HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 28, 2019

UTUNZAJI MAJALADA YA ARDHI CHAMWINO WAMVURUGA NAIBU WAZIRI MABULA

Na Munir Shemweta, DODOMA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekasirishwa na jinsi halmashauri ya wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma inavyotunza majalada ya Ardhi katika halmashauri hiyo.

Dkt Mabula alikutana na kadhia hiyo mwishoni mwa wiki alipotembelea masijala ya ardhi katika halmashauri hiyo akiwa katika mfululizo wa ziara zake kutembelea halmashauri mbalimbali nchini kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.

Dkt Mabula alisema, utunzaji wa majalada ya ardhi katika halmashauri ya Chamwino hauzingatii taratibu za kutunza majalada jambo linaloweza kutoa nafasi kwa baadhi ya nyaraka kupotea na wakati mwingine watumishi wasiokuwa waaminifu kuyahujumu

Wakati wa ukaguzi wa majalada ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino Dkt Mabula alibaini majalada mengi yakiwa hayana maelekezo kutoka kwa afisa mmoja kwenda kwa mwingine jambo linaloonesha kuwa utendaji kazi katika sekta hiyo hauna maelekezo yoyote.

‘’mawasiliano ya ofisi lazima yaonekane kutoka kwa ofisa mmoja kwenda kwa mwingine na hapa kuna index namba lakini haitumiki na huwezi kujua aliyepokea nyaraka kwa mara ya kwanza nani hapo lazima migogoro isiishe.’’ Alisema Mabuila.

Dkt Mabula alisema, utunzaji majalada ya ardhi usiozingatia taratibu kwa kiasi kikubwa ndiyo chanzo cha migogoro mingi ya ardhi katika maeneo mbalimbali kwa kuwa ni rahisi kucheza na majalada kwa nia ya kufanya udanganyifu.

Naibu waziri wa Ardhi alitoa maagizo kwa Mkuu wa Idara ya Ardhi Christopher Sanga na Afisa Ardhi Mteule wa halmashauri hiyo ambaye anahudumu pia wilaya ya Kongwa Letare Shoo kuhakikisha upungufu uliopo katika majalada ya ardhi yanarekebishwa kabla mwezi machi mwaka huu na ukifika muda huo atarajea kuona kama maagizo yake yametekelezwa.

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameagiza kufikia machi mwaka huu 2019 viwanja vyote vya halmashauri ya Chamwino viwe vimepimwa na kupatiwa hati na Mkurugenzi wake ahakikishe halmashauri inalipa kodi ya pango la ardhi kwa viwanja inavyomiliki.

Pia ameitaka halmashauri ya Chamwino kuhakikisha wadaiwa wote wa kodi ya pango la ardhi wanapelekewa ilani za madai na watakaoshindwa kutii wafikishwe kwenye mabaraza ya ardhi na kusisitiza kuwa suala hilo halitakiwi kufanywa kisiasa ili kuja na matokeo chanya.

Katika hatua nyingine Dkt Mabula aliitaka idara ya ardhi katika halmashauri wilaya ya Chamwino kuhakikisha hakuna mmiliki wa kiwanja anayejenga katika halmashauri hiyo bila kuwa na kibali cha ujenzi ili kuepuka ujenzi holela.

Naibu Waziri Mabula alisema anataka halmashauri ya Chamwino kuwa na mji uliopangika na mfano kwa halmashauri nyingine na kusisitiza anachotaka ni wengine kujifunza kwenye halmashauri hiyo hasa ikizingatiwa Ikulu iko Chamwino.

Katika kutekeleza hilo amewataka watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri hiyo kuwa na maadili katika kazi zao ili kuepuka utoaji kiwanja kimoja kwa zaidi ya mtu mmoja jambo linalotokea kwa baadhi ya halmashauri na kuleta migogoro.
 Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akiangalia moja ya majalada ya ardhi aliyokagua katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma wakati wa uhamasishaji ulipaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi, kushoto kwa waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Vumilia Nyamuga na kulia ni Afisa Ardhi Mteule Letare Shoo.
 Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma (hawapo pichani) Mwishoni mwa wiki wakati akihamasisha ulipaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
 Watumishi wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma wakimsikiliza Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula mwishoni mwa wiki wakati akihamasisha ulipaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi.
 Mkuu wa wilaya ya Chamwinop mkoa wa Dodoma Vumilia Nyamuga akizungumza wakati Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula alipofanya ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi katika wilaya hiyo mwishoni mwa wiki.
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akioneshwa sehemu ndani ya jengo jipya la halmashauri ya wilaya ya Chamwino na Mkuu wa Idara ya ardhi Christopher Sanga alipowasili kukagua ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi, wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Vumilia Nyamuga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad