HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 26, 2018

ALIYEKUWA MKURUGENZI PRIDE ASAKWA NA TAKUKURU, UKWEPAJI KODI SOKO LA KARIAKOO WABAINIKA

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) imetoa ripoti ya matukio  ambayo ni mkakati wa kitaifa dhidi ya rushwa na mpango wa utekelezaji wa awamu ya tatu  unaoratibiwa na kitengo cha uratibu wa utawala bora ofisi ya Rais Ikulu katika kupiga vita vitendo vya rushwa.

Akizungumza na waandishi wa habari Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Brigedia Jenerali John Mbungo amesema kuwa aliyekuwa mkurugenzi  mtendaji wa taasisi ya PRIDE  inayojihusisha na utoaji wa mikopo kwa wananchi hasa akina mama ili kuwainua kiuchumi Rashid Gergar Malima (60) anatafutwa kwa tuhuma za kughushi nyaraka na ubadhilifu wa fedha za umma.

Amesema kuwa taasisi hiyo iliundwa kwa lengo la kusaidia wananchi wenye kipato kidogo na ilipata mtaji wake wa kwanza wenye thamani ya dola za kimarekani 4,000  kutoka Norway  kupitia NORAD.

Mbungo ameeleza kuwa katika vipindi mbalimbali kati ya mwaka 2015/2017 Malima na wenzake walifanya ubadhilifu wa fedha za kampuni ya PRIDE za kiasi cha shilingi Bilioni moja na milioni nane  na kuandaa malipo hewa kwa watoa huduma mbalimbali yakiwemo Arusha Art, Antelop Safaries, Essence international na paperwork na pia waliandaa malipo ya salary advance ambayo hayakufuata taratibu na baadaye fedha hizo zote walizichukua na kuzitumia kwa matumizi yao binafsi.

Aidha amesema kuwa mtuhumiwa huyo anadaiwa kutoroka nchini punde tu uchunguzi wa tuhuma hizo ulipoanzishwa mwaka 2018 na taarifa zilizopo ni kwamba alitoroka kupitia eneo la Namanga, na inasemekana kuwa yupo nchini Marekani hivyo amewaomba watanzania nchini na wale wanaoishi Marekani kutoa taarifa za mtuhumiwa huyo ili sheria ifuate mkondo wake.

Watuhumiwa  wengine katika uchunguzi huo wapo na walishahojiwa  na ametoa rai kwa mashirika mengine kuhakikisha kuwa fedha zinazotolewa kwa lengo la maendeleo ya watanzania zinatumika kwa kadri ilivyokusudiwa.

Katika tukio jingine aliyekuwa Afisa Mikopo wa chuo kikuu cha Dar es salaam Ndaki ya Elimu (DUCE) Josephat Museti Machiwa (35) anatafutwa kwa tuhuma za kughushi nyaraka,  wizi na ubadhilifu wa fedha za umma kinyume na sheria.

Imeelezwa kuwa mnamo tarehe 12 Februari 2015 Josephat Machiwa akishirikiana na Mhasibu Lameck Makoye wakiwa watumishi wa Chuo kikuu kishiriki cha Elimu cha Chuo kikuu cha Dar es salaam (DUCE) waliandaa hundi  ya malipo yenye thamani kubwa ya fedha  ambazo zilitokana na fedha za mikopo ya wanafunzi kutoka bodi ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu (HESLB) na kuzilipa fedha hizo kwenye akaunti za watu wasiokuwa walengwa na baada ya kufanikisha hilo watuhumiwa hao walizichukua fedha hizo kutoka kwa watu hao kwa njia mbalimbali za udanganyifu.

Aidha katika tukio jingine mamlaka hiyo imefanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa zoezi la ukusanyaji kodi kupitia mfumo wa kieletroniki (matumizi ya EFD  mashine) katika soko la kariakoo na kubaini ukwepaji kodi  unaofanywa na baadhi wa wafanyabiashara   jambo linalopelekea kukosesha mapato kwa serikali.

Akifafanua tuhuma hiyo Mbungo amesema kuwa wafanyabiashara hao hukwepa kodi kwa kuuza bidhaa bila kutoa risiti na kutoa risiti yenye malipo pungufu ikilinganishwa na thamani halisi. Na hadi sasa wafanyabiashara wengi wakubwa na wadogo wamekamatwa kwa tuhuma hizo.

Mbungo amewataka wafanyabiashara hao kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Naibu Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kutafutwa kwa watuhumiwa waliokimbia baada ya kutenda makosa ya rushwa, wizi na ubadhilifu wa fedha za umma.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad