Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF) Mkoa wa Tabora umelipa jumla ya bilioni 3.8 kwa watoa huduma mbalimbali mkoani humo katika mwaka wa fedha uliopita.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Jacob Mwailubi wakati wa mkutano wa wadau wa afya wa Mkoa huo.
Alisema vituo vya Serikali vimelipwa bilioni 1.021 , watoa huduma wa binafsi bilioni 1.246 na Vituo vya Taasisi za dini vimelipwa kiasi bilioni 1.566.
Aidha Mwailubi alisema NHIF mkoani humo imefanikiwa kusajili wanachama wapya 3,063 katika mwaka wa fedha uliopita na kuufanya ufikishe wanachama 20,400.
Mwailubi alisema kati yao watumishi wa umma ni 16,938, Mashirika binafsi 307, wastaafu 175, Vyuo vya Elimu ya juu 2,131, Madiwani 268,Viongozi madhehebu ya dini 125, Wanachama binafsi 6 na Watoto chini ya miaka 18 ni 450.
Aidha alisema katika kipindi hicho Ofisi ya Mkoa ya NHIF iliweza kukusanya jumla ya milioni 645.9 kama michango ya wanachama ambapo kati yake milioni 325.3 ni michango toka taasisi za umma wakati milioni 320.6 ilikusanywa kutoka mashirika binafsi.
Hata hivyo alisema Halmashauri za Wilaya ya Tabora –Uyui, Igunga na Urambo hazijalipa malimbikizo ya michango ya Watumishi wanaolipwa kupitia mapato ya ndani ya jumla milioni 39.5.
Mwailubi alisema Halmashauri ya wilaya Tabora inadaiwa shilingi milioni 1.6, Igunga milioni 28.2 na Urambo milioni 8.6.
Aliwahimiza michango hiyo ilipwe ili watumishi husika wapate huduma za matibabu.
Wakati huo huo Mwailubi alisema NHIF imesajili jumla ya Vituo vya Huduma za Afya 302 ambapo kati ya hivyo vituo 243 vinavyomilikiwa na serikali, vituo 24 ni Taasisi na mashirika yasio ya serikali na vituo 35 vinavyomilikiwa na watu binafsi yakiwemo maduka ya dawa.
No comments:
Post a Comment