HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, December 13, 2018

Prof. Ndalichako aahidi kushughulikia uchakavu wa miundombinu ya vyuo vya VETA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameahidi kushughulikia changamoto ya uchakavu wa miundombinu katika vyuo vya ufundi stadi vinavyomilikiwa na VETA ili kuwezesha utoaji wa mafunzo bora sambamba na mabadiliko mbalimbali ya teknolojia viwandani na kukidhi viwango vya mahitaji ya waajiri.

Prof.  Ndalichako alitoa ahadi hiyo kufuatia ombi la Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pancras Bujulu wakati akitoa maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha kutoa hotuba kwenye sherehe za mahafali ya 33 ya Chuo cha VETA Moshi yaliyofanyika chuoni hapo Jumatano, 12 Desemba 2018.

Katika maelezo yake, Dkt. Bujulu alisema kuwa baadhi ya vyuo vya VETA ni vikongwe mno na miundombinu yake imechakaa sana, hivyo ukarabati wake kwa kutumia fedha ambazo VETA imekuwa ikipatiwa na serikali umekuwa ni mgumu. Alisema pamoja na uchakavu wa miunndombinu kwa ujumla vifaa na mashine zinazotumika kwenye karakana kwa ajili ya kufundishia pia zimechakaa na zingine  zimepitwa na wakati kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia hivyo hazifai kutumika kufundishia ili kutoa mafundi wanaokidhi mahitaji ya wakati huu.

“Nikizingatia uzoefu wangu na wewe kuwa una mapenzi sana na miundombinu ya vyuo. Umetengeneza catalogue ya kutengeneza miundombinu ya vyuo vikuu na vyuo vya elimu ya juu. Naomba sasa na hivi vya stadi za kawaida navyo utengeneze catalogue (mchanganuo wa mahitaji) ili uwe unajua chuo chetu cha wapi na wapi na wapi kinahitaji nini na utakuwa unajua wapi unapata hela kidogo unatengeneza,” alisema.

Akijibu ombi hilo, Prof. Ndalichako alisema kuwa alisema kwa kutambua jukumu na shauku ya kutaka taasisi zilizo chini yake zinakwenda vizuri, alisema kuwa yuko tayari kupokea mchanganuo wa mahitaji ya vyuo vya ufundi stadi nchini ili ayafanyie kazi.

“Mkiniwezesha nikafahamu vizuri mahitaji yenu, na kwa sababu ni kipaumbele cha serikali ya awamu ya Tano, na Mheshimiwa Rais (John Pombe Magufuli) amekuwa akisisitiza hili eneo la mafunzo ya ufundi stadi niweze kuliimarisha vizuri, basi nina kila sababu ya kuhakikisha ninasikiliza ushauri wa wataalam ili tuweze kuhakikisha kuwa tunaimairisha mafunzo ya ufundi stadi kwa kiwango ambacho ndio kinahitajika na wataalam wetu na kinachokubalika na waajiri ambao huwachukua vijana wanapomaliza mafunzo,” alisema.

Alisema kuwa elimu ya ufundi stadi ina umuhimu sana katika kipindi hiki ambacho serikali imeweka mikakati ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi unaoendeshwa, kwani hakuna kiwanda kinachoweza kuendeshwa bila mafundi stadi. 

Wakati huohuo, Prof. Ndalichako ameiagiza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kushirikiana na Idara ya Ufundi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Chemba ya Madini na Nishati (TCME) na wadau wengine kukaa na kuweka utaratibu wa kupanua Mpango wa Mafunzo ya Uanagenzi katika vyuo vingine vya VETA nchini na kushirikisha sekta zingine zaidi ya madini.

Alisema, mfumo wa mafunzo kwa njia ya uanagenzi una manufaa makubwa kwa pande zote, akifafanua kuwa licha ya kusaidia kuongeza udahili, mfumo huu unasaidia vijana kujifunza teknolojia mpya zilizopo viwandani; kusaidia vijana kupata ujuzi na uzoefu halisi unaohitajika mahala pa kazi katika fani husika na makampuni kuwa na uhakika wa nguvukazi yenye umahiri wa kiwango wanachokihitaji.

Mahafali ya 33 ya chuo cha VETA Moshi yalihusisha jumla ya wahitimu 174 wa fani mbalimbali wakiwemo daraja la 2 (yaani level 2) 104, Daraja la 3 (yaani Level 3) 24 na wanagenzi kupitia mradi wa IMTT ni 46.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akitoa hotuba kwenye mahafali ya 33 ya Chuo cha VETA Moshi yaliyofanyika chuoni hapo Jumatano, tarehe 12 Desemba 2018.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pacras Bujulu akitoa Maelezo kuhusu mipango na mikakati ya VETA katika kutoa na kusimamia mafunzo ya ufundi stadi.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akitazama nyaraka za kampuni ya LES Inspection iliyoanzishwa na wahitimu wa VETA ambao wamefuzu na kupata leseni za kutoa ithibati ya kazi za uungaji vyuma kwa kiwango cha kimataifa wakati akitembelea maonesho ya wahitimu kwenye mahafali ya 33 ya Chuo cha VETA Moshi, Jumatano, tarehe 12 Desemba 2018. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu na anayefuatia ni Mwenyekiti wa Chemba ya Madini na Nishati, Balozi Ami Mpumbwe.
  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akisikiliza maelezo kutoka kwa mhitimu wa fani ya Ufundi wa Kaanga Mvuke (Boiler Mechanics) juu ya mfumo wa kaanga mvuke (Boiler) unavyofanya kazi kwenye mahafali ya 33 ya Chuo cha VETA Moshi, Jumatano, tarehe 12 Desemba 2018. Kulia kwa Waziri ni Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad