HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, January 20, 2019

MKUTA YAWAPATIA WACHIMBAJI ELIMU YA KIFUA KIKUU NA UKIMWI

ILI kutokomeza maambukizi ya kifua kikuu, HIV na Silikosis, kwenye migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wachimbaji 13,328 wamepatiwa elimu ya kujikinga kupitia shirika la mapambano ya kifua kikuu na ukimwi (Mkuta). Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Mapambano ya kifua kikuu na ukimwi Tanzania (Mkuta) Thobias Magati aliyasema hayo wakati akizungumzia kazi za huduma ya jamii kwa mwaka jana. 

Magati alisema katika watu hao 13,328 waliofikiwa, wanaume walikuwa 11,307 wanawake 1,804 na watoto ni 217 na wagonjwa waliogundulika ni 123. Alisema uwezeshaji ni mdogo kwao kwani hawana wafadhili ila mwaka jana waliwezeshwa na Kibong'oto OHSC kufikia wagonjwa wengi. "Uwezeshaji ndiyo mdogo ila wameweza kufungua matawi ya Mkuta kwenye maeneo ya kitalu B (Opec) na kitalu D ambayo yapo kwenye migodi inayowazunguka ili kusaidia shughuli za uibuaji," alisema Magati. 

Alisema wanafanya hayo ili kufikia malengo ya tamko la kisiasa la umoja wa mataifa la kutokomeza kifua kikuu ifikapo mwaka 2022. Alisema endapo kuna asasi au taasisi yeyote itakayokuwa inataka kuonana nao wawasiliane nao kupitia namba za simu 0789564832 au barua pepe ya mkutaclubmirerani@gmail.com watawapata. Katibu wa Mkuta, Benjamin Kaba alisema wanakabiliwa na changamoto ya wagonjwa wengi wa kifua kikuu, gharama ya ufuatiliaji na kutopata vipimo kwa wakati. 

Kaba alisema changamoto nyingine ni wachimbaji wengi wanaugua ugonjwa wa Silikosis na Pneumonia ambayo yanahitaji kufanyiwa utafiti wa kina zaidi na mabadiliko ya ukuta yamesababisha wagonjwa kushindwa kutoka kwenda kupata huduma.  Alisema changamoto nyingine ni kuhamahama kwa wagonjwa kwenda migodi mingine ya Kitwai, Lemshuku, Mwajanga, Landanai na Kimwengani. 

Alisema wana mikakati mingi yakufanikisha mipango yao ila wanakwamishwa kutokana na ukata unaowakabili kwani hawana mfadhili wa kukisaidia kikundi hicho chenye wanachama 58. Mjumbe wa Mkuta, Mwasiti Ntandu alitoa wito kwa serikali kuiangalia Mirerani kwa jicho la pekee kwani magonjwa ya kifua kikuu na Silikosis inayosababishwa na ulanga imewaathiri watu wengi. Ntandu alisema baadhi ya wachimbaji wamewaacha wajane na yatima kutokana na kuugua maradhi hayo ambayo yanaweza kutibika. 
 Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Mkuta la Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Thobias Chacha Magati akielezea mikakati ya asasi yao. 
Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la Mkuta la Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Thobias Chacha Magatiakisoma kanuni na sheria za Mkuta. 
Wanachama wa shirika lisilo la kiserikali la Mkuta wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakifurahia pamoja baada ya taarifa ya utekelezaji wa huduma kwa jamii ya mwaka jana. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad