HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 12 September 2018

NIDA YAANZA KUTOA VITAMBULISHO VYA UTAIFA KWA WALEMAVU KINONDONI

Na Leandra Gabriel, Blogu ya jamii
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo amezindua rasmi zoezi la utambuzi na usajili kwa watu wenye ulemavu ili waweze kupata vitambulisho vya utaifa na hii ni kwa kushirikiana na mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA) na ofisi ya ustawi wa jamii Wilayani humo.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ameipongeza mamlaka hiyo na ofisi ustawi wa jamii Kinondoni kwa kuwajali watu wenye mahitaji maalumu na kuandaa jukwaa maalumu la kuwatambua na kuwasajili na kutoa vitambulisho vya utaifa.

Amesema kuwa vitambulisho hivyo vitawasaidia katika kupata huduma mbalimbali ya kijamii na amewataka wanajamii kuwahimiza na kuhakikisha kila mtu mwenye ulemavu wa aina yoyote anapata huduma hiyo ya utambuzi na usajili na kupatiwa kitambulisho chake cha utaifa.

Aidha Chongolo amewahaidi walemavu hao kuwapatia fungu la fedha lililopo katika bajeti ya serikali ili waweze kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Kwa upande wake Afisa msajili (NIDA) Wilaya ya Kinondoni Dickson Mbanga amesema kuwa mchakato wa utoaji wa vitambulisho kwa walemavu umekuwa na changamoto kubwa hivyo kama mamlaka kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya wameweka mazingira rafiki ya kuwasajili watu wenye ulemavu hivyo wajitokeze kwa wingi ili waweze kujipatia vitambulisho vya uraia.

Afisa usajili huyo ameeleza kuwa vitambulisho hivyo vitawasaidia  kupata huduma za kijamii, mikopo, afya, sensa kwa walemavu pamoja na ulinzi na salama.

Pia Mwenyekiti wa watu wenye ulemavu Mkoa wa Dar es salaam Martin Komboza ameishukuru ofisi ya NIDA kwa kuwapa fursa ya kupata vitambulisho na amewataka walemavu kutumia nafasi hiyo kupata vitambulisho bila kupitia changamoto zozote.

Utoaji vitambulisho vya utaifa kwa walemavu Wilaya ya Kinondoni umeanza rasmi leo hadi siku ya ijumaa ya tarehe 14.
 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo akizungumza na walemavu katika viwanja vya shule ya msingi Ndugumbi wakati wa uzinduzi wa zoezi la utambuzi na usajili wa watu wenye ulemavu ili waweze kupata vitambulisho vya utaifa.
 Afisa Msajili (NIDA) Wilaya ya Kinondoni Dickson Mbanga akisoma hotuba kwa Mkuu wa Wilaya wakati wa uzinduzi wa mchakato wa utoaji wa vitambulisho vya utaifa kwa walemavu Wilayani humo.
 Baadhi ya walemavu waliojitokeza katika zoezi hilo la kujipatia vitambulisho vya utaifa, leo katika viwanja vya shule ya Ndugumbi.
Mmoja wa walemavu akiwa katika hatua ya mwisho ya upigaji picha ili aweze kupata kitambulisho cha utaifa katika mchakato wa utoaji wa vitambulisho vya utaifa kwa watu wenye ulemavu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad