HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 24, 2018

MKUU WA MKOA WA SIMIYU APEWA PONGEZI NA TBF ' MTAKA BASKETBALL TAIFA CUP'


Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Mashindano ya Kombe la Taifa la Kikapu Tanzania (Mtaka Basketball Taifa Cup 2018) yamemalizika katika viwanja vya Halmashauri ya mji wa Bariadi, Jumapili 23 Dec, 2018 ambapo timu ya mkoa wa Dar es Salaam imeshinda Mwanza 78 kwa 75 na kutwaa kombe hilo.


Katika mashindano hayo mshindi wa pili ni Mwanza, wa tatu Shinyanga na wa nne ni Arusha. Zawadi za vikombe, medali na tuzo zilitolewa kwa washindi, wachezaji nyota wa michuano hii na kila timu, mwalimu na mchezaji aliyeshiriki alipewa cheti cha ushiriki. 


Mashindano hayo yalifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu  Anthony Mkata, 17Dec, 2018 na yamefungwa na Rais wa Shirikisho la mpira wa kikapu Tanzania (TBF) Ndg. Phares Magesa tarehe 23 Dec 2018. 

Shirikisho la Mpira wa Kikapu Nchini (TBF) limetoa shukrani nyingi kwa kazi nzuri iliyofanywa na Mkoa wa Simiyu chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa  Anthony Mtaka, Katibu Tawala Jumanne Sagini, Mkurugenzi wa mji wa Bariadi, Afisa michezo wa mkoa wa Simiyu, Afisa Vijana wa Mkoa wa Simiyu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu pamoja na watendaji wote wa idara mbalimbali za Mkoa na wananchi wa Simiyu kwa ujumla kwa kufanikisha mashindano haya. 

Licha ya mkoa huu kuwa ni mchanga ila kupitia jitihada za Viongozi hao na wadau walioko Simiyu wameweza kujenga uwanja mzuri wa kisasa wa kikapu ambao utaendelea kutumika kukuza vipaji vya kikapu mkoani hapa, na pia wameweza kuzihudumia na kuzikarimu vizuri timu zote zikizofika katika Mashindano haya. 

TBF imekubali ombi la Mkoa huu kuandaa tena mashandano haya mwaka ujao ambapo yatafanyika Dec 2019 ambapo yataboreshwa zaidi kiufadhili na kimiundombinu ili kuwezesha timu za mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani ziweze kushiriki. 

Pia TBF imeahidi kusaidia mkoa huu kuwapatia mafunzo ya walimu wa kikapu na pia kupeleka mkoani Simiyu moja ya kambi kubwa za mafunzo ya vijana (Youth Clinics) ambazo zitaendeshwa 2019.

TBF inatoa nafasi kwa mikoa mingine kuomba nafasi ya kuandaa Taifa Cup kuanzia 2020 zianze maandalizi mapema kwa kutumia model ya Simiyu. 

Kupitia mashindano haya timu za Taifa zimeteuliwa na jopo la Makocha waliokuwa hapa Simiyu, jopo hilo lilijumuisha Makocha Ashraf Harun(DSM), Pascal Nkuba(Mwanza), na viongozi kutoka wa kamisheni za Ufundi, Waamuzi na Makocha waliokuwa hapa Simiyu. Majina ya timu zote 2 yatatolewa muda si mrefu mara baada ya kumaliza maandalizi husika ikiwa ni pamoja na kushauriana na wenzetu wa Zanzibar, na pia kushauriana na Kocha Mkuu wa Tanzania Ndg. Matthew McCollister na Makocha Wazalendo kuhusu mpango ya mafunzo ya timu hizo. 

Baada ya hapo tutangaza mipango ya kuziweka kambini timu hizi ili kuanza kuzinoa tayari kwa michuano ya Kimataifa ya Kikapu 2019. Wametoa  shukrani kwa kampuni ya Kiboko Paints ya Dar es Salaam ambayo imetoa msaada wa rangi katika ujenzi wa uwanja huu wa Kikapu wa Simiyu na  wafadhili wengine wote waliosaidia na waliozisadia timu za mikoa kuweza kushiriki mashindano haya. 

TBF wametoa wito kwa mikoa mingine nchini kuiga mfano wa Mkoa wa Simiyu jinsi walivyoweza kutumia rasilimali zake na wadau wake kuweza kujenga uwanja ndani ya muda mfupi na kuandaa mashindano makubwa kama haya. 

Kama shirikisho tunatoa wito kwa Viongozi wa Kitaifa na wa Mikoa, wafanyabiashara na wadau mbalimbali waendelee kushirikiana nasi ili kusaidia maendeleo ya Kikapu katika mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani, ikiwa ni pamoja na kujenga viwanja kama watu wa Simiyu walivyofanya, kufadhili ligi na mashindano mbalimbali yanayohusu vilabu na mikoa katika mikoa yao na pia kuwezesha vilabu na timu za mikoa kushiriki kikamilifu katika Mashindano ya Kitaifa kama National Basketball League (NBL), Kombe la Taifa (Taifa Cup), Kombe la Muungano, Karume Cup Zanzibar, Nyerere Cup, Kilimanjaro Cup n.k.

Mwaka 2019 Timu za Taifa za Tanzania za kikapu zitashiriki FIBA Zone V National teams Championship (Afrobasket 2019 Preliminaries), FIBA Zone V U16 National teams Championship na kama wakifanikiwa FIBA Africa U16 Finals (Boys & Girls) wameomba zifanyike Tanzania ambapo wamepewa masharti ya kuhakikisha wanakuwa na uwanja mpya mzuri wa ndani au tuboreshe uwanja wa sasa wa Taifa ili uwe na hadhi stahili. 

TBF wameomba  wafadhili na wadau tujitokeze kwa wingi kushirikiana na TBF kuendelea mchezo wa kikapu nchini kupitia ujenzi wa viwanja, na kufadhili ligi, mashindano na matukio yetu mbalimbali katika ngazi za mikoa, Taifa na Kimataifa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad