 2019

UWT ZANZIBAR YAZINDUA KAMATI NNE ZA KUCHAPA KAZI KUELEKEA 2020

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi(UWT) Tanzania kwa upande wa Zanzibar, leo umezindua rasmi kamati ndogo ndogo nne zitakazokuwa na majukumu mbali mbali ya kufanisha kwa ufanisi kazi za umoja huo kwa mwaka 2019/2020.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Kisasi alizitaja kamati zilizozinduliwa kuwa ni pamoja na Kamati ya Uchumi, Mipango na Fedha, Kamati ya Mawasiliano kwa Umma, Kamati ya Elimu,Malezi na Mafunzo pamoja na Kamati ya Mahusiano na Taasisi za Wanawake ndani na nje ya Nchi.

Alisema kuwanzishwa kwa kamati hizo ni matarajio makubwa zaidi ni kuwafikia Wanawake  na Vijana pamoja na makundi mbali mbali yaliyopo katika jamii na watoto ili kushinda Uchaguzi ujao mwaka 2020.

Katika maelezo yake Makamu Mwenyekiti huyo aliwasisitiza Wajumbe wote wa Kamati hizo kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika utekelezaji wa majukumu ya msingi ya UWT pamoja na CCM kwa ujumla.

“Wanawake ni Jeshi kubwa tena la ukombozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi, nasaha zangu kwenu ni kwamba tutumie nafasi hii kuhakikisha tunawafikia wanawake wote hasa waliopo Vijijini na Pembezoni kwa nia ya kuwaweka karibu na kufanya nao shughuli zetu za kisiasa.

Pia Wanawake wa UWT lazima tupate Sauti zetu kila mmoja kwa nafasi yake ndani ya Umoja Wetu kuyasema mambo mema yanayotekelezwa na CCM chini ya Viongozi wetu Wakuu ambao ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli wanaoendelea kusimamia kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.”, alisema Makamu Mwenyekiti Thuwayba Kisasi.

Aliwataka Wanawake nchini kushirikiana katika malezi ya Watoto ili waweze kukuwa wakiwa katika malezi na maadili bora yatakayowasaidia kupambana na changamoto za mmomonyoko wa maadili.

Awali akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Tunu Juma Kondo , alieleza kuwa UWT imejipanga kufanya kazi zake Kisayansi zaidi kwa lengo la kufanikisha kwa wakati malengo waliyojiwekea ndani ya Umoja huo.

Aidha alifafanua kuwa Kamati hizo zilizozinduliwa zitakuwa ni chachu ya kubuni miradi mipya ya kiuchumi itakayoongeza kipato ndani ya UWT pamoja na kupatikana fursa ya mahusiano mazuri na Taasisi mbali mbali za Wanawake Duniani.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati tekelezaji WUT Taifa Lucy  Mwakembe alisema Umoja huo utaendelea kupanga mikakati mbali mbali ya kimaendeleo ili kujiinua kiuchumi.
 BAADHI ya Wajumbe wa Kamati ndogondogo za UWT Zanzibar zilizozinduliwa leo wakiwa katika Kikao cha Awali cha utambulisho wa Kamati hizo, huko Afisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui.
 -MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa Thuwayba Kisasi akizungumza na Wajumbe wa Kamati ndogo ndogo za Umoja huo mara baada ya kuzinduliwa.
 NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Tunu Juma Kondo akitoa ufafanuzi wa majukumu mbalimbali ya Kamati hizo ambazo ni nne zilizozinduliwa kutokana na Matakwa ya Kanuni ya Umoja huo.
Picha ya Pamoja ya Wajumbe wote wa Kamati Nne za UWT zilizozinduliwa.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad