HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 28 September 2018

VIGOGO SITA WA KAMPUNI YA CHAI YA MPONDE WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KOSA LA UHUJUMU UCHUMI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Tanga jana imewafikisha mahakamani vigogo sita wa Kampuni ya Chai ya Mponde Tea Estate Limited kwa kosa la uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya dola za kimarekani 15,050,254.00 sawa na shilingi za kitanzania Bilioni 30.

Kosa hilo linadaiwa lilitendeka kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2000 na 2013 ambapo watuhumiwa hao baada ya kukosa dhamana wamepelekwa kwenye Gerezani wakisubiri kesi yao itakapotajwa tena.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Takururu mkoani Tanga Christopher Mariba alisema kosa hilo ni kunyume na aya ya kumi ya Jedwali la kwanza la kifungu cha 57(1) na kifungu cha 60(2) cha sheria ya uhujumu uchumi sura ya 200 pitio la mwaka 2002,iliyofanyiwa marekebisho kwa sheria namba 3 ya mwaka 2016.

Aliwataja waliofikishwa mahakamani kuwa ni Nawab Abdulrahim Mulla, Shahdad Nawab Mulla,William Shelukindo,Richard Abraham Mbughuni, Richard Madadi Semroki na Rajabu Ali Msagati ambao ni wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya Mponde Tea Estate Company na kusomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa mkoa wa Tanga Desdery Kamugisha.

Alisema baada ya kusomewa mashitaka hayo washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo huku pia mahakama hiyo ikizuia kusikiliza maombi ya dhamana ya washtakiwa kwa sababu zilezile kwamba haina mamlaka ya kisheria yakusikiliza shauri hilo.

Akitolea ufafanuzi wa mashtaka hayo Mkuu huyo wa Takukuru mkoani Tanga alisema vigogo hao ni wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni ya MPONDE TEA ESTATE LIMITED ambayo awali ilikuwa inajulikana kama MPONDE TEA FACTORY kampuni ambayo kabla ya ubinafsishaji ilikuwa ni mali ya serikali.

“Uchunguzi wa Takukuru umebaini kwamba vigogo hawa kwa nyakati tofauti walifanya udanganyifu kwa kuagiza mizigo na malighafi mbalimbali kwa niaba ya wakulima wadogo wadogo wa chai waliopo wilayani Lushoto mkoani Tanga wakati si kweli… Vigogo hao wamekuwa wakifanya vitendo hivi na kisha kufanikiwa kuingiza vifaa vya thamani ya zaidi ya sh.bilioni 135.

Alisema kwa udanganyifu huo,vigogo hao waliomba na kupata msamaha wa kodi kutoka mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) wa zaidi ya sh. Bilioni 35 wakati wakijua kwamba mizigo na malighafi hizo hazikuwa ni kwa ajili ya walengwa ambao ni wakulima wadogo wadogo wa chai.

Alieleza kwamba kwa mantiki hiyo vigogo hao wameisababishia serikali hasara ya sh.Bilioni 30 ambazo zingelipwa na kuingia katika mfuko wa serikali.

“Lakini kwa hesabu za haraka haraka sh.bilioni 30 zingeweza kujenga kilometa 30 za barabara ya lami,Zahanati 60,Madarasa 1500,Visima vya maji 1000 au viwanda vidogo vidogo 60 kwa wakazi wa mkoa wa Tanga “Alisema.

Hata hivyo alisema Takukuru mkoani Tanga inatoa wito kwa watanzania wote hususani wakazi wa Jiji la Tanga kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo katika kufichua walarushwa wenye lengo la kuzorotesha maendeleo ya watanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad