HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Saturday, 7 July 2018

Wafanyabiashara wahamasishwa kutembelea PPRA kujiunga na Mfumo wa Ununuzi kwa njia ya mtandao - TANePS

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amewahamasisha wanyabiashara na wazabuni kutembelea banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma – PPRA lililopo ndani ya banda la Wizara ya Fedha na Mipango kwenye viwanja vya Sabsaba ili kuelimishwa kuhusu Mfumo mpya wa ununuzi wa Umma kwa njia ya Mtandao (Tanzania National e-Procurement System – TANePS) pamoja na kujisajili kwenye mfumo huo. 

Dkt. Kijaji alitoa wito wakati alipotembelea banda la PPRA na kupatiwa maelezo kuhusu mambo mbalimbali yanayotekelezwa na Mamlaka hiyo ikiwa ni pamoja na namna mfumo huo unavyofanya kazi. Amesema dhamira ya Serikali ni kuondoa malalamiko kwenye manunuzi ya Umma kwa upande wa wazabuni na Umma kwa ujumla kwa kuhakikisha michakato yake inafanyika kwa uwazi na ushindani ili mwisho wa siku ipate thamani halisi ya fedha inayotumika kwenye manunuzi. 

Pia ametoa wito kwa PPRA kuhakikisha taasisi zote za Umma zinaunganishwa kwenye mfumo huo mapema iwezekanavyo. 

Kwa upande wake Mtaalamu wa Mifumo ya Habari wa PPRA Bi. Giftness David alisema, kwa kuanza, mfumo wa TANePS umeanza kutumiwa na taasisi za Umma mia moja kwa ajili ya manunuzi ya dawa, vifaa tiba, bidhaa na huduma mtambuka. Ameongeza kwamba, kwa wakati huu, PPRA imetoa kipao mbele katika kutoa mafunzo kwa watoa huduma (wazabuni) na taasisi nunuzi kuhusu matumizi ya mfumo huo. 


TANePS ni mfumo ulioandaliwa na PPRA ili kukidhi matakwa ya sheria ya ununuzi wa Umma, na unawezesha mchakato mzima wa ununuzi wa bidhaa, vifaa, huduma na kazi za ujenzi kufanyika kwa njia ya mtandao (kielektroniki).

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji akisaini kitabu cha wageni kwenye banda la PPRA
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji akipata maelezo kuhusu shughuli zinazotekelezwa na PPRA kutoka kwa Mtaalam wa Mifumo ya Habari wa Mamlaka hiyo Bi. Giftnes David
Mmoja wa wafanyabiashara walojitokeza kusajiliwa kwenye mfumo wa TANePS akielekezwa namna ya kujisajili na Mtaalam wa Mifumo wa PPRA Bi. Giftnes David
Baadhi ya watumishi wa PPRA wakifurahia matunda ya kazi wanazofanya kwenye banda la Mamlaka hiyo katika viwanja vya Sabasaba

Picha na Emmanuel Massaka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad