HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 14 January 2019

MABORESHO YA SERA YA MAENDELEO YA JINSIA KUKAMILIKA JUNI 2019

Maboresho ya Sera ya Maendeleo ya  Jinsia ya mwaka 2000 yanategemewa kukamilika ifikapo mwezi Juni mwaka 2019 ili kuwezesha hatua nyingine za ukamilishaji wa Sera hiyo na kuanza kutumika rasmi.

Hayo yamebainikia leo jijini Dodoma katika kikao kilichokutanisha wadau wa masuala ya jinsia kikosi kazi cha wadau wanaoshughulikia masuala  ya jinsia katika Wizara, Taasisi za Serikali na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini.

Akifungua kikao hicho Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto (Idara Kuu Maendeleo ya Jamii)  Bw. Patrick Golwike amesema kikao kazi hicho ni muhimu kwa kupeana mrejesho wa masuala mbalimbali yahusuyo jinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Ameongeza kuwa wadau wa nafasi ya muhimu na wajibu wa kutetea masuala ya kijinsia kwa kuunganisha nguvu kwa pamoja na Serikali na wananchi na kuwa suala  la usawa wa kijinsia  na uwezeshaji wanawake linawezekana endapo kutakuwepo na ushiriki wa pande zote husika.

Akielezea suala la marekebisho ya Sera ya Maendeleo ya Jinsia ya mwaka 200 Kaimu Katibu Mkuu huyo amesema kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kufanikisha marekebisho hayo ili kuendana na mabadiliko katika jamii ambapo masuala mbalimbali yahusuyo jinsia yamekuwa yakijitokeza ikiwemo uwepo wa  kipaumbele kwa mahitaji ya wanawake katika mapambanao dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Bw. Julius Mbilinyi ameeleza kuwa Mchakato wa maboresho ya Sera ya Maendeleo ya Jinsia upo katika hatua ya mwisho ya kupata ushauri wa wadau ili kuanza kuipitia Sera hiyo na kuifanyia marekebisho kwa kushirikisha wadau wa masuala  ya jinsia.

Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia katika Jeshi la Mgereza Kamishna wa Magereza Tusekile Mwaisabila amesema Jeshi hilo linaendeleza jitihada za kuleta usawa wa kijinsia na imetekeleza maagizo ya kuanzishwa kwa Dawati la Jinsia ndani ya Jeshi hilo.

Ameongeza kuwa uazishwaji wa Dawati la Jinsia ndani ya Jeshi la Magereza unalenga kusaidia jeshi kuweka Mipango ya usawa wa jinsia, kupokea, kusikiliza, kufuatilia na kutoa uamuzi, ushauri, na mapendekezo kuhusu migogoro, malalamiko ya masuala ya kijinsia na changamoto zake.

Kamishna Tusekile amesisitiza kuwa Dawati la Jinsia katika Jeshi hilo linasimamia masuala yote ya kijinsia kwa kutoa elimu na ushauri kuhusu masuala hayo kwa wadau wa ndani na nje ya Jeshi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto (Idara Kuu Maendeleo ya Jamii)  Bw.  Atupele Mwambene akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto amesema kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2018 jumla  ya Kamati za ulinzi kwa wanawake na watoto  3,605 zilianzishwa katika ngazi ya mikoa, wilaya, mitaa na vijijini na mpaka sasa jumla ya Kamati 10,988 zimeanzishwa nchi nzima.

Ameongeza kuwa Idadi ya Kamati zinazotakiwa kuanzishwa ni 21,500 na mpaka sasa ni asilimia 51 tu ya Kamati hizo ndio zimaenzishawa na kusema kuwa kuna changamoto kubwa katika uanzishwaji wa Kamati hizo katika ngazi ya Vijiji na Mitaa.

Bw. Mwambene amesema kuwa ili kuondoakana na changamaoto hizo Serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuwezesha uanzishwaji wa Kamati hizo hasa katika ngazi za Vijiji na Mitaa na mpaka sasa mikoa yote imeanzisha Kamati katika ngazi hiyo.
 Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu Maendeleo ya Jamii)  Bw. Patrick Golwike akifungua kikao cha wadau wa masuala  ya kijinsia kilichofanyika jijini Dodoma kulia ni Mwakilishi wa Shirika la UN Women Bi Hoda Addou na kushoto ni Mkurugenzi wa  Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Bw. Julius Mbilinyi.
 Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Julius Mbilinyi (kushoto) akielezea juhudi za Wizara katika masuala ya jinsia na uwezeshaji wanawake wakati wa kikao kilichokutanisha wadau wa masuala ya kijinsia jijini Dodoma kulia ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu Maendeleo ya Jamii)  Bw. Patrick Golwike.
 Mwakilishi wa Shirika la UN Women Bi. Hoda Addou(kulia) akifafanua masuala  mbalimbali yanayofanywa na Shirika hilo kuhusu usawa wa kijinsia wakati wa Kikao kilichowakutanisha wadau wa masuala ya jinsia jijini Dodoma kushoto  ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu Maendeleo ya Jamii)  Bw. Patrick Golwike.
 Mkuu wa Dawati la Jinsia Jeshi la Magereza Kamishna wa Magereza Tusekile Mwaisabila (katikati) alielezea namna Dawati hilo linavyowasaidia wafungwa wanawake, familia za watumishi wa magereza na jamii iliyokaribu na magereza wakati wa Kikao kilichowakutanisha wadau wa masuala ya jinsia jijini Dodoma.
Baadhi ya wadau wa masuala ya jinsia wakifuatilia mijadala na maoni yaliyokuwa yakitolewa na wajumbe katika kikao kilichowakutanisha wadau hao jijini Dodoma kujadili masuala mbalimbali ya kijinsia na uwezeshaji wanawake. Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad