HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 16 January 2019

RC TABORA AIAGIZA KAMPUNI YA L AND T KUREKEBISHA KASORO UJENZI WA TANKI LA MAJI LA KIJIJI CHA IBELAMILUNDI

Na Tiganya Vincent, Tabora
SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imemwagiza Makandarasi wa L and T kufanyia marekebisho ya kasoro na udhaifu uliojitokeza katika utekelezaji wa ujenzi wa tenki la maji la ujazo lita milioni moja uliokuwa ukijengwa katika Kijiji cha Ibelamilundi wilayani Uyui baada ya Kamati iliyoundwa kubaini baadhi ya mapungufu kwenye maendeleo ya mradi huo.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ametoa maagizo hayo hiyo jana baada ya kupokea taarifa ya Kamati aliyokuwa ameiunda kuchunguza ubora wa kazi katika ujenzi wa hilo kubaini uwepo wa kasoro katika usukaji wa nondo na Mkandarasi kutumia michoro ambayo hajaidhinishwa na Mshauri wa Mkandarasi.

Alisema pia Kamati imebaini udhaifu katika usimamizi wa Mhandisi Mshauri(Consultant ) mradi huo ikiwemo na ule upande wa Serikali kutotembelea mradi na kutoa ushauri wa kuboresha kasoro na kutokuwa na mawasiliano ya karibu wakati wa ujenzi wa mradi huo.

Mwanri alisema baada ya kupokea taarifa ya Kamati amemtaka Mkandarasi kuendelea na shughuli wakati akiendelea kurekebisha mapungufu yote yaliyojitokeza na kuwataka wasimamizi kwa upande wa Serikali kutembelea mara kwa mara maeneo ya mradi ili kuhakikisha unakuwa na ubora kulinga na mkataba wa ujenzi wake.

Alisema lengo ni kupata mradi ambayo utadumu kwa muda mrefu badala ya kujengwa kisha inaharibika katika kipindi kifupi. Aidha Mkuu huyo wa Mkoa aliitaka Kamati hiyo kufanya ukaguzi wa miradi yote ya ujenzi wa bomba la maji hilo ili kuona kama kweli Mkandarasi anazingatia michoro iliyopo kwenye mkataba.

Naye Mwenyekiti wa Kamati maalumu  iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Injinia Damian Ndabalinze alisema kuwa Kamati ilibaini mapungufu kadhaa ikiwemo matumizi ya micho ya ramani ambayo hakuidhinishwa na Mhandisi Mshauri na kuwepo na udhaifu katika usimamizi katika mradi huo.

Alisema Kamati inashauri kuwepo na usimamizi wa karibu na mawasiliano ya maandishi yawe yanafanyika kuonyesha kama kwenye pande zinahusika zimekutana kwa kuandika katika kitabu maalumu(log book). Kwa upande wa Meneja Mradi kutoka Kampuni ya Mhandishi Mshauri ya Wapcos LT Bw. Manohar Mattendda alisema atahikisha anamsimamia vema Mkandarasi ili kuhakikisha anfanyia kazi mapendekezo ya Kamati na kuweza kuwepo na ubora kwa kazi iliyokusudiwa na inakamilika kwa wakati.

Naye Meneja wa Kampuni inayotekeleza ujenzi mradi huo ya L and T Giresh Krishnamoorthy aliahidi kufanyia marekebisho kasoro na mapungufu yaliyojitokeza ili aweze kutekeleza kazi nzuri kulingana mkataba alioingia na Serikali ya Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa  Mamlaka ya Maji Safi katika Manispaa ya Tabora(TUWASA) Mkama Bwire alisema watajitahidi kushirikiana na pande ili kuhakikisha wanaboresha mapungufu yaliyojitokeza.
 Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya kuchunguza ubora wa tenki katika Kijiji cha Ibelamilundi Injinia Damiani Ndabalinze akitoa ripoti ya uchunguzi wa ubora walioifanya hivi karibuni. 
 Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya kuchunguza ubora wa tenki katika Kijiji cha Ibelamilundi Injinia Damiani Ndabalinze (kulia) akikabidhi  ripoti ya uchunguzi wa ubora walioifanya hivi karibuni kwa Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu (katikati) ili naye akabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri(kushoto).
 Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu akitoa maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora ili apokee ripoti ya uchunguzi wa ubora wa tenki lililokuwa likijengwa katika Kijiji cha Ibelamilundi wilayani Uyui.
 Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu(kulia) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri(kushoto) ripoti ya uchunguzi wa ubora wa tenki lililokuwa likijengwa katika Kijiji cha Ibelamilundi wilayani Uyui.
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri(kushoto) akitoa ufafanunuzi jana mara baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi wa ubora wa tenki lililokuwa likijengwa katika Kijiji cha Ibelamilundi wilayani Uyui. Picha na Tiganya Vincent

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad