HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, July 31, 2018

SERIKALI KUMNYANG’ANYA MOHAMMED ENTERPRISES MASHAMBA

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angeline Mabula (katikati) akimuhoji Meneja anayesimamia Mashamba yote ya mkonge ya kampuni ya Mohammed Enterprises ndugu Newalo Nyari (wapili kushoto) kwanini hawajaendeleza maeneo yao tangu walipokabidhiwa mwaka 2000.

Na Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angeline Mabula amesema serikali imekusudia kuchukua baadhi ya mashamba yanayomilikiwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises na kuwapa wananchi kwa kuwa wameshindwa kutimiza masharti ya endelezaji wake. Mhe. Mabulla amesema hayo baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa mashamba katika Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ambapo amegundua kampuni ya Mohammed Enterprises inamiliki maeneo makubwa sana kwa zaidi ya hekta 9,418 sawa na hekari 20,779 ambayo wamechukulia mkopo kwa ajili ya kupanda mkonge, kitu ambacho hakijafanyika kwa asilimia kubwa.

“Hii kampuni ya Mohammed Enterprises imetupa taarifa ambazo si za kweli kwamba wameendeleza maeneo yao wanayoyamiliki kwa asilimia 83, mimi nimefika katika mashamba yote 14 wanayoyamiliki na nimeona ni eneo kubwa sana ambalo limebaki pori na halijapandwa mkonge tangu wakabidhiwe mwaka 2000 takribani miaka 17 sasa wakati wananchi wa Korogwe wanakosa maeneo ya kulima, kuishi na kufugia” amesema Mhe. Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angeline Mabula (kushoto) akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Handeni aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Godwine Gondwe wakati wakikagua mashamba ya kampuni ya Mohammed Enterprises yasiyoendelezwa katika wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

“kwa sasa Wizara yangu imejiridhisha kwamba kuna haja ya kugawa maeneo yanayomilikiwa na Mohammed Enterprises ambayo hayajendelezwa kwa kupandwa mkonge ili wapewe wananchi wa Korogwe ambao wana uhaba wa ardhi kwa muda mrefu kutokana na maeneo makubwa kumilikiwa na watu wachache”. Mhe. Mabula ameongeza.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angeline Mabulla amefanya ziara ya ukaguzi wa mashamba yote 14 yanayomilikiwa na Kampuni ya Mohammed Enterprises na kugundua kuwa amepanda mkonge eneo dogo sana na sehemu kubwa ni mapori tofauti na taarifa aliyopewa na kampuni hiyo. Waziri pia amesema mashamba hayo yametumika kuchukua mikopo benki lakini mikopo hiyo haijatumika kuendeleza mashamba hayo kitu ambacho kinafanya wananchi wayahitaji maeneo hayo lakini wanashindwa kuyatumia kwa kuwa yanamilikiwa na kampuni ya Mohammed Enterprises.
Mashamba yanayomilikiwa na kampuni ya Mohammed Enterprises yaliyopo kijiji cha Mazinde, Wilayani Korogwe mkoani Tanga yakionekana hayana zao la mkonge kama inavyotakiwa.

Akijatetea mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi Meneja anayesimamia Mashamba yote ya mkonge ya kampuni ya Mohammed Enterprises ndugu Newalo Nyari mesema kwamba si kweli kwamba hawajaendeleza maeneo hayo bali wameendeleza na wamepanda mkonge baadhi ya maeneo na mengine wameyaacha mapori ili kuhifadhi misitu na mengine wanawaachia wananchi waweze kupanda mazao yao ikiwa ni ushirikiano wa kijirani.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni aliyekuwa akikaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Godwine Gondwe ambaye ameonesha kukasirishwa na maneno ya meneja huyo kwamba wameendeleza mashamba hayo wakati yeye mwenyewe ameshuhudia kwa macho yake mashamba yote 14 na kuona hali halisi ya mapori ambayo hayaendelezwa.
Mashamba yanayomilikiwa na kampuni ya Mohammed Enterprises yaliyopo kijiji cha Mazinde, Wilayani Korogwe mkoani Tanga yakionekana ni mapori na hayana zao la mkonge kama inavyotakiwa.

Baadhi ya wananchi wa Korogwe wameonesha kufurahishwa na hatua hiyo ya Serikali ya kuipunguzia umiliki wa baadhi ya maeneo yanayomilikiwa na kampuni ya Mohammed Enterprises ambayo watapewa wananchi hao ili waweze kufanya shughuli zao za maendeleo.

Hata hivyo kwa mujibu wa sheria ya ubatilishaji umiliki wa mashamba ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ndiye mwenye dhamana ya kumyanga’anya mmiliki wa ardhi au mashamba baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Ardhi.
Baadhi ya maeneo ya Mji wa Mombo uliyopo Wilayani Korogwe mkoani Tanga ambayo yapo ndani ya hati miliki ya kampuni ya Mohammed Enterprises ambayo yalitakiwa kulimwa mkonge lakini wananchi wanaishi kwakuwa eneo hilo halikuendelezwa kwa muda mrefu. (Picha zote na Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad