HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 17 December 2018

TAMASHA LA MAPINDUZI FESTIVAL LAZINDULIWA

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
MABINGWA wa burudani ya muziki wa kizazi kipya visiwani Zanzibar jana wameonyesha uwezo wao katika kuiwakilisha vyema sanaa ya muziki nchini. Wasanii hao wamezitumia vyema sauti, kumiliki jukwaa pamoja na kucheza na hisia kali za mashabiki waliobobea katika uwanja wa burudani ambapo yote hayo yalionekana kwa kila msanii aliyepanda kuimba katika Tamasha hilo la 'Safari ya muziki miaka 55 Mapinduzi' .

Akizindua Tamasha hilo Naibu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Zanzibar  Bimkubwa Sukwa katika Uwanja wa Mpendae Shule ya Sekondari  Wilaya ya Mjini , aliitaka jamii kuunga mkono juhudi za wasanii wa kizazi kipya waliojitolea kwenda kwa wananchi kujitangaza na kuonyesha vipaji vyao.

Alisema umefika muda mwafaka wa Serikali na wadau mbali mbali wa maendeleo ndani na nje ya Zanzibar  kuwa mstari wa mbele kusaidia juhudi za wasanii kwani sanaa ya muziki ni sehemu pana ya vijana wengi kujiajiri wenyewe. Katika maelezo yake Naibu Mstahiki Meya, alieleza kuwa tamasha limebeba tunu ya nchi ambayo ni Mapinduzi ya miaka 55 jambo ambalo wasanii hao wameonyesha uzalendo wa kweli wa kuenzi falsafa ya Mapinduzi.

 Akizungumza Rais wa Chama Cha Wasanii wa muziki wa Kizazi kipya Mohamed Abdallah "Laki wa Promise'  ameiomba jamii kujenga utamaduni wa kuthamini sanaa ya muziki wa kizazi kipya visiwani zanzibar ili wasanii  wafanye vizuri zaidi ndani na nje ya  Visiwa vya Zanzibar. Rais huyo alisema Wasanii Zanzibar wanashindwa kufanya vizuri katika muziki hususani ndani ya Zanzibar  kutokana na jamii ya Zanzibar kutojali kazi za wasanii hali inayosababisha changamoto ya kushuka kwa kiwango cha muziki nchini.

Wakizungumza kwa wakati tofauti baadhi ya mashabiki wa muziki wa burudani katika tamasha hilo, wamekiri kuwa Zanzibar ina wasanii wengi wenye vipaji na tamasha hilo likiendelea kila mwaka litakuwa ni sehemu ya kuibua vipaji hivyo. Tamasha hilo lilipambwa na michezo mbali mbali ikiwemo mchezo wa nage,keramu pamoja na mpira wa miguu ambapo washindi wote katika michezo hiyo wamepewa zawadi mbali mbali ikiwe mshindi wa mpira wa miguu timu ya Mpendae 3-0 dhidi ya timu ya wananii na kupewa zawadi ya mbuzi.

Wasanii mbali mbali waliokuwepo katika tamasha hilo ni pamoja na Rico Single, Juma Town, Sultan King na waliopanda jukwaani kwa ajili ya kuimba ni pamoja na Shaby Six, Ismail na wengine wengi walitoa burudani katika tamasha hilo.
 NAIBU Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mjini Bimkubwa Sukwa akikagua Timu ya Wasanii wa Muziki wa Kizazi kipya waliocheza na Timu ya Mpendae ikiwa ni sehemu ya wasanii kuwa karibu na jamii.

 Wasanii mbali mbali wa muziki wa kizazi kipya wakionyesha uwezo wao wa kuteka jukwaa huko katika Tamasha la Safari ya Muziki Mapinduzi Festival lililozinduliwa jana katika Jimbo la Mpendae Wilaya ya Mjini Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad