HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 29, 2019

CHUO CHA BANDARI KUDAHILI WANAFUNZI KIDIJITALI

Chuo cha Bandari kitaanza kudahili wanafunzi wapya kupitia mfumo wake mpya wa kidijitali ujulikanao kama Student’s Information Management System (SIMS). Mfumo huo wa kidijitali uliozinduliwa jana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac Kamwelwe utawezesha chuo hicho kuwadahili wanafunzi kidijitali.

Mbali na hayo, mfumo huo ambao ulibuniwa na kutengenezwa na wafanyakazi wa TPA kitengo cha TEHAMA, pia utatumika kukokotoa matokeo ya mitihani na kuanda taarifa ya mwisho wa mwaka wa mafunzo yaani ‘final year transcript’. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tovuti ya mfumo huo mpya, Waziri Kamwelwe alisema uwepo wa mfumo huo utasaidia kudhibiti udanganyifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu.

Mhandisi Kamwelwe ameongeza kwamba awali wakati udahili ulipokuwa ukifanywa kwa kujaza fomu kwa mkono ‘manual’, kulikuwa na tatizo la uchakachuaji wa vyeti na upotevu wa pesa.  “Wakati wa application manual (kujisajili kupitia mikono) kuna fomu za maombi zilikuwa zinapotea na kulikuwa na upotevu wa pesa pamoja na tatizo la kuchapisha vyeti feki na baadhi ya wanafunzi kutohudhuria mafunzo ipasavyo,” amesema.

Mhandisi ameongeza kwamba kipindi hicho kuna baadhi ya wanafunzi waliishia kusajiliwa tu na baada ya miaka miwili unamkuta mtaani na cheti lakini kwa uwepo wa mfumo, hayo mambo hakuna tena. Kwa upande wake Mkuu wa Bodi ya Magavana ya Chuo hicho, Mhandisi Deusdedit Kakoko alimshukuru Waziri kwa kutenga muda na kuja kuwazindulia tovuti hiyo ambayo ni muhimu mno kwa chuo hicho. 

Mhandisi Kakoko ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa TPA amesema kwamba waziri ana mambo mengi lakini kutokana na umuhimu wa jambo hilo, ameamua kuja kuzindua mfumo huo ambao ni muhimu kwa wanafunzi na chuo kwa ujumla. “Uwepo wa mfumo huu, utarahisisha utendaji kazi wetu kama chuo na kudhibiti wale wote waliokuwa wakitumia mianya ya kutokuwepo kwa mifumo hiyo, kufanya udanganyifu,” amesema.

Akizungumzia faida za mfumo huo, mmoja wa wafanyakazi wa TPA ambaye ameshiriki kubuni mfumo huo, Rainer Mwashu alisema utarahisisha zoezi la udahili wanafunzi na kupata taarifa zao kwa urahisi wakati wowote zikihitajika. “Kupitia mfumo huu, mwanafunzi ataweza kujisajili kwa ajili ya mwaka wa masomo popote pale alipo…amesema na kuongeza kwamba,…kwasasa taarifa zote za wanafunzi wa chuo hiki zitapatikana kidijitali kupitia mfumo huu.” Mbali ya hayo, pia mfumo huo utatumika kuzalisha taarifa ya mwisho ya matokeo ‘final year transcript’, na utawezesha kuoana kwa mifumo ya ndani na nje ya taasisi kama vile NACTE, NECTA na GePG.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac Kamwelwe akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa tovuti hiyo. Wengine picha ni Mkuu wa Chuo kushoto, Dkt. Joseph Kakeneno, pembeni ya Waziri ni Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya Chuo Cha Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko na Mjumbe wa bodi hiyo, Dkt. Eliamini Kasembe.

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaac Kamwelwe katikati mara baada ya kukata riboti kuashiria uzinduzi wa tovuti hiyo. Wengine pichani ni Mkuu wa Chuo cha Bandari, Dkt. Joseph Kakeneno, kushoto, Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya Chuo Cha Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko, wa pili kulia na Mjumbe wa bodi hiyo, Dkt. Eliamini Kasembe 
  

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad