HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 24 December 2018

Mwakyembe kuona kijiji cha wasanii Mkuranga

WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo,Harrison Mwakyembe amekubali mwaliko wa kutembelea kijiji cha wasanii Mwanzega kujionea maendeleo ya ujenzi wa nyumba za wasanii.

Katibu wa Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) Michael Kagondela akizungumza jana wakati wa hafla ya  kukabidhi nyumba 15 kwa wasanii na wanamichezo alisema katika mazungumzo ya SHIWATA na Waziri Mwakyembe kuomba kijiji chao chenye nyumba za makazi kutambuliwa wizarani yamefanikiwa.

"Nawataarifuni kuwa SHIWATA inafanya kazi zake kwa uwazi na kufuata taratibu za kiserikali, tumemuomba Waziri Mwakyembe atutembelee na yeye amekubali kuja hapa kijijini kwetu huo ni ugeni uliopo mbele yetu "alisema Kagondela. Mmoja kati ya waliokabidhiwa nyumba hizo Mwanabaraka Mchinga alishukuru kukabidhiwa nyumba yenye thamani ya sh. Mil. 4.3 alizochangia kidogo kidogo mpaka kukamilisha kiasi hicho na kukabidhiwa nyumba yake.

Mwanachama mwingine anayeishi kijijini hapo Monica Humba alisema ameona mafanikio makubwa kutoka ahamie kijiji cha wasanii kwa sababu anaishi maisha ya gharama ya chini kwa sababu kila kitu analima na kufuga mwenyewe. Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwanzega, Kitongoji cha Gomapembe Seif Katundu aliwashauri wasanii kuwekeza kijijini kwa kumalizia ujenzi wa nyumba kwa vile Serikali ya awamu  ya tano ni sikivu itatekeleza kero zote za wananchi wake za maji,barabara na zahanati.

SHIWATA ambayo mbali ya kuendesha matamasha ya wasanii wa fani mbalimbali pia inajenga nyumba kwa wanachama wake na kumiliki shamba la ekari 220 katika kijiji cha Ngarambe wilayani Mkuranga. Wakati huo huo uchaguzi wa viongozi wa SHIWATA utafanyika Januari 19,2019 kama ulivyopangwa awali na fomu zitaendelea kutolewa na kurudishwa mpaka Januari 4, mwakani ni mwisho.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad