RPC ARUSHA ATOA AHADI YA “KUMWAGA” VIFAA VYA TAEKWONDO - MTAA KWA MTAA BLOG

HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 12 November 2018

RPC ARUSHA ATOA AHADI YA “KUMWAGA” VIFAA VYA TAEKWONDO

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Baada ya kuchukua ubingwa wa Nane Nane Championship ulioshirikisha timu kumi kati ya hizo tatu toka nchini Kenya, timu ya Taekwondo ya Polisi Arusha imeahidiwa vifaa vilivyokosekana katika Gym lao ili liweze kukamilika kila idara.

Ahadi hiyo ilitolewa jana asubuhi na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi mara baada ya kukabidhiwa kombe la ubingwa huo toka kwa timu hiyo.
“Pamoja na changamoto kadhaa lakini mlitambua umuhimu wa mashindano hayo na mlionyesha uzalendo wa hali ya juu ambao umesaidia kuliwakilisha vyema Taifa letu na Jeshi la Polisi kwa kupata ubingwa ambao umekuwa fahari yetu sote, hivyo mimi kama mlezi wa timu hii naahidi kuendelea kutoa vifaa vya mazoezi ili liweze kukamika” Alisema Kamanda Ng’anzi.

Kwa upande wake Mwalimu wa timu hiyo Master shija Shija alisema ushindi wa timu hiyo ulitokana na nidhamu, kujituma kwa wachezaji lakini pia kufuatilia maelekezo yake.

“Hawa ni askari huwa wanatii na kuheshimu kila wanachoelekezwa lakini pia uungwaji mkono wa Kamanda wa Polisi umekuwa chachu ya ushindi kwani wachezaji wamekuwa na morali ya hali ya juu” Alisema Master Shija.

Kwa upande wake askari wa kike Edith Msafiri, alisema kwamba anajisikia furaha sana kushiriki mchezo huo kwa kuwa unamsaidia katika kazi yake kutokana na ujuzi alioupata na anaoendelea kuupata unaomuwezesha kupambana na wahalifu bila hata kulazimika kutumia silaha.

Timu hiyo ilichukua ubingwa huo katika mashinadano yaliyofanyika tarehe 3 na 4 mwezi huu katika ukumbi wa Triple A kwa kupata Medali 27 kati ya hizo Nane zilikuwa za Dhahabu, Saba za Fedha na 12 za Shaba wakati nafasi ya Pili na Tatu ilichukuliwa na Kilifi na Regional zote za nchini Kenya. 

Aidha Kamanda Ng,anzi alisema mbali na kuwepo kwa timu hiyo pia Jeshi la Polisi mkoani hapa limeanzisha Programu ya kushirikisha askari wote kila Ijumaa ili kila mmoja ashiriki katika mchezo anaoutaka kama vile riadha, Mpira wa miguu, Mpira wa Pete, kunyanyua vyuma “Gym” na kadhalika  kwa nia ya kuimarisha afya zao.
 Nahodha wa timu ya Taekwondo ya Polisi Arusha Yohana Nicodem akimkabidhi Kombe la ubingwa wa Nane Nane Taekwondo Club Championship Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Arusha (SACP) Ramadhani Ng'anzi mara baada ya timu hiyo kuwasili ofisini kwake.
  Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi akinyanyua kombe juu mara baada ya kukabidhiwa na nahodha wa timu ya Polisi Arusha Taekwondo askari Polisi Yohana Nicodem (kushoto kwake) huku wachezaji wengine wakishangilia. (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha)
 Askari wa kike Edith Msafiri (Kushoto) akionyesha umahiri wa kukwepa na kupangua teke la askari mwenzake Eva Laswai katika mpambano usio rasmi uliofanyika Makao Makuu ya Polisi Arusha kabla ya kumkabidhi kombe la ubingwa mlezi wa timu ya Arusha Polisi Taekwondo Kamanda wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng'anzi
 Askari wa kike wa timu ya Taekwondo ya Polisi Arusha Eva Laswai akipiga  " Kick Pad Target" iliyokuwa juu zaidi ya kichwa chake kwa teke huku Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha (SACP) Ramadhani Ng'anzi akimshuhudia. (Picha na Rashid Nchimbi wa Polisi Arusha)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad