HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, 7 November 2018

UBA Benki kuwajengea nyumba watoto pacha waliotenganishwa Muhimbili

Mama wa Watoto pacha waliotenganishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo wamekabidhiwa hundi ya shilingi milioni 16 na elfu 80 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ili kuwawezesha watoto hao kuishi katika makazi bora. Msaada huo umetolewa na United Bank for Africa (UBA), ambapo pia watoto hao wamepatiwa bima ya afya ya miaka kumi pamoja na kuwafungulia akaunti yenye akiba ya shilingi milioni mbili.

Akikabidhi msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Mwegelo amesema mafanikio ya kutenganishwa kwa watoto hao yametokana na maboresho makubwa ya utoaji wa huduma za afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

‘’Nawapongeza Muhimbili kwa upasuaji huu wa kihistoria, utoaji wa huduma hapa Muhimbili umeboreshwa sana hata malalamiko yamepungua ili juhudi hizi zisiende bure naahidi Serikali ya Kisarawe tutaendelea kuwafutilia watoto hawa na kuhakikisha yaliyoahidiwa yanatimizwa.’’Amesisitiza mkuu huyo wa wilaya.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru amesema Muhimbili imetumia takribani shilingi milioni 34 kuwahudumia watoto hao katika kuhakikisha upasuaji huo wa ubingwa wa juu unafanyika kwa mafanikio makubwa.

 ‘’Watoto hawa tuliwapokea mwezi wa saba mwaka huu, kama hospitalli tuliona tuangalie namna ya kuwasaidia mara watakaporuhusiwa, hivyo wataalam wetu wa ustawi wa jamii walienda kuona mazingira wanayoishi na kushuhudia mazingira hayo si rafiki hasa kwa watoto hawa ambao wamefanyiwa upasuaji mkubwa’’. Amesema Prof. Museru.

‘’Suala hili tuliamua tulipe kipaumbe ili juhudi zetu za kuwatenganisha zisipotee bure, juhudi zilifanywa tukatafuta misaada kwa wadau mbalimbali  tunamshukuru sana Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe kwa juhudi zake hatimaye suala hili leo limefanikiwa’’. Amesema Prof. Museru.

Pia, Prof. Museru amesema MNH iatendelea kuwapatia matibabu bure watoto hao mpaka pale watakapofikia umri wa kujitegemea katika Maisha yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya UBA Bwan. Usman Isiaka ameeleza kuwa waliona mazingira wanaoshi wazazi wa watoto hao yanachangamoto hivyo wakaamua kuwasaidia ili wapate makazi bora.

‘’UBA benki itashiriki kwenye ujenzi, itasimamia na kuhakikisha ujenzi wa nyumba hiyo mpaka unakamilika. Natoa wito kwa wadau wengine pamoja na watu binafsi kuendelea kuwachangia watoto hawa kwani wanaendelea kukua na watahitaji kwenda shule’’. Amesema Mkurugenzi huyo wa benki ya UBA.

Upasuaji wa kuwatenganisha watoto walioungana ulifanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa mara ya kwanza mwaka 1994.
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Mwegelo akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kabla ya kumkabidhi Ester Simon na mumewe, Michael Mkono hundi ya Tshs. 16,080,000 leo. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru, Mkurugenzi Mtendaji wa UBA, Usman Imam Isiaka na kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa wa benki hiyo, Dominick Timothy.
Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili (MNH), Prof. Lawrence Museru akizungumza kwenye mkutano huo leo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Mwegelo.
Michael Mkono ambaye ni mume wa Ester Simon akiwa kwenye mkutano huo leo kabla ya kukabidhiwa hundi hiyo.
Ester Simon akiwashukuru wataalam wa Muhimbili kwa kumpatia matibabu ya kibingwa pamoja na uongozi wa UBA benki kwa kumkabidhi hundi ya fedha za ujenzi wa nyumba ya kisasa.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad