HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 14, 2018

MIAKA MITATU YA JPM IMEONGEZA ARI YA KUFANYA KAZI-MAJALIWA

*Ameimarisha nidhamu, uadilifu kwenye utumishi wa umma

*Ameboresha miundombinu ya reli, barabara, nishati, elimu na afya

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. John Magufuli katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, amefanikiwa kuimarisha nidhamu, uadilifu na uwajibikaji ndani ya utumishi wa umma pamoja, kukemea uzembe na kujenga ari ya kufanya kazi.

Mafanikio mengine ni ununuzi wa meli katika ziwa Nyasa, Tanganyika na Victoria pamoja na kufufua Shirika la Ndege la Tanzania ili kuimarisha usafiri wa anga na kukuza sekta mtambuka zikiwemo za utalii, afya, kilimo na kujenga reli ya kiwango cha kimataifa (SGR).

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Septemba 14, 2018) wakati akiahirisha mkutano wa 12 wa Bunge, Bungeni jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Novema 6, 2018.

Amesema mafanikio mengine yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Magufuli ni kuendesha vita dhidi ya rushwa na ufisadi kwenye taasisi za umma sambamba na kuanzisha Mahakama ya Mafisadi na kuimarisha ulinzi wa rasilimali za nchi ikiwemo madini na maliasili.

“Kujenga vyanzo vipya vya umeme kama vile mradi wa kuzalisha umeme wa maji megawati 2,100 katika bonde la mto Rufiji (Stiegler’s Gorge), kusambaza umeme hadi vijijini sambamba na kuongeza kasi ya utekelezaji wa  miradi ya awamu ya tatu ya mpango wa REA ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania).”

Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli ameimarisha huduma za afya hususan upatikanaji wa dawa, vifaatiba katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na ujenzi wa vituo vya afya na hospitali za wilaya na utoaji Elimumsingi Bila Malipo kwa watoto wa Kitanzania.

Pia amehakikisha miradi yote ya maji inayotekelezwa inakuwa bora, yenye uwiano na thamani halisi ya fedha pamoja na kukamilishwa kwa wakati na kuimarisha kilimo, ushirika na bei za mazao ya biashara.

Waziri Mkuu amesema juhudi zote hizo zinafanywa kwa lengo la kuiwezesha nchi kufikia malengo ya dira ya Taifa ya kuwa na uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. “Niwaombe Watanzania wenzangu tuendelee kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais katika kuleta maendeleo.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wawekezaji kutumia fursa ya uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji nchini, biashara na upatikanaji wa malighafi kwa kuja kujenga viwanda mbalimbali hususan vya kuchakata mazao ya kilimo.


 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa Kumi na Mbili  wa Bunge jijini Dodoma, Septemba 14, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipongezwa na wabunge baada ya kusoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge jijini Dodoma Septemba 14, 2018. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, Bungeni jijini Dodoma, Septemba 14, 2018. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Hanang, Dkt. Mary Nagu Bungeni jijini Dodoma, Septemba 14, 2018. 
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Septemba 14, 2018. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad