HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 16, 2018

WANANCHI ZAIDI YA 2000 WANUFAIKA NA MRADI WA MAJI SIMIYU

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akifungua bomba la maji kujiridhisha ikiwa linatoa maji kabla ya kuzindua mradi wa maji wa Lagangabilili wilayani Itilima wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo, Agosti 15, 2018. 
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akimtwisha ndoo ya maji Bi. Perusi Makeleja Mkazi wa Kijiji cha Lagangabilili wilayani Itilima mara baada ya kufungua mradi wa maji utakaowahudumia zaidi ya wananchi 2000, katika mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo leo Agosti 15, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi(kulia) akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Mhe. Dkt. Joseph Chilongani katika kijiji cha Gamabasingu ili Mwenge wa Uhuru uanze mbio zake wilayani Itilima, leo Agosti 15, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akitundika mzinga wa Nyuki wa kisasa katika Shamba darasa la Ufugaji wa Nyuki na Utunzaji wa Mazingira katikaKijiji cha Lagangabilili mara baada ya kukagua shamba darasa hilo wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Agosti 15, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho (wa pili kulia) akiangalia baadhi ya vifaa vya maabara ya Somo la Bailojia katika Shule ya Sekondari Budalabujiga kabla ya kufungua vyumba vitatu vya maabara vya shule hiyo wilayani Itilima, wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo, Agosti 15, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho (kushoto) akizungumza na baadhi ya viongozi na wananchi wa Wilaya ya Itilima mara baada ya kukagua Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo, Agosti 15, 2018.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho akiweka Jiwe la Msingi Maboresho ya Kituo cha Afya Ikindilo wilayani Itilima mkoani Simiyu, wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo, Agosti 15, 2018.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Dkt. Anold Musiba(kulia) akimuongoza Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho kukagua Maboresho ya Kituo cha Afya Ikindilo kabla hajaweka Jiwe la msingi, wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo, Agosti 15, 2018.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Zaidi ya wananchi 2000 wa Kijiji cha Lagangabilili wilayani Itilima Mkoani Simiyu wamenufaika na mradi wa maji safi na salama  na kuondokana na adha ya kutumia muda mrefu kutafuta maji kwa kusogezewa huduma ya maji karibu na makazi yao.

Hayo yamesemwa na Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu, Goodluck Masige wakati akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Francis Kabeho, aliyefika katika mradi wa maji wa Lagangabilili wenye thamani ya shilingi milioni 967, kwa ajili ya kufungua.

Masige amesema Mradi wa Maji wa Lagangabilili ulianza kutekelezwa mwaka 2015 na kukamilika mwaka 2018 na kuanza kutumika huku akibainisha  uwezo wake kuwa, una kisima chenye uwezo wa kutoa maji lita 15,000/= kwa saa, vituo vya kuchotea maji 23 na mtandao wa maji wenye urefu wa mita 29,431.

“Kukamilika kwa mradi huu wakazi  2228 wanapata huduma ya maji safi na salama kwa ajili ya kunywa na matumizi mengineyo,mradi umepunguza muda waliokuwa wanaoutumia wananchi kutafuta maji kwa kuwasogezea huduma ya maji karibu na makazi kwa saa 24,mpaka sasa kaya 25 na taasisi za Umma 20 zimeunganishiwa maji” alisema Masige .

Awali Mkuu wa Wilaya ya Itilima Mhe. Benson Kilangi amesema kuwa tangu Uhuru eneo hilo lilikuwa halina maji kabisa, na baada ya kupatikana kwa huduma hiyo kutapunguza adha ya uhaba wa maji, huku akibainisha kuwa Serikali inategemea  mradi mkubwa kutoka Ziwa Victoria kuwa suluhisho la kudumu la changamoto ya maji ka ajili ya matumizi ya binadamu na wanyama pia.

Perusi Makeleja  mkazi wa Kijiji cha Lagangabilili amesema kukamilika kwa mradi huo kumewapunguzia adha wananchi hususani wanawake ya kusafiri umbali mrefu na kuamka alfajiri kufuata maji lakini umesaidia kupunguza magonjwa.

“Kabla ya mradi huu tulikuwa tunaamka usiku usiku kwenda kutafuta maji mbali tunapishana na fisi njiani, watoto wetu walikuwa wakiugua magonjwa ya tumbo na kuhara kutokana na kunywa maji ambayo hayakuwa salama, , lakini kwa sasa hizo shida hamna tena, tunamshukuru sana Rais Magufuli kwa kutuletea mradi huu sisi Wanalagangabilili” alisema

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Charles Kabeho ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kutatua changamoto za wananchi wake, ambapo katika ujenzi wa mradi huo Serikali ya Tanzania imechangia kiasi cha shilingi milioni 907 huku serikali ya Misri ikichangia kiasi cha shilingi milioni 60 ili kukamilisha ujenzi huo.

Mwenge wa Uhuru ukiwa wilayani Itilima umefungua vyumba vinne vya madarasa shule ya msingi Lagangabilili pamoja na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa maboresho ya kituo cha afya Ikindilo unaojumuisha jengo la wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti na nyumba ya mganga na kukagua Shamba darasa la Ufugaji wa Nyuki na Utunzaji wa Mazingira.

Aidha, kiongozi huyo ariridhishwa na ubora wa majengo ya miradi hiyo, huku akiwapongeza viongozi wa wilaya na Halmasharui kwa usimamizi makini ambapo aliwataka kuhakikisha majengo hayo yanakamilika ujenzi wake na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Katika hatua nyingine akiwa Wilayani Itilima Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2018, Ndg. Charles Kabeho  amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Simiyu  kuendelea kuchangia chakula cha mchana shuleni ili  watoto wapate  Muda wakujisomea zaidi hali itakayosaidia kupunguza utoro.


Mwenge wa Uhuru unaendelea na Mbio zake Mkoani Simiyu ambapo Agosti 15 Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Wilaya yaItilima umepita katika miradi sita yenye thamani ya bilioni 1.6.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad