HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 27, 2018

Tanzania na China zasaini makubaliano ya sh Bil. 22.4 kujenga Chuo cha VETA Kagera

 Serikali za Tanzania na China zimetia saini makubaliano ya ujenzi wa Chuo cha Mkoa wa Kagera utakaogharimu Shilingi za Kitanzania bilioni 22.4 zikiwa ni ufadhili kutoka serikali ya China.

Makubaliano hayo yametiwa saini leo tarehe 26 Novemba 2018 na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Taknolojia Dkt. Leonard Akwilapo aliyeiwakilisha Serikali ya Tanzania na Yuan Lin, Mwakilishi Mkuu wa Uhusiano wa China na Tanzania katika masuala ya Kiuchumi na Kibiashara aliyeiwakilisha Serikali ya Watu wa China. 

Hafla ya kutia saini makubaliano hayo ilifanyika katika ofisi za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na wawakilishi mbalimbali wa pande zote mbili, ambapo kwa upande wa Tanzania miongoni mwa waliohudhuria na kushuhudia utiaji saini huo ni pamoja na Mkurugenzi wa  Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET), Dkt. Noel Mbonde; Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Peter Maduki; Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Dkt. Pancras Bujulu na Mkurugenzi Msaidizi wa TVET, Enock Kayani.

Akizungumza wakati wa kutia saini makubaliano hayo, Dkt. Akwilapo alisema ujenzi huo unatarajiwa kuanza mara moja na  utachukua takribani miezi 18 kukamilika na kwamba unaongeza mchango katika kuandaa nguvukazi kwa ajili ya Uchumi wa Viwanda nchini. 

Alisema, baada ya kukamilika chuo hicho kitakuwa ana uwezo wa kudahili wanafunzi 400 katika kozi za muda mrefu na zaidi ya 1000 kozi za muda mfupi huku kikiwa na nafasi za bweni 200 kwa wanafunzi wa kiume na 120 kwa wanafunzi wa kike. 

Kwa upande wake, Yuan Lin alisema kuwa ujenzi wa Chuo hicho ni sehemu ya uendelezaji mahusiano mema kati ya China na Tanzania na kwamba unaonesha uhalisia wa China kuunga mkono kwa vitendo juhudi za Tanzania kuelekea katika uchumi wa viwanda. 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt Pancras Bujulu licha ya kuishukuru serikali ya China kwa msaada huo, alisema kuwa VETA kwa kushirikiana na serikali mkoani Kagera tayari wameshaweka miundombinu muhimu kwa ajili ya kuwezesha shughuli za ujenzi wa chuo hicho kuanza mara moja.

Aliitaja miundombinu iliyoandaliwa kuwa ni pamoja na kuboresha barabara iendayo kwenye eneo la ujenzi wa chuo kwa kuichonga na kuitengeneza kwa kiwango cha changarawe; kuvuta umeme hadi kwenye eneo la ujenzi na kutengeneza chanzo cha muda cha maji kwa ajili ya shughuli za ujenzi. 

Aliongeza kuwa wakati chuo hicho kikitarajiwa kuanza kujengwa, tayari walimu 20 kutoka VETA wamekwenda nchini China kujifunza namna ya uendeshaji wa vyuo vya ufundi stadi ikiwa ni sehemu mojawapo ya kuimarisha mahusiano katika uendeshaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi. 
Alisema, VETA inaendelea kuongeza juhudi za ujenzi na upanuzi wa vyuo na nia ni kuhakikisha kila mkoa una chuo cha elimu na mafunzo ya ufundi stadi chenye hadhi ya Kimkoa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad