HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 31 October 2018

TRA yachangia Milioni 25 ujenzi wa maabara ya Kompyuta Misitu Sekondari

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imechangia kiasi cha Shilingi Milioni 25 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya Kompyuta katika shule ya Sekondari Misitu iliyopo Wilaya ya Ilala, jijini Da es Salaam.
Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere, ametoa mchango huo ikiwa ni sehemu ya kuchangia maendeleo kwa jamii alipokuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 9 ya kidato cha Nne katika shule hiyo ambapo wanafunzi 205 wanaotarajia kuhitimu masomo yao mara baada ya kufanya mtihani wa Taifa mwezi Novemba 2018.
Kamishna Mkuu Bw. Kichere, amesema kuwa kiasi hicho cha fedha kitachangia ujenzi wa Maabara ya Kompyuta na kuwafanya wanafunzi kujifunza na kuongeza uelewa zaidi wa  masuala ya Teknolojia.
“Nimesikia katika changamoto mlizozitaja kuwa mnahitaji jengo la maabara ya kompyuta, uzio pamoja na jengo la utawala na mimi nimeona vyema nichangie ujenzi wa jengo hilo ili wanafunzi wapate kujifunza na kuwa na uelewa wa teknolojia kwani dunia sasa inatumia zaidi teknolojia ya habari na mawasiliano katika kuleta maendeleo”, alisema Kichere
Aidha, Bw. Kichere aliongeza kuwa, ujenzi na maendeleo ya shule za serikali unatokana na kodi hivyo aliwataka wanafunzi, walimu na wazazi kuwa na utamaduni wa kudai risiti za mashine za kielektroniki (EFD) ili kuchangia Mapato yatakayotumika kuboresha ujenzi na uboreshaji wa shule pamoja na shughuli mbalimbali za kijamii.
Bw. Kichere alisisitiza kuwa matunda ya kodi zinazopatikana pia hutumika kuboresha huduma mbalimbali za jamii kama vile ununuzi wa vitabu kwa ajili ya maktaba, utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, ujenzi wa madarasa, mabweni, nyumba za walimu na ununuzi wa vifaa vya maabara na kufundishia.
“Hivyo, natoa wito kwenu wahitimu, wazazi, walimu pamoja na wanafunzi kwa ujumla kuwa mabalozi wazuri wa masuala ya kodi na kuifundisha jamii umuhimu wa kulipa kodi popote mtakapokuwa” alisisitiza Kamishna Mkuu wa TRA.
Kamishna Mkuu pia alifafanua juhudi za Mamlaka ya Mapato Tanzania kuanzisha Vilabu vya kodi katika shule za sekondari kuwa ni kuwaandaa walipakodi wa baadaye ambao ni wazalendo pamoja na mabalozi wa mafanikio ya ulipaji kodi wa hiyari.
“Tunaamini kwa kufanya hivi tutakuwa na Taifa la watu wazalendo wanaopenda kuchangia maendeleo ya nchi yao kupitia kodi wanazolipa kwa hiari”, alisema Kichere
Bw.Kichere aliwapongeza wanafunzi na uongozi wote wa shule kwa juhudi mbalimbali wanazozifanya kuhakikisha shule hiyo inafanya vizuri mbali na Changamoto za vitendea kazi na madarasa walizonazo, ambapo shule imeongeza ufaulu kutoka asilimia 50 mwaka 2010 hadi asilimia 63.5 kwa mwaka 2017.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shule Bw. Malima Clement ameishukuru TRA kwa kuchangia ujenzi wa jengo la maabara ya kompyuta na kuahidi kushirikiana na wajumbe wa Bodi ya shule pamoja na wazazi kuhakikisha Kompyuta pamoja na vifaa vingine mbalimbali vinapatikana kwa ajili ya wanafunzi kujifunza pindi jengo litakapomalizika.
Shule ya Misitu ni moja kati ya shule zenye Vilabu vya Kodi kwa shule za Sekondari ambapo kwa mwaka huu 2018 ilishika nafasi ya tatu kwa upande wa uwasilishaji mada zinazohusu masuala mbalimbali ya kodi katika mashindano ya 11 ya vilabu vya kodi kwa mikoa wa Dares Salaam na Pwani yaliyofanyika katika chuo cha kodi.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (mwenye skafu) akimkabidhi cheti mwanafunzi bora katika masomo yote wa kidato cha nne katika shule ya Sekondari Misitu iliyopo Kivule Jijini Dar es Salaam, Richard Sagwe wakati wa Mahafali ya kidato cha nne shuleni hapo.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere akiwahutubia Wanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya Sekondari Misitu iliyopo Kivule Jijini Dar es Salaam wakati wa Mahafali ya kidato cha nne shuleni hapo.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (mwenye skafu) akiangalia baadhi ya kazi mbalimbali za Sanaa zinazofanywa na Wanafunzi katika shule ya sekondari Misitu iliyopo Kivule Jijini Dar es Salaam wakati wa Mahafali ya kidato cha nne shuleni hapo.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (mwenye skafu) akiwa ameongozana na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Bw. Richard Kayombo (kushoto) pamoja na uongozi wa shule ya sekondari Misitu iliyopo Kivule Jijini Dar es Salaam wakati wa Mahafali ya kidato cha nne shuleni hapo.
(PICHA ZOTE NA TRA)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad