HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 17 October 2018

ALIYEKUWA MKURUGENZI TPA NA WENZAKE WAPELEKWA KIZIMBANI KWA MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),  Ephraim Mgawe na wenzake watatu wamefikiwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 984.8.

Mbali na Mgawe washtakiwa wengine ni, Wajumbe wa Bodi ya Manunuzi ya TPA, Happiness Senkoro, Apolonia Mosha na Theophil Kimaro.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita akisaidiana na Wakili wa Takukuru Maghela Ndimbo, amedai, Septemba 28,2010 katika ofisi za TPA zilizopo Ilala jijini Dar es Salaam, washtakiwa walitenda kosa

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Wilbard Mashauri. Imedaiwa, siku hiyo mshtakiwa Mgawe akiwa mtumishi wa umma kama Mkurugenzi Mkuu na ofisa masulufu,  alitumia madaraka yake vibaya kwa kushuhudia mikataba kati ya TPA na Kampuni Leighton Offshore Pte Ltd 19800397 na kupata faida ya Sh. 984,828,000 baada ya kuvunja sheria ya manunuzi kwa kuiwezesha kampuni hiyo kupata upendeleo.

Aidha mshtakiwa senkoro, Mosha na Kimaro wanadaiwa Julai 13,2010 katika ofisi ya TPA, wakiwa watumishi wa umma na wajumbe wa bodi ya manunuzi, walitumia vibaya madaraka kwa kuidhinisha zabuni na kuvunja sheria ya manunuzi ya umma kwa kuiwezesha Kampuni ya Leighton Offshore Pte Ltd kupata faida ya Sh. 984,828,000.

 Katika shtaka la tatu imedaiwa Siku na mahali hapo, washtakiwa wote waliisababishia TPA kupata hasara ya Sh. 984,828,000.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wamekana kutenda makosa hayo na kesi imeahiriashwa hadi Oktoba 30 itakapokuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu amewataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminiwa wenye barua na nakala za vitambulisho vya uraia watakaweka bondi ya sh.. Milioni 15.

Pia wametakiwa kuwasilisha fedha taslimu Sh. milioni 100  au kuweka hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo ya fedha.

Ni mshtakiwa wa pili na wa tatu ndio waliofanikiwa kutimiza masharti ya dhamana huku mshtakiwa wa kwanza na wa nne wakipelekwa mahabusu
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA),  Ephraim Mgawe na wenzake watatu wakiingia katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo wakikabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 984.8.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad