HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, October 4, 2018

TAASISI YA MAENDELEO YA JAMII TENGERU YADHAMIRIA KUPAMBANA NA UKEKETAJI, NDOA NA MIMBA ZA UTOTONI

 Kaimu Mkuu wa Taasisi ya  Maendeleo ya Jamii Tengeru Dkt. Bakary George akifungua mdahalo wa kujadili masuala ya Mimba na Ndoa za utotoni pamoja na ukeketaji uliofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru.
 Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Bw. Christopher Mushi akieleza lengo la mdahalo  kwa wajumbe wa mdahalohuo  uliojadili masuala ya Mimba na Ndoa za utotoni pamoja na ukeketaji uliofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru.
Wadau na wanafunzi  mbalimbali wakifuatilia kwa makini mdahalo wa kujadili masuala ya Mimba na Ndoa za utotoni pamoja na ukeketaji uliofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru. Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano- WAMJW

Na Mwandishi Wetu- Arusha
Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru imeadhimiria kupambana na vitendo vya ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni kwa kuzalisha wataalamu wa maendeleo ya jamii ambao watasaidia kutoa elimu na kuhamasisha jamii ili kuondokana na ukatili huu wa kijinsia ambao kwa kiasi kikubwa humkosesha haki mtoto wa kike katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru Dkt.  Bakari George wakati akifungua mdahalo wa siku moja uliofanyika Chuoni hapo wenye lengo la kujadili changamoto ziwapatazo watoto wa kike na kusababisha kukatiza ndoto zao kuelekea mafaniko ya kimaisha.

Aidha Mkuu huyo wa Chuo aliwataka washiriki wa mdahalo huo kujadiliana kwa uwazi ili kutoa fursa kwa washiriki wa mdahalo huo kupata elimu sahihi ya changamoto zinazowakabili watoto wa kike na kuwa kikwazo kwao kufikia ndoto zao kielimu lakini pia kutoa fursa kwa wanafunzi wa chuo chake kutambua namna bora kukomesha vitendo vya ukatili kwa kuwa itakuwa jukumu la kiutendaji kwa kwakuwa wao ni wataalamu wa maendeleo ya Jamii.

Dkt. Bakari amesema kuwa vijana ni waathirika wakubwa wa mimba na ndoa za utotoni ikiwemo tatizo la ukeketaji hususani katika mikoa ambayo inaongoza kwa mimba na ndoa za utotoni na ukeketaji tatizo ambalo kimsingi linatokana na mila na desturi potofu hapa nchini.

Kwa upande wa Mzee wa mila za kimasai Julius Lukumay kutoka Wilaya ya Arumeru alisema kuwa kwasasa jamii ya wamasai  wameanza kutambua kuwa ukeketaji ni kosa la kisheria na taratibu wanabadilika kimtizamo kuhusu mtoto wa kike na kueleza kuwa wataendelea kutoa elimu kwa wanajamii kuondokana na tamaduni na mila zenye madhara zinazochangia ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni.

Naye Kiongozi wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru Annaglory Swai   akichangia katika mdahalo huo amesema jamii ya watanzania iachane na mila potofu ambayo imejengeka miongoni mwa Jamii zetu kuwa unapomsomesha mtoto wa kike unakuwa unasomesha mke wa mtu.

 Bi. Annaglory alisistiza kuwa binti anapochumbiwa akiwa mdogo anapata watoto katika umri mdogo na hasara kubwa kiuchumi kwa sababu Serikali inalazimika kugharimia idadi kubwa ya watoto inayopatikana kutokana na uelewa mdogo wa Afya ya uzazi lakini pia tatizo hili linachangia kuongezeka kwa umasikini katika Nchi kutokana na mabinti kushindwa kuchangia katika pato la Taifa kwa sababu ya ukosefu wa pato la uhakika.  

Mdahalo huo unafanyika kutokana na maazimio ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike iliyofanyika Kitaifa Mkoani Arusha mwaka 2017 na kutaka masuala ya ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni ziwe na mjadala mpana nakufanyika  katika ngazi ya Taasisi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad