HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, September 15, 2018

TUMEJIDHATITI KUPUNGUZA FOLENI ENEO LA TAZARA- MHANDISI MFUGALE

Na Paschal Dotto-MAELEZO
Serikali Kupitia Wakala wa Barabara TANROADS  leo imesimamia zoezi la kuanza majaribio ya kutumia  Barabara za juu flyover zilizoko katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere,  ambazo ujenzi wake umemalizika hivi karibuni.

Zoezi  hilo ambalo lilianza saa 3:00 asubuhi limepokelewa vyema na waendesha magari na wananchi kwa ujumla na majira ya saa sita mchana eneo la TAZARA limeonekana tupu huku watazamaji wakishangaa na nyuso zao kuonekana za furaha kwa kazi nzuri ya Serikali yao.

Kuanza kutumika kwa barabara za juu eneo hilo la TAZARA kunafuta mlundikano wa magari ya mizigo toka bandarini kwenda mikoani na abiria wa ndege waingiao na kutoka Uwanja wa kimataifa Dar es Salaam  kutumia muda mwingi kwenye barabara za Nyerere na Mandela hadi saa moja au zaidi badala ya dakika 20 za sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TANROAD Mhandisi Patrick Mfugale, ameeleza kuwa barabara hizo ziko tayari kwa matumizi kwa waendeshaji wa magari jijini Dar es Salaam, na kuwahakikishia kuondokana na foleni eneo hilo la TAZARA.

“tumeamua kupunguza foleni kutoka mjini kwenda  uwanja wa ndege wa Julius Nyerere na kutoka Ubungo kwenda bandarini ambapo kwa sasa kunafikika kwa dakika chache tofauti na hapo zamani watu walikuwa wanatumia zaidi muda wa saa moja lakini sasa hivi ni dakika 20 tu”, Mhandisi Mfugale.

Mhandisi Mfugale alifafanua kuwa wakazi wa Dar es Salaam sasa wataondokana na tatizo la foleni kama hapo mwazo ampako kulikuwa na msongamano wa magari na watu lakini kwa sasa barabara hizo za juu flyover zitasaidia kupunguza  tatizo hilo.

Aidha, Mfugale alieleza kuwa matumizi ya barabara hizo yanakuja baada ya ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliyoifanya Agosti mwishoni kuona maendeleo ya mradi huo mkubwa, aliagiza kufanyika kwa ufunguzi wa majaribio katika barabara hizo.

“Waziri Mkuu, alikuja kukagua  na akaahidi wananchi majaribio kuanza leo,  na magari kupita juu ya barabara hizi, na hii maana yake ni kuona kama barabara tulizozijenga ni imara pia kuona kama foleni inapungua kama tulivyotaka, na sasa tunaona magari yanapita juu”, alisema Mhandisi Mfugale.

Katika kuainisha uwezo wa barabara hizo Mhandisi Mfugale alisema kuwa barabara hizo zitadumu kwa miaka 100 na zina uwezo wa kubeba tani 180 kwa wakati mmoja .

Kwa upande wao wananchi wa Jiji la Dar es Salaam wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi hizo kubwa, akizungumza katika mahojiano maalum, Faridi Maganga alisema “Tunampongeza sana Rais Magufuli kwa kusimamia ulipaji kodi, kwani ndizo zilizowezesha ujenzi wa flyover hii, kama mnavyoona watu wanajiachia tu, hii inaonesha kuwa wananchi wanalipa kodi, na kupata vitu vinavyoonekana kama hivi.”
Magari yakipita kwa ajili ya majaribio leo (Jumamosi septemba 15, 2018 barabra za juu flyover ya Mhandisi Patrick Mfugale lililopo eneo la TAZARA Jijini Dar es Salaam ambalo hivi karibuni linatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli. Picha na Paschal Dotto –MAELEZO

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad