HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 18, 2018

SERIKALI KUTOVIVUMILIA VYUO VITAKAVYOTOA MAFUNZO KINYUME NA UTARATIBU

Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii
SERIKALI imesema haitavivumilia  vyuo ambavyo vitabainika vinatoa mafunzo yake kinyume na utaratibu uliowekwa na lengo ni kuhakikisha vijana wanapata elimu bora.

Pia imeiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU), kuongeza kasi ya ukaguzi na kuvifungia vyuo hivyo bila kujali ni vya umma au binafsi na kufafanuliwa Serikali hutenga Sh.bilioni 427.5 kwa ajili ya utoaji wa elimu kwa vyuo vya elimu ya juu nchini, hivyo haitarajii kuona madudu yanafanyika.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakati anafungua maonesho ya 13 ya Vyuo  vya Elimu ya Juu katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali haitaweza kuvumilia uwepo wa vyuo visivyokuwa na sifa nchini kwani vimekuwa ni chanzo vya kuzalisha uwepo wa wanafunzi wasio na sifa.

Prof.Joyce amesema hivi karibuni Serikali  ilifanya ukaguzi kwa baadhi ya vyuo na kubaini kuwepo kwa programu nyingi zilizokuwa zikiendeshwa kinyume cha taratibu.

“Sasa TCU ongezeni kasi ya ukaguzi kwa vyuo vyote nchini na endapo mkibaini viko  baadhi  vinaendesha mafunzo  kinyume cha taratibu zilizoweka aidha kiwe cha Umma au binafsi  fungia mara moja.

“Hatuwezi tukawabaini wanafunzi wasio na sifa miaka yote na kuwepo na vyuo visivyo na sifa kwa sababu kama elimu bora hakuna  hatutaweza kuwa na kizazi kitakachofanishisha adhma ya serikali ya Tanzania ya Viwanda  bali tutakuwa na vijana wanaojihusisha na tabia zisizostahili,”amesema.

Kuhusu mikopo amesema kwa mwaka wa fedha wa 2018\2019 ambapo jumla ya wanafunzi 123,285 watanufaika nao kwa sababu Serikali imetenga kiasi cha sh.bilioni 427.5 kwa ajili ya utoaji wa elimu ya nchini.

Amewataka wanafunzi wa vyuo vya elimu ya  juu kuhakikisha tafiti wanazozifanya ziwe chanzo cha kutatua changamoto za wanyonge nchini.

Kwa upande wa Katibu wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema jumla ya vyuo na taasisi 68 zimeshiriki maonesho hayo ambapo 64 ni vya nchini na vinne nje ya nchi.

Katika Maonesho hayo Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Mzumbe Profesa Ganka Nyamsogoro amesema  katika maonesho ya TCU wamejipanga kwa huduma ya kudahili pale tu wanapotembelea wanafunzi.

"Wanaotaka kujiunga na Chuo Kikuu Mzumbe wakifika watafanya maombi moja kwa moja na maelekezo watapewa na wataalam waliopo katika banda hilo.
 Waziri wa Elimu wa Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza katika Maonesho ya Vyuo vikuu nchini pamoja na vya nje vinavyoshiriki maonesho hayo katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar Salaam.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akipata maelezo katika Chuo Kikuu Mzumbe  pamoja kuangalia jnisi wanafunzi wanapoomba udahili kwa njia ya kieletroniki (hawapo pichani)katika maonesho ya vyuo jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipata maelezo kutoka kwa Afisa Habari Mwandamizi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Venaranda Malima kuhusiana Bodi hiyo katika maonesho ya vyuo Vikuu.
 Wanafuzi wakipata maelezo kutoka kwa  Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano wa Umma wa Taasisi ya Uhasibu Nchini (TIA) Lilian Rugaitika. Kuhusiana na kozi wanazozitoa katika maonesho ya vyuo vikuu jijini Dar es Salaam.
 Afisa Habari Mwandamizi na Uhamasishaji Zawadi Msalla akitoa maelezo wananchi waliotembelea maonesho ya Vyuo Vikuu nchimi.
Mjumbe wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Profesa  Caroline Nombo akipata maelezo kutoka kwa Afisa Habari Mwandamizi wa Bodi  hiyo Venaranda Malima kuhusiana bodi kushiriki maonesho ya vyuo vikuu katika kutoa elimu kwa waombaji mikopo hiyo katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad