HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, September 6, 2018

TFS IMESABABISHA MACHO YA WASHIRIKI SHINDANO LA MISS TANZANIA 2018 KUYAONA AMBAYO HAWAJAWAHI KUYAONA .

 Washiriki wa Shindano la Miss Tanzania mwaka 2018 wakishangilia baada ya kufika katika Mapango ya Amboni mkoani Tanga.
 Baadhi ya washiriki wa shindano la Miss Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja mkoani Tanga.
 Warembo wa Shindano la Miss Tanzania wakiwa katika kibao cha Mapango ya Amboni mkoani Tanga baada ya kufika hapo kwa ajili ya kushuhudia vivutio vya utalii vilivyopo.

 Baadhi ya washiriki wa Miss Tanzania 2018 wakiwa wamenyoosha mikono juu baada ya kufika katika Shamba la Chai lililopo katika hifadhi ya msitu wa asili wa Amani mkoani Tanga 
Washiriki wa Miss Tanzania 2018 wakiwa katika hifadhi ya msitu wa asili wa Amani mkoani Tanga baada ya kutembelea majiko banifu yanayotumiwa na wananchi wa vijiji vinavyozunguka msitu huo uliopo mkoani Tanga.
Baadhi ya washiriki wa shindano la Miss Tanzania 2018 wakiwa katika moja ya  mlango wa pango la Amboni mkoani Tanga.

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

MOJA ya kauli ambayo nimeisikia zaidi ya mara moja ikitamkwa na washiriki wa Shindano la Miss Tanzania mwaka 2018 ni ile inayoonesha kutoa shukrani zao za dhati kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS),

Warembo hao walioumbwa na Molla wao wakaumbika hawakuwa na shaka hata kidogo kupaza sauti zao tena kwa madaha na madoido wakisema Tanzania yetu, Misitu yetu, Fahari yetu, Urembo oyeee na kisha wanamalizia kwa kusema hivi TFS oyeeeeee..Nikwambie mapema nilikuwa nawasikia kwa masikio yangu.Ndio maana nakwambia nimewasikia.Niamini.

Unajua kwanini?Iko hivi TFS ambayo ipo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kwamba iliamua kuwapeleka warembo hao kwenye Hifadhi ya Mazingira ya Msitu Asili wa Amani iliyopo mkoani Tanga.

Hifadhi hiyo inapatikana katika Wilaya ya Muheza na ipo umbali wa kilometa 35 kutoka Muheza Mjini.Hivyo ni hifadhi ambayo haiko mbali saaana, lakini kwa vivutio vilivyopo kwenye hifadhi hiyo hata ingekuwa mbali kiasi gani ningekushauri ufike ujioonee mwenyewe. Na hivi TFS wanavyojua kutunza hifadhi zetu hadi raha.Nenda Mtanzania mwenzangu ukaone vilivyomo.

Kwa kukumbusha tu ukubwa wa hifadhi hiyo ni hekta 8380 .Ni eneo kubwa na ukweli ni kwamba TFS wameonesha kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha hifadhi hiyo inatunzwa kama ambavyo wamekuwa wakizitunza hifadhi nyingi za misitu ambayo wamepewa jukumu la kuhakikisha inakuwa salama na haiharibiwi.

Safari ya warembo hao kwenda katika hifadhi hiyo ilianza katika Hoteli ya Serene jijini Dar es Salaam.Kama kumbukumbu zangu ziko sawa safari ilianzaa saa 10 alfajiri.Kwa picha ya haraka haraka ni kwamba warembo hao walianza maandalizi ya safari hiyo usiku wa manane.Haikuwa tatizo kwao kuhusu muda wa kuondoka.Shauku yao ilikuwa ni kwenda msitu wa Amani.

Wakiwa kwenye basi kubwa lenye hadhi ya kubeba warembo ambapo miongoni mwao ndimo atapatikana Miss Tanzania mwaka 2018 ifikapo Septemba 8 mwaka huu safari ilianza kwa mwendo ambao hata trafiki akiiona hana sababu ya kupiga tochi kuangalia spidi.Ilikuwa ni ya kawaida sana na lengo ni kutoa nafasi ya warembo hao kuona na vingine watakavyokutana navyo barabarani.

Naomba nieleze kidogo kabla ya kuendelea zaidi. Sababu ya kuandaliwa kwa safari hiyo ni kwamba mkakati wa TFS ni kuhakikisha warembo hao mbali ya kwenda katika hifadhi hiyo na kisha kutumia jukwaa la Miss Tanzania kama sehemu ya kuzitangaza hifadhi zetu nchini.

Naishukuru TFS kwa kutambua nafasi ya warembo hao katika kuutangaza hifadhi zilizopo nchini pamoja na utalii uliopo kwenye hifadhi hizo na ule ambao upo nje ya hifadhi.

Pia naishukuru TFS kwasababu iliona haja ya kuwa na waandishi ambao nao walikuwa miongoni mwa walioambatana na mamisi hao kushuhudia hifadhi hiyo.TFS inaamini waandishi kwa kutumia kalamu zao wataandika maandishi ambayo yatafikisha ujumbe mmoja tu wenye lengo la kuhamasisha watalii wa ndani na nje ya nchi yetu kutembelea vivutio vilivyopo.

Ahsante Mtendaji Mkuu wa TFS Profesa Dos Santos Silayo kwa kufanikisha safari hiyo. Ahsanteni kitengo cha mawasiliano cha TFS kinachosimamiwa na Madame Glory na msaidizi wake Tulizo Kilaga.Ni maofisa makini na wanajua wajibu wao katika eneo la mawasiliano kwa umma.Unauliza kwanini nashukuru sana? Nimefundishwa kushukuru kwa kila jambo jema.

Baada ya kutoa shukrani hizo ngoja niendelee kuelezea.Safari ikawa inaendelea na basi lilipofika Mto Wami tukasimama kidogo na warembo kushuka na kisha kwenda katika eneo la mto huo.

Wakapiga picha kama kawaida yao na baada ya hapo safari ikaendelea mdogo mdogo. Kwa kuwa dhamira ni kuangalia utalii kabla kuingia Hifadhi ya Msitu wa Amani warembo hao wakapata nafasi ya kwenda hoteli ya Tanga Beach.Wakapumzika kwa muda na kisha kwenda kwanza Mapango ya Amboni.

Naomba niseme jambo unapozungumzia mapango ya Amboni maana yake unazungumzia mapango ambayo yamejaa historia ya aina yake na kuvutia kwa kweli.Usijidanganye kwa kusema Tanga hakuna utalii.Utachekwa.

Kuna maeneo mengi ya utalii mkoani Tanga.Ukitaka kujua waulize warembo hao.Wameona kila aina ya vivutio. Hivyo wakiwa katika mapango ya Amboni wakapata nafasi ya kuelezwa mambo mengi na hasa vivutio vya utalii.Hakika eneo hilo limejaa historia kubwa na yenye mvuto ambayo kimsingi inakwenda sambamba na michoro inayoonekana kwa macho.

Mchoro wa Simba ambao upo kwenye mlango wa mapango hayo uliwafanya warembo hao kuonesha mshango.Ujue ukingalia mchoro ule ambao upo kwenye moja ya wa pango unaona kabisa kichwa cha Simba kinatazama ndani. 

Inaelezwa hivi miaka ya zamani.Tena zamani sana eneo hilo lilikuwa ni la bahari na baadae maji yaliposogea  kwenye kina kirefu cha bahari ndipo yakaacha mapango hayo ambayo ndio imejaa michoro.

Ukiwa hapo utaelezwa pia pango la linaloitwa Osare Otanga na pango la Paul Hamisi na kisha utaoneshwa pango dogo kabisa lililopo hapo linajulikana kama pango la jinsia.Ndani ya mapango hayo kwa mujibu wa watoa maelezo wanasema ukiingia ndani kuna njia.

Ukipita njia ya kulia unaenda kutokea Mombasa nchini Kenya na ukipita kushoto unaenda kutokea Stendi ya Mabasi ya Kange huko huko mkoani Tanga. Hata hivyo kwa sasa njia hizo zimezibwa.

Pia kuna michoro ambayo ukiangali inaonesha jengo la Msikiti na Kanisa.Ndani ya mapango hayo kuna michoro ya inayoomunesha Mama Bikira Maria. Pia kuna maandishi ya Koraani.

Wakati maelezo hayo yanatolewa warembo hao walikuwa makini kuhakikisha wanailewa vema. Kilichoawaacha midomo wazi warembo hao ni maelezo kwamba ndani ya mapango kuna eneo la mzimu ambapo watu mbalimbali wanakwenda kufanya maombi na hasa wanaoamini katika kuomba mzimu. Eti ukiwa na shida yako au jambo unalitaka basi ukiomba unafanikiwa.

Kwa kuwa lengo la ziara hiyo ni kujifunza zaidi, hivyo walipata nafasi ya kuuliza maswali kwa waliokuwa wanatoa maelezo kuhusu mapango hayo.Wakajibiwa vizuri.Baada ya kujionea utalii wa ndani katika mapango ya Amboni warembo wakaanza kupiga picha.Nadhan lengo lao lilikuwa ni kuweka kumbukumbu muhimu baada ya kufika hapo.

Hata hivyo kwa kuwa ratiba ilikuwa ni kwenda Hifadhi ya Amani warembo hao wakaanza safari ya kwenda katika hifadhi hiyo.Waliingia hifadhini saa 3:30 usiku.Walipofika moja kwa moja wakaenda kuangalia vinyonga wenye pembe tatu.

Tena unaambiwa kuna aina saba ya vinyonga ndani ya hifadhi hiyo.Ikifika usiku wanaonekana vizuri kuliko mchana.Mbona maajabu mwenzangu! Nashukuru binafsi nimewaona vinyonga na ikitokea nafasi nitakwenda kwa mara nyingine.Wala haichoshi kuwaangalia.

Unajua bwana vinyonga hao tunaelezwa kuwa wanapatikana tu kwenye hifadhi hiyo na si mahali kwingine kokote duniani.Watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani wanafunga safari ili kufika hifadhi ya Amani kuona vinyonga.Wewe unasubiri nini?Nenda ukaone.

Utalii ambao warembo hao wameushuhudia ujumbe wao kwa Watanzania  ni kwamba wawe na utamaduni wa kutembelea hifadhi ya Amani yenye utalii wa kila aina.Mbali ya kushuhudia vinyonga hao siku iliyofuata ilipofika saa 12 asubuhi walipata nafasi ya kwenda eneo ambalo ni maalum kwa ajili ya kuangalia jua linavyochomoza.

Ukiwa katika eneo hilo utapata nafasi ya kuona vizuri namna jua linavyochomoza(Sun Rise).Kwa kuwa TFS ilishajipnga kuhakikisha warembo hao wanaona vivutio vya utalii ndani ya hifadhi hiyo iliamua kuwapeleka eneo ambalo lipo juu ya hifadhi na ni maalumu kwa ajili ya kilimo cha Chai.

Safari ya kufika kwenye mashamba hayo nayo ilikuwa ni utalii tosha kabisa.Warembo walipanda kwenye magari ya wazi(Pick Up).Pia kama unavyojua unapanda mlima katika barabara ambayo haina lami zaidi ya udongo wenye tope jingii. Nitoe rai kwa Mtanzania mwenzangu nenda kashuhudie utalii uliopo Amani.

Binafsi nikiri TFS wanajitahidi kutunza misitu ya asili na kubwa zaidi wanatambua umuhimu wa misitu katika maisha binadamu.Ukiwamo wewe na mimi.Hivyo wanaitunza kwa kiwango cha hali ya juu.

Pia ukiwa Amani utapelekwa na eneo ambalo kuna ndege ambao wanapatikana tu ndani ya hifadhi hiyo.Warembo wamepata nafasi ya kuona

Akizungumza na warembo Mhifadhi wa Msitu wa Mazingira Asili wa Aman Mwanaid Kijazi amefafanua kwa kina kuhusu utalii unaopatikana ndani ya hifadhi hiyo ambayo inatunzwa na TFS. 

Akatumia nafasi hiyo kuwaomba warembo hao kuwa mabalozi wa kuutungaza hifadhi hiyo na nyingine zilizopo nchini pamoja na utalii wa kila aina tulio nao nchini kwetu. Pamoja na mambo mengine warembo hao walipata nafasi ya kulala katika eneo hilo la hifadhi .

Kuna nyumba ambazo zilijengwa na Wajerumani miaka ya zamani na ndizo ambazo zinatumika kwa kulala wageni wanaokwenda kulala eneo hilo.Ni nyumba zilizojengwa miaka ya zamani kidogo.

Iinaelezwa baada ya Wajeruman kuingia wilayani Muheza waliamua kwenda Muheza na kutaka kujenga nyuma karibu na makazi ya watu.

Hata hivyo inaelezwa wenyeji walikubaliwa kwa shingo upande.Walipojenga nyumba na kufikia hatua ya kuezeka nyumba upepo mkali ukauzua paa na katika mazingira ya ajabu ajabu.Wajerumani wakaona si sehemu salama kwa kuishi.Ndipo walipoamua kwenda kujenga ndani ya msitu huo na baada ya kuanza kuishi wakaamini eneo hilo ni la Amani.

Hivyo sababu ya kwanini msitu unaitwa Amani ni kwamba imetokana na Wajerumani hao. Inaelezwa ukiondoa msitu huo kujulikana kwa jina la Amani, hakuna kata wala taaarifa inayoitwa hivyo ndani ya eneo hilo.

Kwa upande wa TFS unawahimiza warembo hayo kuchukua jukumu la kuutangaza hifadhi zilizopo nchini pamoja vivutio vya utalii. Meneja Masoko wa TFS Mariam Kobero anasema kazi iliyopo ni kuendelea kuzitangaza hifadhi hizo pamoja na utalii na ndilo jukumu ambalo wamekuwa wakilifanya kila siku.

Inatosha kwa leo.Niliyoyashuhudia mimi ndani ya hifadhi ni mengi.Nikuahidi nitandelea kukuelezea.Kubwa tuombe uzima.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad