HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 11 October 2018

MAKUMBUSHO YA NYERERE KUFANYIWA DUA BAGAMOYO

FAMILIA ya sheikh Mohammed Ramiya, imeiangukia serikali na wizara ya utalii kuangalia uwezekano wa kuweka sehemu ya kumbukumbu kati ya hayati sheikh Ramiya na Mwl.J.K Nyerere, eneo la Zawiyani kata ya Dunda,Bagamoyo ili kuenzi historia ya ukombozi wa nchi yetu .

Aidha familia hiyo inakumbuka wakati marehemu sheikh Ramiya (78) akiugua kabla ya kufikwa na umauti wake mwaka 1985 ,Mwl. Nyerere alimchukua kumuuguza nyumbani kwake Msasani jijini Dar es salaam .

Akizungumzia namna anavyomkumbuka hayati Mwl.Nyerere, wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, mtoto wa mwisho wa sheikh Ramiya, aitwae Ramiya Mohammed Ramiya alisema ,watalii wengi wakienda kwenye makumbusho za Bagamoyo wanakuta historia ya sheikh huyo na hayati Mwl. J.K Nyerere .

Alieleza watalii hao, huwa na shauku ya kwenda kujua historia ya picha na nyumba aliyokuwa akienda kufanyiwa dua muasisi huyo ,kisha kubarikiwa kwenda kuikomboa nchi mwaka 1961.

Ramiya alisema ,enzi hizo mwalimu Nyerere alikuwa rafiki wa sheikh Ramiya ,na alipelekwa huko na wazee wa Dar es salaam kwa nia ya kuombewa dua kwa ajili ya kupata uhuru bila kumwaga damu .

"Tukiacha marehemu baba kupigania uhuru,kuheshimika lakini pia sheikh Ramiya alikuwa mtu wa dini hivyo tutapendezwa kama serikali itatambua umuhimu wa kuweka makumbusho hiyo hapa basi iwe ya kidini zaidi " 

"Historia itakuwa haipotei ,lakini iwe tofauti kwa kuwa ni sehemu ya dini ,haitowezekana eneo hilo watu wakawa nje ya maadhi ya kiislamu ,isiruhusiwe wadada kwenda vichwa wazi ,ama kuvaa suruali bila kujistili " alibainisha Ramiya .

Hata hivyo alieleza ,Mwalimu Nyerere kubwa alilokuwa akifanyiwa na baba yao ni dua, kwa ajili ya ukombozi ili kupata uhuru wa nchi ambapo nyumba iliyokuwa ikitumika kufanyiwa dua ina karne mbili kwasasa.

Mtoto huyo alifafanua ,nyumba hiyo imeshakuwa gofu imejengwa kwa mawe na Sheikh Ramiya aliirithi kwa baba yake .

"Baba alikuwa mtu mwenye kalama zake ,Allah alimpa uwezo wa kukuombea kitu ukafanikiwa ,aliwahi kusimama na hayati Mwl.Nyerere juu ya maji ,sio nchi kavu ikiwa ni sehemu ya dua zake ,alishawahi kupelekwa makaburini na kutakiwa kufunga ili kupata maombi kwa ajili ya nchi " alisisitiza Ramiya .

Nae Mzee Salum Maftaha alisema ,ukifika Bagamoyo kutaka kujua historia ya Mwalimu, basi huwezi kuacha kumgusia sheikh Ramiya.

Alisema, historia ya Tanganyika kupata uhuru huwezi kutenganisha Uhuru wa watu wa Bagamoyo  na maisha ya baba wa Taifa kwani yapo aliyofanya akipitia Bagamoyo .

Maftaha alieleza , waasisi  akiwemo Mwl J.K .Nyerere aendelee kukumbukwa kwa juhudi zake na kuendeleza kutumia busara na hekima zake.

Mzee mwingine Juma Hussein aliwataka vijana wapikwe kisiasa ili kuwekezwa kwa manufaa ya chama na taifa kwa miaka ijayo.

Alisema ,kijana anaedharau wazee atambue anapotea kwani kuna ulazima wa kuiga mema ambayo waliyafanya wazee katika nchi na kuendelea kujifunza kwao.

Awali mwenezi wa chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Bagamoyo ,John Francis (Bolizozo),aliwataka viongozi wa chama kuanzia ngazi ya chini ,kufuata maadili na miiko ya kiungozi kama ilivyo kwenye machapisho ya vitabu mbalimbali vilivyochapishwa enzi za marehemu baba wa taifa hayati Mwl.J.K.Nyerere.

Alieleza ,kuimarisha chama na kuendeleza sifa zake ni lazima viongozi waliopo wakasimamia maadili ipasavyo.

Ni miaka takriban 19 sasa tangu atutoke muasisi na Rais wa awamu ya kwanza nchini ,marehemu Mwl.J.K Nyerere.
 Mtoto wa mwisho wa sheikh Ramiya ,aitwae Ramiya Mohammed Ramiya akielezea namna anavyomkumbuka hayati Mwl. J. K .Nyerere huko Zawiyani ,Bagamoyo. (Picha na Mwamvua Mwinyi)
 Mtoto wa mwisho wa sheikh Ramiya   ,aitwae Ramiya Mohammed Ramiya (wa kulia )akionyesha historia ya  nyumba aliyokuwa akienda kufanyiwa dua muasisi hayati Mwl.J.K Nyerere ,kisha kubarikiwa kwenda kuikomboa nchi mwaka 1961, nyumba ambayo kwasasa ina karne mbili  , imekuwa gofu na ilijengwa kwa mawe ,(wa kushoto) ,Mwenyekiti wa CCM Bagamoyo alhaj Abdul Sharif .
 Jumba lenye historia aliyokuwa akienda kufanyiwa dua muasisi hayati Mwl.J.K Nyerere ,kisha kubarikiwa kwenda kuikomboa nchi mwaka 1961, nyumba ambayo kwasasa ina karne mbili  , imekuwa gofu na ilijengwa kwa mawe ,ipo eneo la Zawiyani ,Dunda wilayani Bagamoyo.
Mtoto wa mwisho wa sheikh Ramiya, aitwae Ramiya Mohammed Ramiya, akionyesha historia ya picha mbalimbali baina ya hayati sheikh Ramiya na Mwl. J.K. Nyerere.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad