HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 22, 2019

SIMANJIRO YAPITISHA MPANGO WA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 35.4

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, limepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya sh35.4 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Yefred Myenzi akisoma rasimu ya mpango huo wa bajeti alisema umezingatia vipaumbele sita. 

Myenzi alitaja vipaumbele hivyo kuwa ni sekta ya elimu, afya, maji, utawala bora, maendeleo ya jamii, kilimo, mifugo na uvuvi. Alisema katika rasimu hiyo ya bajeti, sh17.5 bilioni ni mishahara, sh827.4 ni ruzuku ya uendeshaji ofisi, sh16 bilioni ni miradi ya maendeleo na mapato ya ndani sh1.8 bilioni. 

Alisema kwa vile Simanjiro ni miongoni mwa halmashauri zilizo kwenye mazingira magumu, wamewasilisha maombi maalum kwenye vipaumbele ambavyo havikutengewa fedha. Alisema kupitia maombi hayo wanatarajia kukamilisha madarasa 42 ya shule za msingi, madarasa 77 ya sekondari na nyumba 74 za walimu na watumishi wa elimu. 

Alisema wanatarajia kukamilisha zahanati sita na vituo vya afya viwili na kujenga vituo tisa vya afya na zahanati nne kwenye maeneo ya Msitu wa Tembo, Emboreet na Moipo. "Pia tunatarajia kukamilisha jengo jipya la makao makuu ya wilaya, umaliziaji wa miradi ya maji vijijini na nyumba mbili za watumishi wa afya," alisema Myenzi. 

Diwani wa kata ya Endiamtu, Philemon Oyogo alisema wamepitisha bajeti hiyo ila serikali kuu inapaswa kufikisha fedha kwani kwenye bajeti ya mwaka jana hawakuwaletea fedha zote. Diwani wa kata ya Naberera, Haiyo Yamati alipongeza bajeti hiyo ila alitarajia sekta ya mifugo kutengewa fedha nyingi zaidi. Diwani wa kata ya Mirerani, Thomas Yohana alisema shule mpya ya sekondari Songambele itanufaika kupitia bajeti hiyo. Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2018/2019 halmashauri hiyo ilipitisha bajeti ya sh22.6 bilioni. 
 Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wakipitia rasimu ya mpango wa bajeti ya shilingi bilioni 35.4 kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020. 
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Yefred Myenzi akisoma rasimu ya mpango wa bajeti ya shilingi bilioni 35.4 kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wakifuatilia kikao cha Baraza la Madiwani lililopitisha bajeti ya shilingi bilioni 35.4 kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.  

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad