HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, December 4, 2018

Wekezeni kwenye afya kwa kujiunga na NHIF- Waziri Ummy

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bwana Bernard Konga katika mkutano wa hadhara Halmashauri ya Wilaya ya Nanyamba Mkoani Mtwara wakati wa uhamasishaji wa wananchi kujiunga na NHIF, kupitia Mpango wa Ushirika Afya.

Na Grace Michael

Wananchi Mkoani Mtwara wametakiwa kufanya uwekezaji kwenye afya zao kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote. Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizungumza na wananchi katika Halmashauri ya Mji wa Nanyamba mkoani Mtwara.

Amesema kuwa ili kila mwananchi aweze kuwa na uhakika wa kufanya shughuli zingine za maendeleo na uwekezaji mwingine lazima awe na uhakika na afya yake kwa kuwa na uhakika wa kupata matibabu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akikagua Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara. 

“Nawaomba sana wananchi wa Mtwara wekezeni kwenye eneo la afya zenu na uwekezaji mzuri ni kuwa na Bima ya Afya kupitia NHIF ili iwawezeshe kupata huduma zote za matibabu kwa ngazi mbalimbali za vituo vya kutolea huduma kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Hospitali ya Taifa,” alisema Mhe. Ummy.

Alisema kuwa Serikali imeweka utaratibu mzuri wenye gharama nafuu wa kupata huduma za matibabu kupitia NHIF, utaratibu ambao unamtaka mwananchi kujiunga kabla ya kuugua ili aweze kunufaika na huduma za matibabu wakati wowote anapopatwa na maradhi.

“Wengi wetu hapa mmeuza mazao yenu na mnalipwa fedha nyingi, kati ya fedha mnazopata hakikisheni mnatenga shilingi 76,800 tu kwa ajili ya kukata kadi ya bima ya afya ambayo itakusaidia kupata huduma mahali popote ndani ya nchi kwenye zaidi ya vituo 7000 vilivyosajiliwa na NHIF,” alisema Mhe. Ummy wakati akizungumza na wananchi wa Nanyamba Mkoani Mtwara.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akimhamasisha mmoja wa akina mama kumwandikisha mtoto wake na mpango wa Toto Afya Kadi ili awe na uhakika wa kupata matibabu. 

Aliwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma za matibabu katika hospitali zote nchini kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imeongeza kwa kiasi kikubwa bajeti ya afya hususan bajeti ya dawa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bwana Bernard Konga alisema kuwa, Mfuko umejipanga kuhakikisha unawafikia wananchi wote katika maeneo yao na kuwasajili ili waweze kuwa kwenye utaratibu rahisi wa kupata huduma za matibabu.

“Tumeweka mazingira rahisi ya upatikanaji wa huduma za matibabu, tunao wigo mpana wa vituo vya kutoa huduma kwa wanachama wetu hivyo tumejipanga kuwafikia katika maeneo yenu ili tuwasajili na muanze kunufaika na huduma zetu ambazo unaweza ukazipata wakati wowote hata ambao hauna fedha,” alisema Bw. Konga.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akiendelea na uhamasishaji wa wananchi. 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Bw. Evod Mmanda aliupongeza Mfuko kwa kuanzisha mpango wa Ushirika Afya ambao unawawezesha wakulima kunufaika na huduma za matibabu kwa gharama nafuu.

Mheshimiwa Waziri Ummy yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya siku tatu, ambapo mbali na kutembelea vituo vya kutolewa huduma atazungumza na wananchi na kuwahamasisha kujiunga na Bima ya Afya ili kila mwananchi awe na uhakika wa kupata matibabu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akiwaeleza wananchi umuhimu wa kujiunga na NHIF.
Viongozi wa Vyama vya Ushirika katika Halmashauri ya Nanyamba wakimsikiliza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu juu ya kujiunga na NHIF, kupitia Mpango wa Ushirika Afya.
Ufafanuzi wa masuala ya namna ya kujiunga na huduma za NHIF ukiendelea.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga wakijibu maswali ya wananchi juu ya huduma za NHIF.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad