Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
MOJA ya kauli ambayo nimeisikia zaidi ya mara moja ikitamkwa na washiriki wa
Shindano la Miss Tanzania mwaka 2018 ni ile inayoonesha kutoa shukrani zao za
dhati kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS).
Warembo hao waliombwa na Molla wao wakaumbika hawakuwa na shaka hata kidogo
kupaza sauti zao kwa madaha na madoido wakisema Tanzania yetu, Misitu yetu,
Fahari yetu, Utembo oyeee na kisha wanamalizia kwa kusema TFS oyeee...
Unajua kwanini?Iko hivi TFS ambayo ipo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliamua
kuwapeleka warembo hao kwenye Hifadhi ya Mazingira ya Msitu Asili wa Amani
iliyopo mkoani Tanga.
Hifadhi hiyo ipo katika Wilaya ya Muheza .Ipo umbali wa kilometa 35 kutoka Muheza
Mjini.Hivyo ni hifadhi ambayo haiko mbali saaana lakini kwa vivutio vilivyopo kwenye
hifadhi hiyo hata ingekuwa mbali kiasi gani ningekushauri ufike ujioonee mwenyewe.
Nzuri na hivi TFS wanavyojua kutunza hifadhi zetu hadi raha.Nenda Mtanzania
mwenzangu ukaone vilivyomo.
Kwa kukumbusha tu ukubwa wa hifadhi hiyo ni hekta 8380 .Ni eneo kubwa na ukweli
ni kwamba TFS wameonesha kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha hifadhi hiyo inatunzwa
kama ambavyo wamekuwa wakifanya kwenye hifadhi nyingi za misiti ambayo
wamepewa jukumu la kuhakikisha iko salama.
Safari ya warembo hao kwenda katika hifadhi hiyo ilianza katika Hoteli ya Serene
jijini Dar es Salaam.Kama kumbukumbu zangu ziko sawa safari ilianzaa saa 10
alfajiri.Kwa picha ya haraka haraka ni kwamba warembo hao walianza maandalizi ya
safari hiyo usiku wa manane.Haikuwa tatizo kwao kuhusu muda wa kuondoka.
Wakiwa kwenye basi kubwa lenye hadhi ya kubeba warembo ambapo miongoni mwao
ndimo atapatikana Miss Tanzania mwaka 2018 ifikapo Septemba 8 mwaka huu safari
ilianza kwa mwendo ambao hata askari wa Usalama Barabarani akiuona anasema kweli dereva anafuata sheria za ulama barabarani.Hakuna sababu ya trafiki kumulika tochi.
Naomba nieleze kidogo kabla ya kuendelea zaidi. Sababu ya kuandaliwa kwa safari hiyo ni kwamba mkakati wa TFS ni
kuhakikisha warembo mbali ya kwenda katika hifadhi hiyo pia wanapata nafasi ya kushuhudia vivutio vya utalii ambavyo watakutana navyo wakati wanaelekea huko.
Naishukuru TFS kwa kutambua nafasi ya warembo hao katika kuutangaza hifadhi zilizopo nchini pamoja na utalii uliopo kwwnye hifadhi hizo na ule ambao upo nje ya hifadhi.Pia naishukuru TFS kwasababu iliona haja ya kuwa na waandishi
ambao nao watashuhudia hifadhi hiyo na utalii uliopo na kisha kwa kutumia kalamu
zao ili kuandika maandishi ambayo yatafikisha ujumbe mmoja tu wenye lengo
la kuhamasisha watalii wa ndani na nje ya nchi yetu kutembelea vivutio vilivyopo.
Ahsante Mtendaji Mkuu wa TFS Profesa Dos Santos Silayo. Baada ya kutoa shukrani zangu kwa Profesa Silayo basi acha niendelee kuelezea.Safari ikawa inaendelea na basi lilipofika Mto Wami tukasimama
kidogo na warembo kushuka na kisha kwenda katika eneo la mto huo.
Wakapiga picha kama kawaida na kisha safari ikaendelea mdogo mdogo. Kwa kuwa dhamira ni kuangalia utalii kabla kuingia Hifadhi ya Msitu wa Amani warembo hao wakapata nafasi ya kwenda hoteli ya Tanga Beach.Wakapumzika kwa muda na kisha kuelekea mapango ya Amboni.
Naomba niseme jambo unapozungumzia mapango ya Amboni maana yake
unazungumzia mapango ambayo yamejaa historia ya aina yake.Usijidanganye kwa
kusema Tanga hakuna utalii, utachekwa.
Kuna maeneo mengi ya utalii.Ukitaka kujua waulize warembo hao.Wameona kila aina ya vivutio. Hivyo warembo hao wakiwa katika mapango ya Amboni wakapata nafasi ya kuelezwa mambo mengi.Hakika utabaini eneo hilo limejaa historia kubwa na yenye mvuto ambayo kimsingi inakwenda sambamba na michoro inayoonekana kwa macho.
Mchoro wa Simba ambao upo kwenye mlango wa mapango hayo uliwafanya warembo hao kuonesha mshango.Ujue ukingalia mchoro ule ambao upo kwenye mapango hayo
unaona kabisa kichwa cha Simba kinatazama ndani.
Inaelezwa hivi miaka ya zamani.Tena zamani sana eneo hilo lilikuwa ni la bahari na baadae maji yaliposogea kwenye kina kirefu cha bahari ikaacha mapango hayo ambayo ndio imejaa michoro.
Yaani unaambiwa kuna mapango moja linaitwa
Osare Otanga na lingine linaitwa Paul Hamisi na pango dogo kabisa lililopo hapo linajulikana kana pango la jinsia.Ndani ya mapango hayo kwa mujibu wa watoa maelezo wanasema ukiingia ndani kuna njia.
Ukipita njia ya kulia unaenda Mombasa nchini Kenya na ukipita kushoto
unaenda kutokea Stendi ya Mabasi ya Kange huko huko mkoani Tanga. Pia kuna michoro ambayo ukiangali inaonesha jengo la Msikiti na Kanisa.Ndani ya mapango hayo kuna michoro ya inayoonesha Biblia na Koraani.
Wakati maelezo hayo yanatolewa warembo hao walikuwa makini
kuhakikisha wanailewa vema. Kilichoawaacha midomo wazi warembo hao ni maelezo
kwamba ndani ya mapango kuna eneo la mzimu ambapo watu mbalimbali
wanakwenda kufanya maombi na hasa wanaoamini katika kuomba mzimu.
Kwa kuwa lengo la ziara hiyo ni kujifunza zaidi, hivyo walipata nafasi ya kuuliza maswali kwa waliokuwa wanatoa maelezo kuhusu mapango hayo..Wakajibiwa vizuri.Baada ya kujionea utalii wa ndani katika mapango ya Amboni hatua iliyoafuata kwa warembo hao wakaanza kupiga picha za kumbukumbu kuwa nao wamewahi kufika hapo.
Hata hivyo kwa kuwa ratiba ilikuwa ni kwenda Hifadhi ya Amani warembo hao
wakaanza safari ya kwenda kwenye hifadhi hiyo.Waliingia hifadhini saa tatu
usiku.Walipofika moja kwa moja wakaenda kuangalia vinyonga wenye pembe tatu.
Tena unaambiwa kuna aina saba ya vinyonga ndani ya hifadhi hiyo.Usiku wanaonekana vizuri kuliko mchana.Mbona maajabu mwenzangu! Nashukuru binafsi nimewaona vinyinga na ikitokea nafasi nitakwenda kwa mara nyingine.Wala haichoshi kuwaangalia.TFS basi twendeni tena.
Unajua bwana vinyonga hao tunaelezwa kuwa wanapatikana tu kwenye hifadhi hiyo na si mahali kwingine kokote duniani.Watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani wanafunga safari kwenda kuangalia vinyonga.
Utalii ambao warembo hao wameushuhudia ujumbe wao kwa Watanzania ni kwamba
wawe na utamaduni wa kutembelea hifadhi ya Amani yenye utalii wa kila aina.Mbali ya
kushuhudia vinyonga hao siku iliyofuata ilipofika saa 12 asubuhi walipata nafasi ya
kwenda eneo ambalo ni maalum kwa kuangalia jua linavyochomoza.
Ukiwa katika eneo hilo utapata nafasi ya kuona vizuri namna jua
linavyochomoza(Sun Rise).Kwa kuwa TFS ilihakikisha imejipanga vema kwa kuwapa nafasi ya warembo hao kushuhudia utalii uliopo ndani ya hifadhi hiyo waliamua kuwapeleka eneo ambalo lipo juu ya hifadhi na ni maalumu kwa ajili ya kilimo cha Chai.
Safari ya kufika kwenye shamba hilo nayo ilikuwa ni utalii tosha kabisa.Warembo walipanda kwenye magari ya wazi.Pia kama
unavyojua unapanda mlima katika barabara ambayo haina lami zaidi ya udongo wenye
tope. Nitoe rai kwa Mtanzania mwenzangu tena muda kisha tembelea katika hifadhi
hiyo.
TFS wanajitahidi kutunza misitu ya asili na kubwa zaidi wanatambua umuhimu wa misitu katika maisha binadamu.Ukiwamo wewe na mimi.Hivyo wanaitunza kwa kiwango cha hali ya juu.
Ukiwa Amani utapelekwa na eneo ambalo kuna ndege ambao
wanapatikana tu ndani ya hifadhi hiyo.
Akizungumza na warembo Mhifadhi wa Msitu wa Mazingira Asili wa Aman Mwanaid
Kijazi amefafanua kwa kina kuhusu utalii unaopatikana ndani ya hifadhi hiyo ambayo
inatunzwa na TFS.
Akatumia nafasi hiyo kuwaomba warembo hao kuwa mabalozi wa kuutungaza hifadhi
hiyo na nyingine zilizopo nchini pamoja na utalii wa kila aina tulio nao nchini kwetu.
Pamoja na mambo mengine warembo hao walipata nafasi ya kulala katika eneo hilo la
hifadhi .
Nyumba zilizopo zilijengwa miaka ya zamani na Wajeruman.Hivyo nyumba zilizopo
ndani ya hifadhi hiyo nazo zinahistoria yake. Kabla ya kujengwa eneo la hifadhi
Wajeruman baada ya kuingia nchini waliamua kwenda Muheza na kutaka kujenga
nyuma karibu na makazi ya watu.
Hata hivyo inaelezwa wenyeji walikubali kwa shingo
upande.Hali hiyo Wajeruman waliona si sehemu salama na kisha kuamua kwenda kujenga ndani ya msitu huo.Hivyo waliona wako eneo lenye Amani na ndio kisa cha msitu huo kujulikana kwa jina hilo.
Kwa upande wa TFS unawahimiza warembo hayo kuchukua
jukumu la kuutangaza hifadhi zilizopo nchini pamoja vivutio vya utalii.Inatosha kwa leo.
No comments:
Post a Comment