Na John Nditi, Morogoro
NAIBU Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa amesema , Serikali inatarajia kufanya usanifu wa barabara ya Morogoro- Dodoma yenye urefu wa kilometa zipatazo 259 katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 kwa ajili ya kupata michoro na gharama halisi ili kujengwa upya kwa viwango cha ubora na mahitaji ya sasa .
Naibu Waziri alisema hayo mjini Morogoro alipofanya ziara ya ukaguzi wa matengenezo ya barabara katika maeneo mbalimbali kutoka Dodoma hadi Moropgoro yakiwemo ya Kibaigwa , Gairo na kuangalia shughuli za ujenzi wa mizani mpya ya kisasa eneo la Dakawa Magereza barabara ya Morogoro- Dodoma .
Alisema , licha ya kuendelea kuihudumia barabara kuu hiyo , kwa sasa Serikali imekuja na mpango mwingine wa kufanya usanifu kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 ili kupata michoro ambayo itaelezea gharama halisi ya kujenga barabara mpya katika kiwango cha ubora na mahitaji ya sasa.
Naibu Waziri alisema, Serikali inatenga fedha nyingi kila mwaka fedha kwa ajili ya ukarabati wa barabara kuu ikiwemo ya Morogoro- Dodoma ili ziweze kutoa huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo ambapo kwa baabara hiyo iliyojengwa miaka zaidi ya 30 iliyopita kwa hali yake ya sasa imechakaa na kuzeeka.
Akizungumzia ujenzi wa mizani , Naibu Waziri alisema , Serikali itaendelea kujenga mizani ya kisasa katika barabara kuu nchini ambayo itapunguza msongamano wa magari na kuharakisha usafirishaji wa mizigo , abiria na pia kulinda barabara .
Naibu Waziri alisema ,mizani ya kisasa inayojengwa na iliyopo itakatoboreshwa ili ikidhi utoaji wa huduma zote muhimu kama vituo vya Polisi, TRA, ukaguzi wa magari, upimaji wa ulevi kwa madereva , kuengesha magari na maeneo ya kupumzika madereva .
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara ( TANROADS ) mkoa wa Morogoro, Mhandisi Doroth Mtenga alisema, ujenzi mzani hiyo ya kisasa ulianza Oktoba 25, 2017 kwa gharama ya Sh bilioni 14. 784 fedha zilizotolewa na Serikali kuu na hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 70 na kiasi cha malipo kwa mkandarasi kilicholipwa ni Sh bilioni 5.7 sawa na asilimia 40.
Mhandisi Mtenga alisema , mradi huo wa ujenzi wa mizani mbili za kisasa za kupima magari , eneo la Dakawa Magereza una majengo mawili ya ofisi, vibanda viwili vya Polisi , vinne vya mlinzi na vyoo viwili na ni moja wapo ya hatua za kudhibiti na kupunguza uharibifu wa barabara kutokana na magari kuzindisha uzito.
“ Hapa kutakuwa na mzani miwili mmoja utapima magari yakiwa kwenye mwendo mdogo na utarekodi na kuhifadhi taarifa zote za gari husika na gari itaruhusiwa kuendelea na safari iwapo hajazidisha uzito na ikiwa uzito umezidi litaelekezwa kwenda kupima kwenye mzani wa kawaida kwa uthibitisho” alisema Mtenga.
Hta hivyo alisema , ujenzi huo ulipangwa ukiamilishwe ifikapo Januari 24, 2019 , lakini kutoka na kuchelewa kupata eneo la upande mmoja wa ujenzi kwa zaidi ya miezi sita ambazo zilikuwa nje ya uwezo wa mkandarasi kutokana na ardhi kumilikiwa na Taasisi mbili tofauti za Serikali .
Mhandisi Mtenga alisema , kwa sasa mkandarasi wamewasilisha ombi la kuongezewa muda hadi Aprili 24, 2019, na kwamba Wakala utaendelea kumsimamia ili ujenzi huo ukamilishwe kwa wakati katika muda wa nyongeza ulioombwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa ( kaunda suti) akipata maelezo ya Mhandisi mkazi wa Kampuni ya uhandisi ya Ambicon , Mustafa Kasmir ( kulia) alipokagua shughuli za ujenzi wa mizani mpya ya kisasa eneo la Dakawa Magereza barabara kuu ya Morogoro- Dodoma hivi karibuni na ( anayemfuatia Naibu Waziri ) ni Meneja wa Wakala wa Barabara ( TANROADS ) mkoa wa Morogoro, Mhandisi Doroth Mtenga.
Naibu Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa ( kaunda suti) akisisitiza jambo wakati akikagua shughuli za ujenzi wa mizani mpya ya kisasa eneo la Dakawa Magereza barabara kuu ya Morogoro- Dodoma hivi karibuni na ( wapili kushoto) ni Meneja wa Wakala wa Barabara ( TANROADS ) mkoa wa Morogoro, Mhandisi Doroth Mtenga.
Naibu Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa ( kaunda suti) akikagua shughuli za ujenzi wa mizani mpya ya kisasa eneo la Dakawa Magereza barabara kuu ya Morogoro- Dodoma hivi karibuni akiongozwa na Mhandisi mkazi wa Kampuni ya uhandisi ya Ambicon , Mustafa Kasmir ( kulia) akiambatana na Meneja wa Wakala wa Barabara ( TANROADS ) mkoa wa Morogoro, Mhandisi Doroth Mtenga ( wapili kushoto) pamoja na Wakala wa Mradi kutoka Kampuni ya Group Six International Ltd , Mhandisi Abdallah Rashid.( Picha na John Nditi).
No comments:
Post a Comment