HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 14 November 2018

WANANCHI WANASHUHUDIA MAAJABU MAKUBWA NDANI YA MIAKA MITATU YA RAIS DKT.JOHN MAGUFULI-WAZIRI JAFO

Na Said Mwishehe, Dodoma

WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Rais Rais Dk.John Magufuli ikiwa imetimiza miaka mitatu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Suleiman Jafo amesema kuna mambo makubwa ya kujivunia ambayo yamefanyika ndani ya muda huo.

Pia ameeleza hatua kwa hatua namna ambavyo Wizara yake imeshiriki kikamilifu katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora katika sekta mbalimbali nchini huku akieleza namna anavyomsukuru Rais Dk.Magufuli kwa namna ambavyo amemuamini na kumteua kuhudumu nafasi hiyo.

Waziri Jafo ambaye ni miongoni mwa mawaziri vijana waliopata nafasi ya kuaminiwa na Rais Magufuli amesema hayo katika mahojiano maalumu na timu ya waandishi wa habari wa Michuzi Blog na Michuzi TV walipofika ofisini kwake katika Jiji la Dodoma.

Ambapo pamoja na mambo mengine mahojiano yalijikita katika kuzungumzia miaka mitatu ya Rais Magufuli na mchango wa Tamisemi katika kuleta mabadiliko ya kimaendeleo kwa Watanzania wote.

Waziri Jafo kabla ya kuelezea maendeleo makubwa ambayo yamefanyika kwenye sekta mbalimbali ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imebeba ajenda ya wananchi na hilo amekuwa akilizungumza mara kwa mara.

Amefafanua ajenda hiyo imetokana na kiu ya

wananchi ya kutaka mabadiliko na kwamba hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015 karibu Watanzania wote walisema wanataka mabadiliko.

“Watanzania wote walisema wanataka mabadiliko na hivyo kuundwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano kumetokana na ajenda ya wananchi ya kutaka mabadiliko. Rais Magufuli baada ya kuingia madarakani akawa anajua jukumu lake ni kuhakikisha anakwenda na kiu cha wananchi ya kuleta mabadiliko,”amesema Jafo.

Hivyo amesema wakati Rais Magufuli anatimiza miaka mitatu, kwanza kabisa anamshukuru kwa uamuzi wake wa kumchagua na kumkabidhi ahudumu kwenye wizara hiyo ya Tamisemi na kufafanua unapozungumzia Tamisemi maana yake unazungumzia maisha ya watu ya kila siku.

Jafo amesema ukiangalia bajeti ya nchi asilimia 21 iko chini ya wizara yake na asilimia 72 ya watumishi wote iko kwake.Pia miradi mingi ya maendeleo ya wananchi iko chini ya Tamisemi na hivyo Wizara hiyo ikishinda kutekeleza majukumu yake maana yake hata mabadiliko ya kimaendeleo nayo yatakwama.

“Wizara ya Tamisemi ndio inayohangaika na maisha ya wananchi ya kila siku na hivyo kwa ujumla wake lazima iwe na mikakati ya kuchagiza ukuaji wa maendeleo ya wananchi ili kufikia uchumi wa kati.Mwananchi akikosa huduma atalalamika na malalamiko yake yatakuwa yanafikisha ujumbe yale mabadiliko ambayo ameyategemea hayapo,”amesema.

Waziri Jafo amesema wakati Rais Magufuli akiwa ametimiza miaka mitatu , utabaini mtazamo wake umejikita kuleta mabadiliko kwa Watanzania wa kada zote kwa kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua kubwa ya kimaendeleo.

“Mtazamo wa Rais ni kwamba nchi yetu lazima ifikie uchumi wa kati na ili kufika safari hiyo lazima tuchague njia ya kupita ambayo ni ujenzi wa viwanda na ndio maana Serikali ya Awamu ya Tano inahimiza ujenzi wa viwanda.

“Katika kwenda na mtazamo wa Rais wangu mchapakazi ndio maana katika wizara yangu agizo langu la kwanza ilikuwa ni kufanikisha ujenzi wa viwanda.Nikatoa maagizo kwa wakuu wa mikoa wote nchini watenge maeneo ya ujenzi wa viwanda.Pia nikafanya tathimini iliyokwenda sambamba na kutoa maagizo ya kila mkoa kujenga viwanda 100 ndani ya miezi 12.Katika hilo tumefanikiwa,”amesema.

Waziri Jafo amesema wakati anatoa agizo la ujenzi wa hivyo viwanda wapo waliosema amekurupka lakini ukweli alikuwa anajua anachokifanya na hivyo kampeni hiyo imesaidia kwani kuna viwanda vidogo 2600 vimejngwa ndani ya miezi 12 na Desemba mwaka huu atapata taarifa rasmi.

Amesema kwa kawaida kidogo kinaajiri kuanzia watu sita mpaka watu mpaka 10 na hivyo ajira ambazo zimetengenezwa kutoka na kuhimiza ujenzi wa viwanda hivyo ni zaidi ya 7000.

Amesisitiza historia yake ya maisha yeye amezaliwa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto na ndio maana kwenye kampeni hiyo ya ujenzi wa viwanda hajarudi nyuma na hivyo wakati Rais anamimiza miaka mitatu kuna jambo ambalo wanajivunia kwani wamefika hapo kutokana na kufuata maagizo ya Rais.

Hivyo amesema unapozungumzia miaka mitatu ya Rais Magufuli,Tamisemi inajivunia kwa kutoa mchango wake mkubwa katika kuhakikisha wanaendana na kasi ya Rais katuka kuleta maendeleo ya wananchi na ndio maana ukienda maeneo mbalimbali nchini utaona kuna mambo makubwa yamefanyika.

Amesema wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani kulikuwa na changamoto ya uhaba wa vituo vya afya lakini kupitia Rais Magufuli kuna mabadiliko makubwa yamefanyika kwenye sekta hiyo na Watanzania ni mashahidi kwani yanayofanyika wanayaona kwa macho na wanafurahia.

“Katika miaka mitatu ya Rais Magufuli kwenye sekta ya afya hakika kuna maajabu makubwa yamefanyika na wananchi wengi wanaohojiwa wanaeleza kufurahishwa kwao kwani changamoto nyingi zimepata ufumbuzi wake,”amesema Waziri Jafo.

Kuhusu sekta ya elimu anasema baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani aliamua kuja na mkakati maalumu wa kutoa elimu bure ambapo zaidi ya Sh.bilioni 20 zinatolewa na Serikali kwa kila mwezi .Hali hiyo imesaidia kuondoa changamoto ambayo wazazi wengi walikuwa wanakutana nayo ya kushindwa kuwapeleka watoto shule kwasababu ya kukosa ada.

Amesema mbali ya elimu bure Serikali imendelea kukarabati shule kongwe nchini  huku akiweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha elimu inayopatikana katia shule za serikali inakuwa bora na tayari matunda yameanza kuonekana kwani Shule ya Sekondari Kibaha imeshika nafasi ya kwanza kitaifa kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha sita.

Pia amesema fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nayo imeongezeka kwa kuhakikisha wenye sifa wote wanapata mkopo tena kwa wakati na ndani ya miaka mitatu ya Rais Magufuli , wanafunzi wengi wamekuwa wakipata fedha hizo na ndio maana hakuna tena malalamiko.

Waziri Jafo amesisitiza kuna mambo mengi yamefanyika kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na kwa mipango iliyopo kuna hatari ya Watanzania waliondoka nchini mwaka 2010 wakiamua kurudi mwaka 2020 itabidi washikwe mkono kwani watapokea maeneo waliyokuwa wanaishi.

“Kwangu niseme tu kuna mambo mengi makubwa ambayo yamefanyika katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Dk.Magufuli.Amerudisha nidhamu ya kazi.Usimamizi wake mzuri umesaidia kuongezeka kwa ukusanyaji wapato.Hakika kuna mambo mengi amefanya na kwetu sisi ni kuendelea kumuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kumpa afya njema ili aendelee ,kuwatumikia Watanzania wote,”amesema Waziri Jafo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad