HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 2 October 2018

Dkt. Mwakyembe avipa wiki mbili vilabu ya mchezo wa Kriketi kujisajili

Na Lorietha Laurence-WHUSM,Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa wiki mbili kwa vilabu vyote vya mchezo wa Kriketi nchini ambavyo havijasajiliwa  kufika Baraza la Michezo La Taifa kwa ajili ya kujisajili .
Akizungumza na wadau hao wa mchezo huo jana katika Ukimbi wa mikutano  uliopo Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, Dkt. Mwakyembe ameeleza kuwa ni wajibu wa kila kilabu cha mchezo nchini kufuata sheria na taratibu zinazosimamia sekta ya michezo.
“Kama kuna kilabu chochote cha mchezo wa kikreti kipo na hakijasajiliwa, natoa wiki mbili  kuweza kufuata taratibu na sheria za usajili ili viweze kutambulika kisheria ” alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha aliongeza kwa kuutaka uongozi wa Chama cha Kriketi Tanzania kuhakikisha unatenga siku moja  kwa ajili ya mkutano na wanachama wake ili kupata nafasi ya kupitia vipengele vinavyounda katiba ya chama hicho kwa ajili ya maboresho mbalimbali.
Vilevile Waziri Dkt. Mwakyembe  alipata fursa ya kusikiliza changamoto mbalimbali  zinazokikabili chama hicho cha mchezo wa Kriketi na kuhaidi kuzifanyia kazi changamoto hizo.
Kwa Upande wake Kaimu Katibu  Mtendaji wa Baraza la Michezo  la Taifa Bw.Makoye  Nkenyenge amewataka wanachama hao kufanyia kazi maagizo yaliyotolewa na Waziri Dkt. Mwakyembe kwa kuhakikisha wanasajili vilabu vyote ambavyo havijasajiliwa.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Kriketi Tanzania Bw. Taher Kitisa ameahidi kushirikiana na wanachama wenzake katika kuhakikisha wanapitia katiba ya chama hicho na kuifanyia maboresho.
Dkt. Mwakyembe alikutana na wanachama wa Kriketi  zaidi ya 60 lengo ikiwa  ni kujadiliana mambo mbalimbali yanayohusu mchezo huo ikiwemo uboreshwaji wa uongozi wa chama hicho kwa manufaa  ya ustawi wa mchezo huo.
 Waziri wa Habari , Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Kulia) akifafanua jambo wakati wa mkutano na wadau wa mchezo wa Kriketi  alipokutana nao hapo jana katikati ukumbi wa mkutano uliopo Uwanja wa Taifa, kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw. Yusuph Singo.
 Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw. Yusuph Singo (kushoto) akieleza jambo kwa wadau wa chama cha kriketi Tanzania walipokutana nao jana uwanja wa Taifa wa Michezo, katikati ni  Waziri wa Habari ,Utamaduni ,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe  na kulia ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Bw. Makoye Nkenyenge. 
 Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Bw. Makoye Nkenyenge (kulia) akizungumza na  wadau wa chama cha kriketi Tanzania walipokutana nao jana uwanja wa Taifa wa Michezo, katikati ni  Waziri wa Habari ,Utamaduni ,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe  na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw. Yusuph Singo (kushoto). 
  Mwenyekiti wa Chama cha Kriketi Tanzania Bw. Taher Kitisa akizungumza wakati wa kikao kilichowahusisha wadau wa chama cha Kikreti pamoja na Waziri wa Habari ,Utamaduni ,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (hayupo katika picha), kilichofanyika jana Jijini Dar es Salaam.
 Mchezaji wa Kriketi ambaye pia ni Kocha wa mchezo huo Bw. Hussein Mohamedi akichangia jambo katika kikao kilichowahusisha wadau hao pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (Hayupo katika Picha),katika kikao  kilichofanyika jana uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Wadau na wanachama wa chama cha Kriketi Tanzania wakifuatilia kwa makini majadiliano yaliyokuwa yakiendelea baina yao na Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (Hayupo katika Picha), katika kikao kilichofanyika jana uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
 (Picha na Lorietha Laurence-WHUSM,Dar es Salaam).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad