HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 24 September 2018

HESLB yajipanga kuchota mbinu kutoka kwa wadau Lilongwe

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru
Na Omega Ngole, Lilongwe,
TAASISI za kiserikali zinazotoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu Afrika zinakutana kwa siku nne kuanzia kesho (Jumatatu, Septemba 24, 2018) mjini Lilongwe, Malawi katika mkutano ambao Bodi ya Mikopo ya Tanzania (HESLB) ikisema imejipanga kuchota mbinu za kuongeza ufanisi.

Mkutano huo wa kimataifa utafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Bingu wa Mutharika na umeandaliwa na Shirikisho la Taasisi hizo linalofahamika kwa kifupi kama AAHEFA. Washiriki zaidi ya 160 kutoka nchi 11 na wadau mbalimbali kama Benki ya Dunia, USAID wanatarajiwa kushiriki.

Washiriki hao ni maafisa wa Serikali, Watendaji Wakuu wa taaasisi hizo zinazotoa mikopo na wageni waalikwa kutoka Tanzania, Kenya, Rwanda, Ghana, Uganda and Zambia. Wengine wanatoka Botswana, Lesotho, Namibia, Afrika Kusini na wenyeji Malawi.

Mkutano huo utafunguliwa kesho (Jumatatu, Sept 24, 2018) na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Malawi Bw. Bright Msaka.

Akiongea mjini hapa kuhusu mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru ingawa HESLB imepata mafanikio makubwa karika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, bado kuna nafasi kubwa ya kujifunza kutoka kwa nchi nyingine hususan za kiafrika ambazo zinakutana na changamoto kama za Tanzania.

“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita tumekusanya zaidi ya TZS 298 bn kati ya TZS 398 bn zilizokusanywa tangu kuanzishwa kwa HESLB mwaka 2005 … na kwa miongozo tunayopata kutoka Serikalini, tumefanikiwa kushughulikia malalamiko ya wanafunzi kwa kiasi kikubwa… ni lengo letu kutenda bora zaidi,” amesema Bw. Badru katika mkutano na wanahabari mjini Lilongwe leo.

Ameongeza: “Pamoja na mafanikio haya, tunaamini kuna mengi ya kujifunza hususan katika kuwasaka wanufaika wa mikopo tunayotoa ambao wapo katika sekta binafsi na isiyo rasmi kwa kuwa bado uzingatiaji wa sheria sio mzuri,” amesema.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Sekretariati ya AAHEFA, zaidi ya mada 10 zitawasilishwa na kujadiliwa katika kipindi cha siku nne na zote zitahusu masuala ya utoaji mikopo kwa Africa.

Baadhi ya mada hizo ni‘Je, Taasisi za Utoaji Mikopo Afrika zinazingatia kozi zinazotoa ajira kwa soko la kesho?” ambayo itawasilishwa na Dkt. Valentino Zimbita, Mkuu wa Elimu ya Juu katika Serikali ya Malawi.

Kwa upande wake, Bi. Liliane Igihozo, Mkuu wa Operesheni katika Benki ya Maendeleo ya Rwanda atawasilisha mada kuhusu ‘Uendeshaji wa Taasisi za Mikopo ya Elimu ya Juu kama Benki’ akizungumzia uzoefu wa Benki ya Maendeleo ya Rwanda. Mjadala wa kikao hiki utaongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Bw. Abdul-Razaq Badru.

Pamoja na mada nyingine, Wahasibu-Wataalam wawili watazungumzia ‘Umuhimu wa Kutengeneza Mfumo wa Utoaji Mikopo ya Elimu ya Juu utakaohakikisha Urejeshaji kutoka Popote Duniani – Matumizi ya mifumo ya kidijitali’. Watalaamu hao ni Charles Oduor, kutoka Kampuni ya E&Y na Charles Ringera ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi nchini Kenya.

Mkutano huo unatarajiwa kufungwa Alhamisi, Sept. 27, 2018 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bw. Justin Saidi.

AAHEFA ilianzishwa miaka nane iliyopita kama chombo kinachounganisha taasisi za serikali barani Afrika zinazotoa mikopo ya elimu kwa lengo la kubadilishana uzoefu ili kuongeza ufanisi na wigo wa utoaji mikopo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad