HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 27, 2018

HAKUNA SEKTA YOYOTE ISIYOHITAJI HIFADHI YA MAZINGIRA - MAKAMBA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akizungumza na wakazi wa kijiji cha Nyamirembe juu ya utayari wao wa kuhifadhi mazingira ya Kisiwa hicho ili kuwa miongoni mwa maeneo yanayopendekezwa kulindwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akikagua maeneo ya Kisiwa cha Magafu, takribani mwendo wa dakika thelathini kutoka mwalo wa Nyamirembe. Waziri Makamba aheahidi kutuma wataalamu ili kujiridhisha zaidi kabla ya kutanga katika gazeti la Serikali.

Siku ya Sita ya ziara ya Waziri Makamba imemfikisha Mkoani Geita, Wilayani Chato katika Kijiji cha Nyamirembe ambapo pamoja na mambo mengine Mhe. Makamba ametembelea Kisiwa cha Magafu na kuahidi kutuma timu ya wataalamu kwa ajili ya kufanya tathmini ya namna ya kulinda kisiwa hicho kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, ikiwa ni eneo tengefu kwa mazalia ya samaki.
Akiongea na Uongozi wa Mkoa wa Geita Waziri Makamba amesema kuwa jitihada za Serikali ni pamoja na kuhakikisha ulinzi madhubuti kwa kisiwa hicho ili kiwe kielelezo cha mandhari tulivu kwa mazalia ya samaki na bioanuai.
Waziri Makamba amesema kuwa hakuna sekta yoyote muhimu kwa uchumi wa nchi isiyohitaji Hifadhi ya Mazingira hivyo Sheria ya Mazingira kifungu namba 51 inatoa mamlaka na nafasi ya kulinda maeneo nyeti na kuainisha kuwa kuna dhana potofu kuwa uhifadhi wa mazingira ni kinyume na maendeleo.
Dhana ya uhifadhi inaendana na utashi, uwezo, utayari na ushirikishwaji wa wananchi wenyewe. “Tunapoongelea uhifadhi tunaamanisha, kuweka utaratibu wa kutumia maeneo yaliyopendekezwa kuhifadhiwa kwa taratibu zitakazopendekezwa, mfano kama tunahifadhi kisiwa, tutaweka utaratibu maalumu wa uvuaji wa samaki katika eneo hilo” Makamba alisisitiza.
Pamoja na mambo mengine Waziri Makamba amesema Ofisi yake iko tayari kuteua wakaguzi wa mazingira kadri iwezekanavyo na kutoa mafunzo kwao pindi majina yatakapowasilishwa kwake na Sekretarieti ya Mkoa.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert  Gabriel Luhumbi amesema kuwa  Mkoa wake kwa asilimi 35 umezungukwa na madini  na kupelekea uharibifu wa Mazingira kutokana na shughuli za uchimbaji hata hivyo Ofisi yake imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika shughuli za uchenjuaji kwa kuhakikisha usalama wa afya za watu na mazingira.
Akielezea jitihada za Mkoa wake katika suala la kuhifadhi mazingira Mhandisi Gabriel amesema wamekuwa na mwendelezo wa kampeni ya upandaji miti kwa kila Halmashauri zote na kutunza miti ya asili, ikiwa ni pamoja kuondoa wavamizi haramu katika misitu, operesheni ambayo ni endelevu. “Huwezi kutenganisha mazingira na uhai wa watu” Mhandisi Gabriel alisisitiza.
Waziri Makamba yuko katika ziara ya kikazi katika Mikoa tisa (8) nchini yenye lengo la kukagua, kutathmini na kuzungumza na viongozi kuhusu maeneo yanayopendekezwa kuhifadhiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira  kifungu namba 51.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad