HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 4 September 2018

PROF.MKUMBO AWATAKA WANASHERIA KUSIMAMIA SHERIA WANAZOZIWEKA

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumza na wanasheria wa Sekta ya Maji (hawamo pichani), Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Simon Nkanyemka (kulia) na Mwenyekiti wa kikao hicho, Bernadetha Mkandya kutoka DAWASA.
 Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Simon Nkanyemka akizungumza, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo (katikati) na Mwenyekiti wa Kikao hicho, Bernadetha Mkandya kutoka DAWASA.
 Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wanasheria wa Sekta ya Maji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo akiwa pamoja na washiriki wote wa mkutano wa wanasheria wa Sekta ya Maji.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo amewataka wanasheria wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji pamoja na taasisi zake kuhakikisha wanasimamia sheria wanazoziweka, ili kuepusha migogoro ambayo inaweza kuisababishia Serikali hasara na kukwamisha maendeleo ya Sekta ya Maji.

Profesa Mkumbo amezungumza hayo katika mkutano uliowakutanisha wanasheria 36 kati ya 41 kutoka taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, pamoja na wanasheria wa wizara hiyo uliofanyika jijini Dodoma; lengo la mkutano huo likiwa ni kuboresha utendaji wa wanasheria katika Sekta ya Maji katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango, jijini Dodoma.

Amesema kama washauri na wasimamizi wa sheria katika Sekta ya Maji waendelee kusimamia vyema sheria, taratibu na miongozo inayotolewa na Serikali na kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na ufanisi; kuzingatia kanuni za maadili na utendaji kazi wa wanasheria. 

Wakihakikisha kuwa wanaifahamu vizuri sekta na vipaumbele vyake na kuvitekeleza; wakitoa ushauri pasipo woga pamoja na kuongeza ujuzi katika utendaji wao wa kazi.

 ‘‘Nichukue fursa hii kuwapongeza kwa kazi nzuri mnayoifanya katika sekta yetu, mmekuwa mkitatua migogoro mingi ya kisheria na kuisaidia Serikali katika mambo mengi ya msingi’’, alisema Profesa Mkumbo.

‘‘Jambo la msingi ni kuhakikisha mnasimamia misingi ya sheria mnazoziweka ili kuisaidia Serikali kuepukana na hasara na migogoro ambayo itakwamisha maendeleo ya Sekta ya Maji, huku mkifanya kazi yenu kwa weledi na uadilifu’’, alisisitiza Profesa Mkumbo.

Awali, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Simon Nkanyemka akizungumza kwenye mkutano huo, amesema lengo lake ni kufahamiana; kujifunza; kubadilishana uzoefu; changamoto wanazokumbana nazo na mbinu za kuzitatua, na kujenga ushirikiano ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao kiutendaji.

Nkanyemka alisema kuna haja ya wanasheria kupata mafunzo ya ziada mbali na taaluma yao ya sheria; ikiwemo mafunzo ya ununuzi na utumishi ili kuwa na weledi zaidi wa kutatua migogoro ya kisheria inayohusisha maeneo hayo katika utendaji wao wa kazi, ambapo mara nyingi wanahusishwa mara baada ya matatizo kutokea.

Aidha, mkutano huo umefanikiwa kukusanya maoni yatakayosaidia kuboresha mapendekezo ya kutungwa kwa Sheria Mpya ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2018, ambayo inalenga kuboresha mfumo wa kitaasisi wa usimamizi wa utoaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira ili kuongeza kasi na ufanisi katika utoaji wa huduma za maji nchini.

Lengo la sheria hiyo itayotekelezeka ni kukidhi mahitaji, ambayo itakuwa ni kichocheo cha kuhakikisha kwamba jamii inapata huduma bora ya maji na endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo na kuimarisha utawala bora wa maji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad