HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 21, 2019

KAMATI YA BUNGE YAISHAURI SERIKALI KUWEKA MKAZO KATIKA KAMPENI YA UPANDAJI MITI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira imeishauri Serikali kuona namna bora ya kuendeleza kampeni ya upandaji miti kwa mafanikio zaidi katika ngazi zote. Ushauri huo umetolewa katika kikao  baina ya Kamati hiyo na watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais wakati wa kuwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi hiyo kwa kipindi cha miezi sita yaani (Julai 2018 – Desemba 2018).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Waheshimiwa Wabunge wameishauri Serikali kuhuisha kampeni ya upandaji miti katika Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo Vikuu ili kasi ya upandaji miti iendane na kasi ya ukuaji wake, ikiwa ni pamoja na kutekeleza kwa vitendo mpango wa kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.

“Wekeni utaratibu wa kutoa motisha kwa wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi katika kupanda na kutunza miti” alisisitiza Mhe. Dotto Gimbi Mjumbe wa Kamati hiyo. Akitoa ufafanuzi mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima amesema katika kipindi cha miezi sita, Ofisi ya Makamu wa Rais imepata mafanikio mengi ikiwa ni pamoja na kutimiza malengo waliojiwekea na kuahidi kuendelea kuzipatia ufafanuzi changamoto nyingine zilizoibuliwa na wajumbe wa Kamati likiwemo suala la utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabia nchi kwa upande wa pili wa Muungano.

Vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge vinaendelea katika kumbi za Bunge Jijini Dodoma na siku ya kesho Kamati hii itapokea taarifa ya Usimamizi na Matumizi salama ya Bioteknolojia ya Kisasa na Maandalizi ya Mpango wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwa Wachimbaji wadogo wa dhahabu chini ya Mkataba wa Minamata.
 Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima aliesimama akitoa ufafanuzi wa hoja kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira mara baada ya Kamati kupokea taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kipindi cha Julai – Desemba, 2018.

Mwenyekiti wa Bodi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Prof. Esnati Osinde Chaggu akijitambulisha kwa mara ya kwanza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira. Prof. Chaggu ameteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Joseph Magufuli. Kulia ni Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Kanali Mstaafu Masoud Khamis.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad