HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, 27 January 2019

KUWAHUDUMIA WAKIMBIZI NI JUKUMU LA WATU WOTE SIO NCHI MOJA

Kuwahudumia Wakimbizi ni jukumu la Wote sio la Nchi moja
Kazi ya kuwahudumia wakimbizi ni Ubinadamu na ni jukumu la kimataifa na ni kitu cha kushangaza kuona nchi zilizoendelea zinaziachia nchi masikini kubeba mzigo wa kugharamia wakimbizi.

Kauli hiyo ilitolewa na Rais Mstaafu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Baraza la Wakimbizi Duniani (World Refugees Council-WRC), Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa kuwasilisha ripoti ya Baraza hilo kwenye Umoja wa Mataifa New York, Marekani tarehe 24 Januari 2019.

Rais Mstaafu alitanabainisha kwamba Baraza lao lilipokea msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kukataa mpango wa kukopa Benki ya Dunia ili kuwahudumia wakimbizi wakati yenyewe inadaiwa mikopo ya kimaendeleo iliyonayo. Serikali inaamini kazi ya kuhudumia wakimbizi ni ya kibinadamu kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa badala ya kuibebesha nchi moja mzigo wa madeni.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa tatizo la wakimbizi limekuwa kubwa sana duniani wakati huu kuliko wakati wowote ule tangu vita vya Pili vya Dunia. Mathalan, kuna idadi ya watu milioni 68.5 waliopoteza makwao (Internally displaced persons) mwaka 2017 na kati yao, milioni tatu wamepoteza makwao kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa na uchafuzi wa mazingira. 

Ripoti inaeleza kuwa, kumekuwa na ongezeko kubwa la wakimbizi na wanaopoteza makwao kusini mwa jangwa la Sahara ambao walifikia milioni 18.4 mwaka 2017 ukilinganisha na idadi ya milioni 14.1 mwaka 2015. Ripoti inabainisha kuwa ongezeko hilo limetokana na sababu mbalimbali zikwemo upvotevu wa amani katika nchi zao.

Ripoti inazidi kubainisha kuwa asilimia 30 ya watu wote duniani mwaka 2017 walikuwa wakimbizi na waliopoteza makwao ukilinganisha na asilimia 23 ya mwaka 2015. Kati ya idadi hiyo, wanaotoka Afrika, asilimia 79% wanatoka katika nchi za Somalia, Nigeria, Sudan kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Ripoti imeeleza nchi zinazopokea wakimbizi wengi kuwa ni pamoja na Uganda, wakimbizi milioni moja na laki nne; Ethiopia, laki Tisa; Tanzania laki tatu na ishirini na Sita elfu; na Rwanda elfu 84. Baadhi ya nchi zimechukua wakimbizi hao ikiwemo Marekani, Canada, Australia na Finland ingawa idadi yao ni ndogo mno. 

Katika ripoti hiyo, baraza limetoa mependekezo mbalimbali ya kukabiliana na tatizo la wakimbizi duniani. Mapendekezo makubwa ni pamoja na kudhibiti nchi ambazo zinachochea au kuanzisha migogoro kwa kuweka mfumo thabiti wa kimataifa, kuongeza usuluhishi wa migogoro, kutowanyanyapaa wakimbizi kwa kujenga ukuta na kusaidia juhudi za kutafuta amani katika maeneo yenye migogoro. 

Baraza la Wakimbizi duniani ni chombo kilichoundwa na wataalamu mbalimbali wakiwemo wanasiasa, watafiti na watunga sera kwa lengo la kufanya utafiti wa kina utakaosaidia kubuni njia na mbinu za kitaalamu na za ubunifu zitakazosaidia kukabiliana na kumaliza kabisa tatizo la wakimbizi duniani. 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma 
27 Januari 2019 
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Wakimbizi Duniani (World Refugees Council, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete (mstari wa mbele wa kwanza kushoto) akiwa na viongozi mbalimbali jijini New York baada ya Baraza hilo kuwasilisha ripoti kwenye Umoja wa Mataifa ya namna ya kukabiliana na tatizo la wakimbizi duniani. Picha inaonesha kitabu cha ripoti iliyowasilishwa. 
Mheshimiwa Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Balozi Modest J. Mero (kushoto) na viongozi wengine wa Baraza la Wakimbizi Duniani. 

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad