HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 6 September 2018

MAMLAKA HALI YA HEWA YATANGAZA UWEZEKANO WA KUNYESHA MVUA JUU YA WASTANI,WATABIRI MAGONJWA YA MLIPUKO

Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),imeeleza uwepo wa uwezekano mkubwa wa kunyesha mvua nyingi za wastani hadi juu ya wastani katika msimu wa mvua za vuli kipindi cha Oktoba Dsemba mwaka huu.

Pamoja utabiri huo TMA pia imetoa  athari na ushauri wa mvua hizo ikiwemo kuwepo kwa hali ya unyevunyevu wa udongo na upatikanaji wa chakula cha samaki vinatarajia kuimarika katika maeneo mengi ya ukanda wa nyanda za juu Kaskazini Mashariki na Pwani ya Kaskazini.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA ,Dkt Agnes Kijazi ametangaza utabiri huo leo jijini Dar es Salaam wakati anazungumza na waandishi wa habari.

Amefafanua kwamba  mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa  inaonesha kuwepo kwa mkubwa wa mvua za vuli kuwa za wastani katika maeneo mengi ya nchi.

 Ameongeza mvua za vuli kipindi cha Oktoba hadi Desemba ni mahususi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.

“Mvua za Vuli 2018 zinatarajiwa kuanza mapema katikati ya Septemba na mwanzoni mwa Oktoba 2018 katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua.

"Ambapo kwa mikoa ya Kagera ,Geita na wilaya ya kibondo mvua inatarajia kunyesha wastani hadi chini ya wastani,”amesema Dk.Kijazi

Wakati katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki pamoja na maeneo ya mashariki na kusini mwa ziwa Viktoria inatarajia kunyesha mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Ameeleza  mvua zinatarajia kuanza mapema kati ya wiki ya pili na ya tatu ya Septemba mwaka huu katika maeneo ya mkoa wa Mara na kusambaa katika mikoa ya Shinyanga ,Simiyu,Mwanza ,Geita na Kagera ifikapo wiki ya tatu ya Oktoba mwaka huu.

 Pia amesema katika ukanda wa Pwani wa kaskazini katika mikoa ya Dar es Salaam ,Tanga,Pwani ,Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro mvua zinatarajia kuanza mapema wiki ya nne ya Septemba ambapo itanyesha mvua ya wastani hadi juu ya wastani,”alisema Dk. Kijazi

Akielezea zaidi utabiri huo amesema katika maeneo ya Kilimanjaro,Arusha na Manyara mvua inatarajia kunyesha kati ya wiki ya pili ya Oktoba mwaka huu  na inatarajiwa kunyesha wastani hadi juu ya wastani.

Dk.Kijazi amesema mazao yasiyohitaji maji mengi yanaweza kuathiriwa na hali ya unyevunyevyu wa kupitiliza na maji kutuama.

Pia amesema magonjwa ya wanyama na upotevu  wa samaki kutokana na uharibifu wa miundombinu ya kufugia samaki vinaweza kujitokeza kutokana na mvua za juu ya wastani zinazotarajiwa katika maeneo hayo.

Ameongeza upande wa sekta ya afya  kutakuwa na uhaba wa maji salama kwa shughuli za binadamu ikiwemo usafi katika maeneo yanayotarajia kupata mvua za chini ya wastani  huku milipuko ya magonjwa inaweza kujitokeza.

Hivyo amesema menejimenti za maafa zinashauriwa kuandaa mkakati wa kupunguza athari zinazoweza kujitokeza katika msimu wa mvua za vuli .

"Hivyo zinapaswa kuandaa mbinu za kukabiliana na mafuriko pamoja na majanga yatokanayo na mafuriko," amesema.

Pamoja na mambo mengine amewaomba wananchi kuchukua tahadhari iwapo mvua zitanyesha juu ya wastani.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad