HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 2, 2018

ZAO LA MCHIKICHI KUMALIZA UHABA WA MAFUTA NCHINI

SEKTA ya kilimo ni mhimili wa uchumi wa Taifa na inategemewa katika kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025, kupitia viwanda kwa sababu kilimo ndicho kitawezesha viwanda kwa kuvipatia malighafi.

Kutokana na umuhimu wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa nchini, serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa kuhakikisha inaiboresha ili iweze kuwa na tija na kufikia malengo iliyojiwekea.

Sekta hiyo mbali na kuwa mhimili wa uchumi wa Taifa, pia imekuwa ikichangia pato la mkulima mmoja mmoja, kaya na pia ni tegemeo la mapato ya fedha za ndani na za kigeni.

Kufuatia hali hiyo, Serikali imeweka msisitizo katika kusimamia mazao makuu matato ya biashara ambayo ni pamba, chai, kahawa, korosho na tumbaku ambayo uzalishaji wake umeonyesha tija.

Baada ya kupata mafanikio katika mazao hayo Serikali kwa sasa inaboresha kilimo cha mazao ya alizeti, ufuta, michikichi ili kuzalisha mafuta ya kula ya kutosha kwa kutumia mazao hayo na mbegu za pamba.

Itakumbukwa kwamba kila mwaka, Serikali inatumia sh. bilioni 600 kwa ajili ya kuagiza mafuta ghafi ya kula kutoka nje ili kukidhi mahitaji kwa kuwa kiwango kinachozalishwa nchini hakitoshi.

Katika kuhakikisha kuwa jambo hilo linafanikiwa Serikali ya awamu tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli imeamua kuanzisha kampeni ya kufufua zao la michikichi ili kuweza kuzalisha mafuta ya kutosha.

Akizindua kampeni hiyo mkoani Kigoma hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kwa kufanya mageuzi makubwa katika zao la michikichi.

Uamuzi huo sasa umelifanya zao hilo kuwa la sita la biashara ambalo katika miaka ya l960 hadi 1970, mkoa wa Kigoma ulijipatia umaarufu kwa uzalishaji wa zao hilo.

Waziri Mkuu anasema kampeni ya kufufua zao la michikichi mkoani Kigoma inaenda sambamba na kuanzishwa kwa kituo cha utafiti wa zao hilo katika chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Kihinga kilichopo wilayani Kigoma kwa kuwa ndiko zao la Michikichi linalimwa kwa wingi.

Anasema zao la mchikichiki ni muhimu katika ukuzaji wa uchumi wa nchini, hivyo ufufuaji wa zao hilo ni kichocheo cha viwanda kwa kuwa kutakuwa na uhakika wa upatikanaji wa malighafi na kuvutia wawekezaji.

Waziri Mkuu anabainisha kuwa licha ya kuwepo kwa michikichi mingi nchini lakini uzalishaji wake unafanyika kwa njia za kienyeji, hivyo Serikali imedhamiria kuboresha kilimo hicho kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili liweze kuleta manufaa makubwa kwa Taifa na wakulima.

Anasema kuwa Serikali haiwezi ikaendelea kutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza mafuta ya kula kutoka nje wakati uwezo wa kulima michikichi na kuzalisha mafuta ya mawese kwa wingi tunao.

Anasisitiza kwamba inawezekana kujitosheleza kwa mafuta ya kula kwa sababu Tanzania ina ardhi ya nzuri yenye rutuba na watu ambao kilimo ndiyo shughuli kubwa wanayoitegemea kujipatia kipato.

Waziri Mkuu anasema ili kufanikisha kampeni hiyo ni lazima  viongozi wa Serikali wabadilike na wawafuate wakulima kwenye maeneo ya vijijini wakawaelimishe na kuwashauri namna bora ya kulima zao hilo.

“Tunataka kufanya mageuzi makubwa ya zao la michikichi, tunataka tuzalishe mafuta ya kutosha kutokana na zao hili, hivyo tuanze kupanda michikichi mipya na kuiondoa ile ya zamani kwa awamu,”. 

Kadhalika, Waziri Mkuu anasema Serikali inataka kuona mabadiliko ya zao hilo, hivyo amewaagiza Maafisa Ugani katika maeneo yote wanayolima michikichi wafualitie maendeleo ya zao hilo kwa ukaribu zaidi. 

Waziri Mkuu amewataka wananchi wote wa mkoa wa  Kigoma pamoja na mikoa mingine inayolima michikichi, wahakikishe wanapanda michikichi kwa wingi kuanzia kwenye makazi yao na kwenye mashamba yote wanayolima mazao mengine ili kuongeza uzalishaji.

“Serikali imefanya maamuzi ya kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini, kila mmoja lazima awajibike katika kuinua zao la michikichi ili tuweze kuzalisha mafuta ya kutosha,” amesema.

Waziri Mkuu amesema Serikali itafuatilia kwa umakini kuhakikisha zao la michikichi linalimwa kwa wingi na kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla. “Tutumie zao hili kama fursa ya kujikwamua na umasikini pamoja na kumaliza changamoto ya upatikanaji wa mafuta nchini,”.

Pia amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri zote nchi kuhakikisha mashamba ya wananchi yanapimwa na wahusika kupewa hati ili ziwawezeshe kupata dhamana ya mikopo kwenye taasisi mbalimbali za kifedha na kuwekeza kwenye kilimo.

Waziri Mkuu anabainisha kuwa halmashauri zinazolima michikichi viongozi wake wanatakiwa kuanzisha vitalu vya miche ya zao hilo na watakaoshindwa kuanzisha vitalu hivyo pamoja na kuhamasisha kilimo cha michikichi kwenye maeneo yao wajitathimini mwenyewe. 

Anaongeza kuwa kuanzia sasa mkoa huo uhakikishe miche ya michikichi inapandwa katika maeneo yote yakiwemo ya pembezoni mwa barabara, katika mashamba ya shule za msingi na sekondari, kambi ya JKT na kwenye magereza na kwenye makazi ya wananchi.

Hata hivyo Waziri Mkuu alitoa angalizo kwa wawekezaji watakaowekeza katika kilimo cha michikichi kutoanzisha migogoro na wananchi watakaowakuta katika maeneo yao na badala yake washirikiane nao vizuri kwa sababu migogoro haina tija kwao na kwa wananchi.

Waziri Mkuu anasema Serikali imeliteua Gereza la Kwitanga lililopo wilayani Kigoma kuwa kituo kikuu cha uzalishaji wa zao la michikichi nchini kwa kuwa tayari lilishaanza kujishughuliza na kilimo cha zao hilo.

Ameuagiza uongozi wa gereza hilo kuongeza nguvu katika uzalishaji wa michikichi kwa kupanua mashamba na kuongeza askari wenye ujuzi wa kilimo cha michikichi.

Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa Trade Mark East Africa, Bw. John Ulanga alisema walifanya utafiti kuhusu zao la michikichi na walibaini kuwa kuna soko kubwa la mafuta ya mawese ndani ya nchi yetu, pamoja na nchi za jirani ila uzalishaji wa mafuta hayo ndani ya nchi bado ni mdogo sana.

Alisema hali hiyo inachangiwa na kuwepo kwavikwazo vichache vinavyokwamisha ongezeko la uzalishaji wa ndani, ambavyo ni matumizi ya teknologia hafifu katika kilimo cha mchikichi, na ukamuaji  wa mafuta ya mawese.

Pia ukosefu wa miundombinu na usafiri, ukosefu wa maghala ya kukusanyia matunda ngazi ya wilaya, na badala yake mkulima mmoja mmoja anahangaika kupeleka kwa mteja hivyo kumuongezea gharama, ukubwa wa gharama za usafiri kutoka shambani mpaka sokoni.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Josephat Faustine alisema kilimo cha zao la michikichi kina faida kubwa na kinawekezeka, hivyo wao wataanisha maeneo yote yanayofaa kuwekeza. 

Pia Mkurugenzi huyo wa TADB alisema benki yao inauwezo wa kutoa mikopo ya mitaji kwa vituo vya uzalishaji mbegu za zao la michikichi na kumaliza changamoto ya upatikanaji wa mbegu, hivyo ni muhimu kwa wakala wa mbegu kuchangamkia fursa hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad