HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 15 October 2018

NEEC kuwawezesha kiuchumi walioacha matumizi dawa za kulevya

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIKA harakati za kutaka kuokoa nguvu kazi ya vijana walioathirika na madawa ya kulevya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kuchumi (NEEC) limepanga kuandaa program kabambe ya kuwawezesha kwa waliokubali kuachana na matumizi ya madawa hayo baada ya kupata tiba kutoka vituo vya tiba ili wakazalishe mali.

Mwenyekiti wa baraza hilo Dkt. Festus Limbu amesema hayo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa juma wakati wa kikao na vijana waliokuwa wanatumia dawa hizo na ambao wanapata tiba katika vituo vya Hospitali ya Muhimbili, Temeke na Mwananyamala, kuwa baraza limejipanga kuwaletea program ya uwezeshaji ili waweze kujiletea maendeleo.

“Baraza limejipanga kuokoa kundi lenu hasa kwa wale waliokubali kuachana matumizi ya madawa ya kulevya na waopata tiba katika vituo mbalimbali nchini,” uwezeshaji unaolengwa ni wa kupata ardhi, mafunzo, mitaji na masoko, aliongeza kusema, Dkt Limbu.

Alisema uwezeshaji huo utawafikia baada ya kuwachambua kulingana na shughuli wanazoweza kufanya kupitia vikundi ambavyo vitaundwa ili kutoa fursa ya kuwawezesha kwa karibu zaidi.

Akitoa mfano alisema kwa wale watakao kubali kwenda katika kilimo watatakiwa kuwa katika kikundi cha watu 20 na watapatiwa kila mmoja heka tano na milioni tano na baada ya miaka mitano wawe wamerudisha mkopo huo.

Aliutaka uongozi wa Mamlaka ya Kudibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya na vituo vya kuwapatia tiba kuona namna ya kufanya ili kusudi serikali iweze kuwafikia kwa ukaribu.

Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Bi. Beng’i Issa amewataka watu hao kutokata tamaa na kutokubali kunyanyapaliwa bali wajitambue na kuona wanaweza kufanya shughuli za uzalishaji mali kama wengine na hiyo itasaidia ndoto zao za awali kuzaa matunda.

“Nawaombeni nyinyi ni vijana msikubali kukata tamaaa na katika uwezeshaji tunasema wewe ni mtu muhimu,” lakini kubali kuwa umetoka kule na sasa unataka kuanza maisha mapya ambayo yatajenga hatua nyingine, aliongeza kusema, Bi. Issa.

Aliwataka kutokubali kukatishwa tamaa wala kunyanyapaliwa bali wajiamini na kufanya yale mazuri na kutumia fursa hiyo kupambana na maisha ili wakajenge familia, na kupata elimu ya kujitambua na kutobadili msimamo wa kutotumia dawa hizo za kulevya.

Baraza lipo tayari kufanya kazi nao  na anataka kuona wanataka wakafanye shughuli zitakazo wazalishia mali na kubadilisha maisha na kunahitajika kutengeneza kanzi data ya wasifu wenu ili kujua unataka kufanya kazi gani katika fursa nyingi zilizopo nchini.

Kamishina wa Kinga na Tiba Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa la Kulevya, Dkt. Peter Mfisi alisema alisema vijana au watu waliokubali kuachana na madawa ya kulevya Dar es Salaam kuna vituo vitatu (Medical Assisted Theraphy)  vya Hospitali ya Muhimbili, Temeke na Mwananyamala.

“Watu wanaopata tiba wapo wengi wanafika 5,000 lakini waliofika hapa ni kama wawakilishi tu,” wakishapata tiba na kuachana kabisa kutumia wanatakiwa wakafanye kazi za kuendesha maisha yao, aliongeza kusema, Dkt. Mfisi.

Alisema uwezeshaji huo ni muhimu kwao kwa vile utawasaidia kutokuwa na msongo wa mawazo kutokana na kukosa kazi ya kufanya, sababu wengi walikuwa na mali wakauza na walitengwa na familia zao.

Bw. Kassim Rashid ambaye anapata tiba kituo cha Hospitali ya Mwananyamala amesema program hiyo imefika katika mwafaka kwa vile wamekubali kuachana na matumizi dawa za kulevya ili wakawe sehemu ya nguvu kazi ya taifa.

“sisi tumekubali kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya na tunapongeza mkakati wa serikali wa kutuwezesha tukafanye kazi,” na sisi lazima tuone umuhimu huu na tusirudi tena katika madawa.
 Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC),Dkt. Festus Limbu wa pili kushoto akisistiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na vijana wanaopata tiba ya kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya wa Vituo vya Hospitali ya Muhimbili, Temeke na Mwanyanyamala, wa tatu kulia ni Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Bi. Beng’I Issa, wa pili kulia ni Mjumbe wa baraza hilo, Bi. Dkt. Astronaut Bagile, kushoto Kamishina wa Kinga na Tiba Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya na kulia afisa toka baraza hilo, Bw. Jozaka Bukuku.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi (NEEC),Dkt.Festus Limbu kushoto akifafanua jambo wakati alipokuwa akizungumza na vijana wanaopata tiba ya kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya katika Vituo vya Hospitali ya Muhimbili, Temeke na Mwananyamala wengine ni vijana hao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad