HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, September 11, 2018

RAIS MAGUFULI ATOA SALAMU ZA POLE KWA MAJERUHI SITA WA AJALI SIMIYU, WAKIWEMO WAANDISHI WATANO

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akikabidhi salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, kwa Mwandishi wa habari wa AZAM TV, Bi Rehema Evance ambaye alijeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea Septemba 09, 2018 wilayani Meatu, wakati Mhe.Rais akiwa ziarani mkoani humo.
Kutoka Kushoto Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw.Jumanne Sagini, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Dk t. Joseph Chilongani na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera wakimjulia hali, Mwandishi wa habari wa AZAM TV, Bi Rehema Evance ambaye alijeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea Septemba 09, 2018, wakati Mhe.Rais akiwa ziarani mkoani humo.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa pole kwa waandishi wa habari watano wa Mkoa wa Simiyu na Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika,Dkt. Titus Kamani waliopata ajali katika wilayani Meatu, wakati akiwa ziarani wilayani humo, salamu ambazo zimewasilishwa kwa niaba yake  na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka, ambaye aliwatembelea katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu walikokuwa wakipatiwa matibabu.

Akiwasilisha salamu za Mhe.Rais,  jana jioni Mhe. Mtaka amesema magari matano ya Simiyu ya Serikali na gari binafsi yaligongana na watu sita wakajeruhiwa wakiwemo waandishi watano na Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika,Dkt. Titus Kamani  na kusisitiza kuwa Mhe. Rais ameguswa na jambo hilo, hivyo ametoa shilingi laki tano kwa kila majeruhi ili iwasaidie katika matibabu.

“...magari ya waandishi wa habari lakini kulikuwa na gari binafsi, baada ya msafara wa Rais kwa sababu ya vumbi,  dereva mmoja katika yale magari alisimama kutaka kuona njia vizuri, magari yaliyokuwa yakifuatana  matano yakagongana kwa nyuma, watu sita wakapata majeraha miongoni mwao walikuwepo waandishi wetu watano na Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika,Dkt. Titus Kamani”

“Mhe. Rais anatoa salamu zake za pole kwa majeruhi wote,  ameguswa sana na jambo hili hasa pale aliposikia kuwa sehemu ya majeruhi ni waandishi ambao tumekuwa nao pamoja katika ziara hii, wakafanya kazi kubwa ya kuuhabarisha Watanzania,  akaomba mimi kama Mkuu wa Mkoa nifikishe salamu zake za pole kwa niaba  yake kwa watu hawa sita” alisema.

Ameongeza kuwa Mkoa utaendelea kuchukua tahadhari kupitia jeshi la polisi hasa katika misafara ya viongozi na kuhakikisha kuwa wanajenga uelewa wa pamoja kwa madereva wakati wa maandalizi ya safari juu ya namna ya kuchukua tahadhari.

Rehema Evance ambaye ni mwandishi wa Azam TV amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwatambua na kuona awape mkono wa pole ambao amebainisha kuwa fedha hizo zitawasaidia katika kugharamia matibabu.

“ Kwanza namshukuru Mungu kwa kutujalia tukapona,  lakini kipekee napenda kumshukuru Mhe. Rais kwa kuona kuna haja ya kutusaidia katika hili, kwa hiki alichotoa Mungu ambariki sana kitatusaidia kwenye matibabu, tunaahidi kuendelea kuwahabarisha Watanzania na kuhakikisha yale yote yanayotendeka ndani ya nchi yanawafikia” alisema.

Ajali hii iliyotokea wilayani Meatu Septemba 09, 2018 imesababisha majeruhi sita ambao ni waandishi watano Rehema Evance (AZAM TV), Belensi China(ITV), Aidan Mhando(Channel Ten), Phaustine Fabian(Mwananchi), Mpiga Picha Samson Masunga pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika,Dkt. Titus Kamani na hakuna kifo kilichotokea..

Majeruhi wote walipatiwa matibabu katika Hospitaliya Wilaya ya Meatu ambapo waandishi wa habari Rehema Evance (AZAM TV), Phaustine Fabian(Mwananchi), Mwenyekiti wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika,Dkt. Titus Kamani waliruhusiwa na Belensi China(ITV), Aidan Mhando(Channel Ten), na Mpiga Picha Samson Masunga walipewa Rufaa kwenda Bugando kwa uchunguzi na matibabu zaidi.

Kwa mujibu wa majeruhi hao waliopelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando wote wamefanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu na leo Septemba 10, 2018  wameruhusiwa. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad